Dar es Salaam. Idadi ya watu waliopoteza maisha kutokana na ugonjwa wa kipindupindu ulioikumba Dar es Salaam, imeongezeka na kufikia watatu.
Mgonjwa wa tatu alipoteza maisha jana huku wengine wawili wakifariki dunia juzi. Hadi sasa wagonjwa 34 wamelazwa wakisubiri vipimo kujiridhisha kama wana ugonjwa huo.
Wagonjwa wanne waliokuwa wamelazwa kwenye Hospitali ya Mwananyama vipimo vyao vimeonyesha kuwa wana ugonjwa huo na wamehamishiwa kwenye kambi maalumu iliyoko katika hospitali hiyo. Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Paul Makonda alisema jana: “Tunachofanya ni kutoa elimu kwa wananchi kupitia mabwana na mabibi afya, ili kuhakikisha wagonjwa hawaongezeki, ikiwezekana kuzuia kabisa maambukizi mapya kwa namna yoyote ile.”
Makonda alisema ofisi yake inaboresha kambi iliyopo kwenye Kituo cha Sinza Palestina ili kuwaweka wagonjwa watakaogundulika kuwa na ugonjwa huo kutoka maeneo jirani na hapo.
Mganga Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Aziz Msuya, alisema kambi maalumu kwa ajili ya wagonjwa hao ya Mburahati ipo tayari na wameshahamishia ikiwa tayari na wagonjwa 11 kutoka Mwananyamala.
No comments:
Post a Comment