Wednesday, 12 August 2015

FAINI ZOTE ZA MAKOSA YA BARABARANI KULIPWA BENKI

Rais Jakaya Kikwete, ameliagiza Baraza la Taifa la Usalama Barabarani kuanzisha mfumo wa ulipaji faini za makosa ya madereva kwa njia ya benki na mitandao ya simu za mkononi, ili kupunguza ushawishi wa rushwa kwa askari wa Kikosi cha Usalama Barabarani.

Rais Kikwete alitoa agizo hilo wiki hii wakati akizindua Wiki ya Nenda kwa Usalama Barabarani mjini Tanga, ambayo mwaka huu kaulimbiu ni ‘Endesha Salama, Okoa Maisha’.
Kauli ya Rais Kikwete imekuja katika kipindi ambacho faini za makosa ya barabarani zimekuwa kero, kutokana na askari wa kikosi cha usalama kuchukulia suala hilo kama mradi wa kujitengenezea kipato.
Askari hao wanaonekana kama wamepangiwa kiwango cha kukusanya faini hizo na hivyo badala ya kufanya kazi ya kuzuia makosa yasitokee au kutoa elimu kwa madereva, sasa wanawategea wakosee ili wawatoze faini, au wanatafuta makosa ya kulazimisha ili wapate sababu ya kulipisha faini.
Matokeo yake, askari wengi hujificha kwenye barabara ambazo hazina matatizo ya foleni ili wapate mwanya wa kusimamisha magari mengi kwa wakati mmoja na kutoza faini kila dereva ili wafikie kile kinachoonekana kuwa ni ‘malengo ya siku’.
Kwa kuwa wengi huenda kwenye barabara zisizo na misongamano ili wapate kufanya vizuri kazi ya kutoza faini, barabara zenye misongamano hukosa msimamizi, kwenye maeneo ya vituo madereva hujifanyia watakavyo bila ya kujali magari mengine na kusababisha misongamano mikubwa zaidi.
Mbali na askari kujali kukamata magari badala ya kufanya kazi ya kuzuia makosa na kuelimisha, faini hizo zimekuwa kama silaha kubwa ya kusumbua madereva kwa kuwa ni lazima askari aliyemkamata dereva alipwe papo hapo na kama hana fedha basi aache gari.
‘Hukumu’ hizo zimekuwa kero kubwa kwa madereva kwa kuwa siyo wakati wote wanatembea na fedha kwa ajili ya kulipa faini, na hivyo hali hiyo husababisha madereva waanze kuwabembeleza askari na hatimaye hupunguza kiwango cha faini na hivyo fedha kutoenda mahali zilikokusudiwa, kwa maana nyingine ni rushwa.
Fomu zile za kutaarifu kosa, zinaeleza bayana kuwa fedha zinatakiwa zilipwe wapi, lakini askari wamekuwa wakijitetea kuwa wameagiza kuwa dhamana pekee inayoweza kuwahakikishia kuwa faini italipwa ni gari na hivyo hawawezi kufanya uamuzi mwingine.
Matokeo yake madereva wamekuwa wakinyanyasika bila ya kuwa na mtetezi, kwa kuwa askari wa barabarani wamekuwa miungu watu, kutokana na ukweli kuwa wanaweza kumtibulia mtu mipango yake ya siku nzima kwa kosa dogo iwapo hataweza kulipa faini.
Tunapenda kumpongeza Rais Kikwete kwa kuliona hilo, ni matarajio yetu wahusika washughulikie kwa haraka kutafuta mfumo mzuri utakaowezesha faini kulipwa bila ya madereva kunyanyasika.
Hii pia italisaidia Jeshi la Polisi kukusanya kwa uhakika zaidi mapato yatokanayo na faini za makosa ya barabarani badala ya mfumo wa sasa ambao unatoa mwanya kwa askari kuchapisha vitabu vyao na kulikosesha jeshi hilo mapato.
Pia, wito wetu kwa Jeshi la Polisi ni kulitaka lijikite katika kuhakikisha linasimamia vyema sheria za barabarani na kutoa elimu kwa madereva badala ya kuwategea wakosee.
Makosa ya barabara yanaweza kupungua kwa kiasi kikubwa iwapo elimu ya sheria za barabarani itatolewa bila ya kuchoka kwa kuwa siyo nia ya Kikosi cha Usalama Barabarani kukusanya fedha kutokana na makosa ya madereva, bali kuhakikisha makosa hayo yanapungua kwa kiwango kikubwa.

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!