Kituo kikubwa na cha kisasa cha huduma za afya kitakachogharimu Sh. bilioni 10.5 kinatarajiwa kujengwa jijini Dar es Salaam kwa ajili ya kutoa huduma mbalimbali zikiwamo za tiba kwa wananchi na mafunzo kwa wataalam wa kada ya afya.
Mwenyekiti wa Bodi wa Rotary Club Dar es Salaam, Sharmila Bhatt, aliyasema hayo jijini Dar es Salaam jana kwenye mazungumzo yanayoandaliwa mara moja kila mwezi siku ya Alhamis na kampuni ya Solution Blocks.
Bhatt alisema sehemu ya fedha za kukamilisha ujenzi wa kituo hicho kinatarajiwa kupatikana kwenye mbio za marathon (Rotary Dar es Salaam Marathon), zinazotarajiwa kufanyika Siku ya Kumbukumbu ya Nyerere Oktoba 14, mwaka huu jijini Dar es Salaam.
Naye Mwanzilishi wa Solution Blocks, Msomisi Mbenna, alitoa wito kwa mashirika ya ndani, taasisi na watu binafsi kuchangia shughuli na mradi yenye manufaa makubwa kwa jamii kama huo.
“Umefika wakati kwa Watanzania kutoendelea kutegemea michango ya fedha kutoka kwa wafadhili wa nje kugharimia shughuli au malengo yenye manufaa kwa jamii ila inabidi shughuli kama hizi za kuchangia fedha wazifanye wenyewe,” alisema.
No comments:
Post a Comment