Thursday, 20 August 2015

HATUA ZA HARAKA ZINAHITAJIKA KUDHIBITI KIPINDUPINDU JIJINI DAR


WIKI hii katika Wilaya ya Kinondoni, mkoani Dar es Salaam kumeripotiwa kuibuka kwa ugonjwa wa kipindupindu na tayari watu wawili wameshapoteza maisha kutokana na ugonjwa huo.

Mbali na waliokufa, wengine zaidi ya 30 wamelazwa katika Hospitali za Mwananyamala na Sinza zilizopo kwenye wilaya hiyo ya Kinondoni yenye watu wengi zaidi katika mkoa wa Dar es Salaam.
Ugonjwa huu katika jiji la Dar es Salaam umekuwa kama makazi yake, kwani haipiti miaka miwili utasikia umeibuka tena na watu kuugua na hata wengine kupoteza maisha. Huu ni ugonjwa unaohusishwa na uchafu.
Kwa maana hiyo jiji la Dar es Salaam bado ni chafu kuanzia mazingira ya mitaani hadi majumbani wanakoishi watu. Katika mitaa ya jiji la Dar es Salaam hakuna utaratibu mzuri wa uzoaji taka, tatizo linaloanzia kwenye Manispaa husika katika kandarasi za kampuni za taka hadi wananchi wenyewe.
Tunashuhudia pia katika maeneo mengi kama Buguruni, Tandale na hata Kariakoo, takataka zikiwa zimezagaa mtaani kwenye majalala na hata barabarani bila kuzolewa na kandarasi husika na licha ya watu kulalamika bado hatuoni hatua zikichukuliwa.
Taka za majumbani zinapokaa muda mrefu mtaani zinaleta nzi na watoto wanapochezea ni rahisi kuchanganyika na chakula hivyo kuleta kipindupindu. Katika migahawa na mahoteli tunaona vyakula vinapikwa kwenye mazingira ya uchafu na ukaguzi unaopaswa kufanywa na maofisa wa afya unafanywa kwa kiwango kidogo sana na maeneo mengi haufanywi kabisa, hivyo hapo kipindupindu kinazidi kupata nafasi ya kusambaa.
Nako katika maeneo hasa yasiyopimwa na yenye msongamano mkubwa wa watu kuna tatizo la uchafu kwenye vyoo huku mitaani maji yanaachwa yakitiririka ovyo na wakati wa mvua maji hayo majitaka yanatapishwa barabarani huku katika maeneo mengi ya jiji yakiwa hayana mfumo mzuri wa kuondoa maji taka majumbani.
Kwenye kata ambako tunaamini ndipo kwenye watendaji walio karibu kabisa na wananchi na wanafahamu kwa ukaribu uchafu wote unaoendelea kumekuwa kimya. Maofisa afya wa kata hawafanyi kazi zao inavyopaswa.
Katika kuepuka ugonjwa huu wa kipindupindu usiendelee kusambaa katika jiji la Dar es Salaam, tunaomba Manispaa zote za jiji zichukue hatua kuanzia ngazi ya chini kwa kuhakikisha kuna usafi kuanzia majumbani na mitaani.
Kila nyumba kupigwe dawa kwenye vyoo, madimbwi na maofisa afya wapitie kila nyumba kukagua usafi kama ilivyokuwa katika miaka ya nyuma. Ni muhimu kandarasi husika zizoe taka, lakini pia wananchi wenyewe wahakikishe wanakuwa wasafi na kutupa taka sehemu zinazostahili au kuzichoma moto.
Kipindupindu kinaenea sana sehemu zenye uchafu hivyo suala la usafi likizingatiwa ugonjwa huu hautasambaa. Wananchi na watoto wao pia wahakikishe wanakunywa maji yaliyochemshwa majumbani na kuepuka kula vyakula njiani hasa vilivyopoa au vinavyoonekana kuuzwa katika mazingira machafu na bila kufunikwa.
Kila ugonjwa wa kipindupindu unapoingia Dar es Salaam kuna maeneo yanaonekana ni kawaida kukumbwa na ugonjwa huo kama Tandale, Vingunguti, Manzese, Mwananyamala, Tandika na Buguruni.
Hali hii inaonesha kwamba kwenye maeneo haya na mengine maarufu kwa ugonjwa huu, kunahitajika kuangaliwa kwa jicho la tatu na kufuatiliwa kwa ukaribu zaidi. Sisi tunaamini manispaa zote tatu za jiji la Dar es Salaam zitakapochukua juhudi za makusudi kuhakikisha jiji linakuwa safi kuanzia mazingira ya mitaani, majumbani na kudhibiti biashara zisizozingatia usafi, ugonjwa wa kipindupindu utatokomea.

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!