Thursday, 20 August 2015

TANESCO lawamani, yakata Umeme bila taarifa, yabainika Mikoa mingi iko kwenye hali tete

Makao makuu ya Shirika la Umeme Tanzania yaliyopo Ubungo, jijini Dar es Salaam. Picha na Maktaba
KERO ya kukatika katika kwa umeme kumewachosha wakazi wa mikoa mingi nchini na kuwafanya kulilalamikia Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco), kuwa kitendo hicho cha kukatika kwa umeme nyakati za asubuhi, mchana na usiku kumesababisha kuibuka kwa kasi ya kuungua vifaa mbalimbali katika maeneo yao.

Aidha, wakati nishati hiyo ikikatika katika maeneo mengi ya nchi, kumekuwepo na vitendo vya wizi wa umeme ambavyo vimeendelea kukithiri na hivyo kuilazimu Tanesco kuanzisha msako mkali kwa watu waliojiunganishia umeme kinyume cha sheria katika vibanda vya biashara na nyumba za kuishi ikiwa ni hatua ya kuwabaini watu ambao wamekuwa wakitumia umeme bila malipo.

Baadhi ya wakazi wa Jiji la Mbeya wameiambia FikraPevu kuwa kukatika huko kwa umeme kunasababisha giza zito na baadhi ya vitu vyao kama majokofu na vitu vingine vinavyotumia umeme, kuharibika. Kero zingine ni ya wanafunzi kushindwa kujisomea na hata kuangalia taarifa za habari katika Televisheni katika nyakati tofauti hususani usiku.
Mmoja wa wakazi wa Jiji hilo akiwemo aliyejitambulisha kwa jina la Solomoni Selemani, amebainisha kwa takribani majuma mawili sasa, kumekuwepo na tatizo hilo. Licha ya kuelezea hal hiyo amesema kuwa Tanesco wangetakiwa kutoa taarifa kwa wananchi kuhusu katizo hilo la umeme kwani tatizo hilo linafanya wawe na hofu juu ya kuharibika kwa vifaa vyao vinavyotumia nishati hiyo ikiwemo kuungua kwa nyumba zao. Wamewataka wawakilishi wao kufuatilia suala hilo na kuwapa taarifa sahihi ya kinachoendelea.
Tatizo la kukatika kwa umeme mkoani Mbeya limekuwa sugu, ambapo katika baadhi ya Wilaya ikiwemo Kyela na Mbeya Vijijini umeme hupatikana kwa saa chache za mchana na nyakati za usiku, hali inayotajwa kukwamisha shughuli nyingi za uzalishaji.
Meneja wa Tanesco mkoani humo, Mhandisi Amosi Maganga, amekiri kuwepo kwa tatizo la umeme ambalo amesema linasababishwa na matengenezo makubwa ya mfumo wa usafirishaji na usafirishaji wa nishati hiyo.
Hata hivyo, amesema hatua hiyo inalenga kuondoa nguzo zilizooza, kufunga vikombe vya nyaya mpya, ikiwa ni maandalizi ya kutumia umeme wa gesi katika gridi ya taifa.
Uchunguzi uliofanywa na timu ya waandishi wetu katika maeneo mbalimbali nchini, umeonyesha kwamba maeneo mengi yamekumbwa na kero hiyo tangu wiki moja iliyopita mpaka leo huku wahusika wakishindwa kutoa taarifa ya nini kinachosababisha kero hiyo ya kukatika kwa umeme.
Baadhi ya mikoa, hususani iliyoko pembezoni mwa nchini, imebainika kuwa imekuwa ikipata nishati hiyo kwa uhakika kutokana na kuunganishwa na umeme wa nchi jirani au mikoa inayokaribiana na mabwaya ya umeme likiwemo bwawa la kuzalisha umeme la Mtera.
Mkoani Arusha imeripotiwa kuwa wafanyabiashara wa barafu, samaki, nyama kwenye bucha na katika baadhi ya maeneo ya majiji na mikoa, wamekuwa wakifunga biashara zao na kuzifungua kwa muda maalumu kutokana na kukosekana kwa umeme wa uhakika.
Afisa Uhusiano wa Tanesco mkoa wa Arusha, Fredy Robert, amekiri kuwepo kwa tatizo hilo ingawa hakutaja sababu za kukatika kwa umeme huku akisema maelezo mengine juu ya tatizo hilo atazitoa kwa maandishi.
Mmoja wa wafanyabiashara wa bucha ya kuuzia nyama ya Ng'ombe katika maeneo ya Kimara Mwisho Jijini Dar es Salaam, akiwemo, Alfredi Bakari, amesema analazimika kununua nyama kidogo ili aweze kuiuza yote akihofia isiharibike. 
Katika maeneo hayo, kumekuwa na kelele za jenereta katika baadhi ya maduka huku wafanyabiashara wengine wakifanya biashara ya jenereta kwa kasi kubwa.
Mathalani, Wilaya zote za Mkoa wa Mwanza ni miongoni mwa zile zinazoendelea kuonja adha hiyo ya kukosekana kwa nishati ya umeme, kwa kukatiwa umeme mara kwa mara ambapo imeelezwa kuwa maeneo mengi huwa gizani kwa muda mrefu hasa nyakati za usiku.
Kukatika huko kwa umeme kumesababisha malalamiko kutoka kwa wananchi ambao wamedai kuwa Tanesco ilistahili kutoa taarifa ili waweze kujiandaa na hali hiyo.
Akizungumzia hali hiyo kwa Mkoa wa Mwanza, Mhandisi wa Umeme wa Mkoa Mwanza, Dastun Ndamugoba, ameiambiaFikraPevu kwamba tatizo hilo limetokana na hitilafu kwenye mashine za uzalishaji umeme kwenye Bwawa la Mtera.
Wakati haya ya kitokea, watu 9 wakazi wa Butiama na Magunga katika Wilaya ya Butiama mkoani Mara, wanashikiliwa na Polisi kwa tuhuma za kukutwa wakiwa wamejiunganishia umeme kinyume cha sheria katika vibanda vya biashara na nyumba za kuishi.
Maofisa Usalama wa Tanesco mkoani humo, wamesema shirika hilo limepata hasara ya zaidi ya shilingi milioni tatu kutokana na wizi wa nishati hiyo kati ya mwezi Aprili hadi Agosti 14, 2015.
Wakizungumza na mwandishi wetu mmoja wa maofisa hao aliyejitambulisha kwa jina la, Sospiter Kaswahili, amesema wamewakamata watu hao katika makazi yao na sehemu zao za biashara wakati walipoendesha msako wa kuwasaka wezi wa umeme nyumba kwa nyumba na kwenye maeneo ya biashara.
Aidha, maofisa hao wamesema kuwa vitendo vya wizi wa umeme vimeendelea kukithiri mikoani, hivyo wameamua kuanza msako huo ikiwa ni hatua ya kuwabaini watu ambao wamekuwa wakitumia umeme bila malipo.
Maduka sita yanayozunguka Soko Kuu la Morogoro, hivi karibuni yaliteketea kwa moto kutokana na hitilafu ya umeme na kuwasababishia hasara wafanyabiashara ambayo thamani yake hadi sasa haijajulikana.
Kwa mujibu wa Jeshi la Polisi mkoani humo, moto huo ulianzia kwenye duka la mmoja wao wafanyabiashara hao usiku wa kuamkia ASgosti 12, 2105 baada ya (Tanesco) Mkoa wa Morogoro, kurejesha umeme wakati ukiwa umekatwa bila taarifa.
Ofisa Uhusiano wa Tanesco Mkoa wa Morogoro, Marcio Semfukwe, alithibitisha moto huo kusababishwa na hitilafu ya umeme ambayo huenda imesababishwa na mmoja wa wafanyabiashara hao kuunganisha nishati hiyo bila kibali cha shirika hilo.
Msemaji wa Shirika la Tanesco, Adrian Severin, alipotafutwa na FikraPevu ili pamoja na mambo mengine aweze kutolea ufafanuzi wa malalamiko hayo hakupatikana mara moja ingawa juhudi za kumtafuta bado zinaendelea.
Uchunguzi unaonyesha tatizo la kukatika kwa umeme nchini linatokana na marekebisho ya mitambo ya Tanesco katika maeneo mengi nchini, hali inayosababisha kukatika mara kwa mara kwa nishati hiyo.
Kumekuwepo na mjadala mzito unaondelea katika mtandao maarufu wa kijamii nchini wa JamiiForums, ambapo baadhi ya wanachama wa mtandao huo wamesema hadi kufikia leo Agosti 18, 2015 katika maeneo mengi (waliyopo nchini) umeme pia hakuna.

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!