Rais Jakaya Kikwete anatarajia kuwaaga marais wa nchi wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (Sadc) Agosti 18, mwaka huu.
Hafla ya kuwaaga kwake ni moja ya shughuli zitakazofanyika katika kilele cha mkutano wa wakuu wa jumuiya hiyo ambao maandalizi yake yalianza Agosti 6, mwaka huu katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Gaborone (GICC), Botswana.
Wakuu wa nchi na serikali wa Sadc watakaohudhuria mkutano wa 35 wa viongozi hao wanatarajiwa kuwasili jijini Gaborone Agosti 16, mwaka huu.
Ratiba ya mkutano huo inaonyesha kuwa Rais Kikwete atawaaga wakuu hao majira ya jioni kabla ya Rais mpya wa Sadc, Rais Seretse Khama wa Botswana kuufunga rasmi mkutano huo.
Rais Khama anatarajiwa kuwa Mwenyekiti wa Sadc kufuatia kumalizika kwa kipindi cha mwaka mmoja cha uongozi wa mtangulizi wake, Rais Robert Mugabe wa Zimbabwe. Nafasi hiyo inazunguka kwa kila Rais ama Mkuu wa serikali za nchi wanachama wa Sadc.
Mbali na Kikwete kuwaaga viongozi hao, ratiba hiyo inaonyesha kuwapo kwa mikutano ya maofisa wa ngazi za juu, baraza la mawaziri wa nchi za Sadc, mkutano wa marais na hotuba za viongozi mbalimbali wa jumuiya hiyo.
Pia washindi wa mashindano ya umahiri wa uandishi wa habari na insha kwa wanafunzi wa shule za sekondari katika ukanda wa Sadc watakabidhiwa zawadi zao.
No comments:
Post a Comment