Mgombea urais kwa tiketi ya CCM, Dk. John Magufuli (pichani), amesema amekomaa kuwa rais wa Tanzania na kwamba haombi achaguliwe kwenda Ikulu kufanya majaribio.
Amesema mafisadi serikalini wana haha kwasababu wanajua msimamo wake kwa watumishi ambao wamekuwa wakiibia serikali na kukwamisha maendeleo ya Watanzania.
Dk. Magufuli aliyasema hayo jana kwa nyakati tofauti kwenye mikutano mbalimbali aliyoifanya njiani wakati akitokea mkoani Kigoma kuelekea Mkoa wa Kagera ambako ameanza kampeni zake leo.
Akiwa wilayani Biharamuro, Dk. Magufuli alisema amekuwa waziri kwa miaka 15 mfululizo hivyo amekomaa vya kutosha kuwaongoza Watanzania katika maendeleo ya kweli yatakayowaletea maisha bora.
“Ikulu si pakwenda kufanya majaribio, mimi natosha kwasababu nimepata uzoefu wa miaka mingi, kote nilikofanyakazi sikuwahi kufukuzwa kazi wala kukumbwa na kashfa yoyote ile, wengine wanapewa uwaziri mwaka mmoja tu wanafukuzwa lakini mimi sikuwahi kufukuzwa kazi naomba mniamini,” alisema.
Aidha, alisema hatakuwa na `blah blah’ katika kuwatumikia Watanzania hivyo aliahidi kuchagua mawaziri wachapakazi ambao watafanyakazi usiku na mchana kuhakikisha kero nyingi za Watanzania zinashughulikiwa kwa wakati.
Aliwaambia wananchi hao kuwa akichaguliwa kuingia Ikulu atakuwa mtumishi wa wote bila kujadili itikadi za vyama vya siasa hivyo aliwaomba Watanzania wa vyama vyote vya siasa wamchague kwa wingi ili aweze kuwaondolea kero zao.
Alisema kama kwenye serikali zilizopita alikuwa akifanyakazi kwa kuagizwa na wakubwa zake na aliweza kufanyakazi nzuri hivyo akiingia Ikulu atakuwa anawaagiza mawaziri ambao hatakubali wampelekee visingizio mbalimbali.
Akiwa katika jimbo la Buyungu, Dk. Magufuli aliwaahidi kuwajengea wananchi wa eneo hilo kilomita tano za lami pamoja na kujenga barabara ya kutoka Kakonko-Kibondo-Kasulu hadi Manyovu Kigoma kwa kiwango cha lami.
Katika maeneo mengi alikopita, Dk. Magufuli aliwaahidi wananchi wa maeneo hayo huduma za maji, umeme, barabara na huduma bora za afya kuwa akiingia madarakani atahakikisha hospitali za serikali zinakuwa na dawa za kutosha.
Aliwaambia wananchi wa maeneo hayo kwamba iwapo watamchagua na kuingia IKulu tatizo la hospitali za serikali kukosa dawa lipatiwa ufumbuzi ndani ya muda mfupi.
Amon Mpanju, mlemavu wa macho ambaye anaambatana na Dk. Magufuli alimwelezea mgombea huyo kwamba ni mzalendo wa kweli na ambaye amelitumikia taaifa kwa uaminifu mkubwa.
Alisema wagombea wengine hawana sifa zinazoweza kumfikia mgombea wa CCM na hawana rekodi nzuri ya uchapakazi na uadilifu.
Akiwahutubia wananchi wa Biharamulo Dk. Magufuli alisema yeye ni rafiki mkubwa wa wafanyakazi lakini ameshangazwa na watu ambao wamekuwa wakimchonganisha na watumishi wa serikali kwamba akiingia madarakani atawashughulikia na watapata shida.
Amesema watumishi waadilifu na ambao wamekuwa wakifanyakazi zao kwa ufanisi hawana haja ya kumwogopa kwasababu akiingia Ikulu atapambana na watumishi wezi, wala rushwa na wenye tabia ya kuwaambia wananchi njoo kesho.
Aliyasema hayo jana kwenye viwanja vya Biharamulo mkoani kagera katika mkutano wake wa kwanza wa kampeni akitokea mkoani Kugoma.
“Kuna watu wanadhani mimi nafanya siasa, nawahakikishia watu wa Bihalamuro kwamba sifanyi siasa, mimi nikisema nimesema na nikiamua mimi natimiza maana mimi hapa ni kazi tu, nafahamu sehemu za kupata fedha nitaziba mianya ya rushwa na sehemu zinazovuja fedha za umma,” alisema.
Dk. Magufuli alisema akichaguliwa kuwa rais ataendelea kuhubiri amani kwani ikitoweka hakuna Mtanzania ambaye atakuwa salama na kukumbusha namna ambavyo wananchi wa Rwanda na Burundi walivyoteseka baada ya kupoteza amani.
Aliwataka Watanzania kuacha kuwakaribisha watu wabaya na kuwa wawe na kawaida ya kutoa taarifa kwenye vyombo vya usalama pale wanapowatilia shaka watu ambao nyendo zao wanazitilia mashaka ikiwa ni jitihada za kulinda usalama wa nchi.
CHANZO: NIPASHE
No comments:
Post a Comment