Saturday, 1 August 2015

NEC YAANZA KUTOA FOMU KUGOMBEA URAIS


Tume ya Taifa ya Uchaguzi (Nec), imetoa ratiba ya uchukuaji fomu za kugombea urais itayakoanza leo, jijini Dar es Salaam.

Wagombea wa vyama vya United Peoples Democratic (UPDP), Tanzania Labour Party (TLP)  na Democratic Party (DP) wametajwa kuanza kuchukua fomu hizo leo katika mchakato unaotarajiwa kumalizika Agosti 21.
Mwenyekiti wa Tume, Jaji Damian Lubuva, aliyasema hayo jana jijini Dar es Salaam, wakati akizungumza na waandishi wa habari.
Alisema chama cha UPDP kitakuwa cha kwanza kuchukua saa 3 asubuhi, kikifuatiwa na TLP, saa 6 na DP saa 8 mchana.
Alisema Jumanne ya wiki ijayo saa 6 mchana Chama Cha Mapinduzi (CCM), kitachukua fomu chini ya mgombea wa kiti cha Urais Dk. John Magufuli.
Alisema siku inayofuata mgombea Urais wa Chama cha Alliance For Democratic Change (ADC), saa 4 asubuhi na Agosti 17, Chama cha Tadea kitachukua saa 4 asubuhi.
Alisema chama cha mwisho ni kitakuwa ni Alliance for Change and Transparency (ACT) ambaye mgombea wake atawasili  saa 3:00.
Alisema vyama vyote vinaruhusiwa kuja na wanachama wao kushangilia, lakini hawataruhusiwa kufika karibu na ofisi za Tume.
Mkuu wa Idara ya Uendeshaji Uchaguzi, Clothilde Komba, alisema kuwa siku ya mwisho ya uchukuaji fomu itakuwa ni Agosti 21 jioni ambapo fomu ya udiwani ni Sh. 5,000 na ubunge ni 50,000.
Wagombea Urais watatakiwa kuchukua fomu mapema kwa sababu wanatakiwa kupita katika mikoa isiyopungua 10 ambapo kati yake miwili itoke Visiwani na kuwa na wadhamini 200.
Jaji Lubuva alisema kwa mujibu wa Katiba ya mwaka 1977 Ibara ya 20 na 21, kila mwananchi anayo haki na uhuru wa kushiriki shughuli za utawala wa nchi ikiwa ni pamoja na haki ya kuchagua na kuchaguliwa au kuanzisha na kujiunga na vyama vya siasa.
Aidha, alisema shughuli hizo zimeweka mipaka chini ya Ibara ya 30 ya katiba kwamba haki ya kushiriki isifanywe kwa namna ya kuingilia kati ya kukatizwa kwa haki na uhuru wa watu wengine au maslahi ya Umma.
Alisema Tume itafuatilia mchakato wote na wale watakaokiuka na kusababisha vurugu hatua za kisheria zitachukuliwa.
Aliwataka wagombea wa nafasi hizo kuzingatia maadili ya uchaguzi waliyotia saini wiki hii kwenye ukumbi wa tume.
Alisema katika mchakato huo, jeshi la polisi litalinda usalama  na kusisitiza kuwa lengo si kutisha watu bali kuzuia uhalifu.
Kuhusu malipo ya fomu hiyo, Jaji Lubuva alisema ya Urais haitakuwa na malipo wakati wa uchukuaji, lakini watakapozirejesha wahusika watatakiwa kutoa dhamana ya Shilingi milioni moja.
Kamanda wa Polisi wa Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Kamishna Suleiman Kova, aliwataka wachukua fomu za Urais watumie barabara ya Obama wakiwa na wafuasi wao na watakapofika viwanja vya Gim Khana wawaache hapo, kisha baadaye wawapitie waendelee na shamrashamra zao.
Kuhusu matumizi mabaya ya namba iliyotolewa na Dk Karia,  alisema matamshi yanayosambaa kwenye mitandao ni uchochezi na jeshi lake limejipanga na linauwezo wa kumpata aliyefanya hivyo.

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!