Saturday, 19 September 2015

UKAWA KUMSHITAKIMAGUFULI



Wakati kampeni za uchaguzi mkuu zikiendelea kupamba moto huku mchuano mkali ukiwa kati ya mgombea urais Chama cha Mapinduzi (CCM),  Dk. John Magufuli na mgombea wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Edward Lowassa, vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), vinakusudia  kumshtaki mahakamani Dk. Magufuli.



Wengine wanaokusudiwa kushtakiwa ni Bodi ya Wadhamini wa CCM na Timu ya Kampeni ya CCM kwa kosa la kuiba haki miliki ya Chadema ambayo ni M4C.
Vyama vinavyounda Ukawa ni Chadema, NCCR-Mageuzi, Chama cha Wananchi (Cuf) na National League for Democracy (NLD),  vinakusudia kuchukua hatua hiyo kwa madai mgombea urais wa CCM anaiga na kutumia nembo za Chadema kwenye mabango na hotuba zake za kampeni.
Akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam, Mwanasheria wa Chadema, John Mallya, alisema watakwenda kufungua mashtaka hayo dhidi ya CCM, Jumatatu wiki ijayo na kwamba wanasheria wa Ukawa wapo katika hatua za mwisho za kukamilisha taratibu za kisheria.
Alisema lengo la kumshtaki Dk. Magufuli ni kwa kukiuka sheria kwa kutumia nembo za Chadema ambazo chama hicho kina hati miliki nazo.
Alizitaja nembo zinazotumiwa na Dk. Magufuli ambazo ni mali ya Chadema kuwa ni M4C (Movement For Change), ambayo imetafsiriwa kama Magufuli For Change na kauli ya Mabadiliko inayotumiwa na Ukawa ambayo imechukuliwa na mgombea wa CCM kama Mabadiliko Magufuli, Magufuli mabadiliko na kuiba sera na ahadi za ilani ya Chadema na Ukawa.
Chadema katika kampeni zake kimekuwa kikitoa salamu kwa wananchi ya “Lowassa mabadiliko”, “Mabadiliko Lowassa”, kaulimbiu ambayo iliasisiwa na Mwenyekiti wa Taifa wa Chadema, Freeman Mbowe, wakati wa mkutano wa Baraza la Wanawake wa Chadema (Bawacha).
Alisema hujuma nyingine zinazofanywa na chama tawala dhidi ya Ukawa ni kushushwa kwa mabango ya wagombea wake katika maeneo mbalimbali nchini, kupiga kampeni za ukanda dhidi ya Chadema na Ukawa, kukamatwa kwa wagombea wa Ukawa na vitendo vya rushwa vinavyofanywa na baadhi ya wagombea wa CCM.
Kuhusu wizi wa kura, alisema Ukawa umejipanga kwa kuweka walinzi wa Red Brigad 400 kwa kila kata ili kudhibiti wizi wa kura.
Kwa upande wake Afisa Habari wa Chadema, Tumaini Makene, alisema mambo yanayofanywa na CCM, Ukawa ilitegemea Tume ya Taifa ya Uchaguzi (Nec), ingekemea ikiwamo baadhi ya kauli za uchochezi zinazofanywa na baadhi ya viongozi wa chama hicho katika mikutano ya kampeni inayoendelea mikoani.
“Baadhi ya viongozi wa CCM wanaifananisha Tanzania na baadhi ya nchi za Kiarabu kama Libya na Iraq kwamba kunaweza kutokea machafuko wakati wa uchaguzi wa mwaka huu kama ilivyo katika nchi hizo licha ya kwamba Tanzania inafanya siasa za kidemokrasia,” alisema. Makene alisema kauli iliyotolewa na Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi Taifa, Abdallah Bulembo kwamba CCM haiwezi kuachia Ikulu, Nec ilistahili kuchukua hatua kwani kauli hizo zinaashiria kuharibu uchaguzi mkuu wa mwaka huu.
CHANZO: NIPASHE

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!