Watu watano wa familia moja wilayani Ludewa, mkoa wa Njombe, wamefariki dunia na wengine wawili kujeruhiwa baada ya gari dogo aina ya Toyota Cresta walilokuwa wamepanda kuacha njia na kutumbukia mtoni.
Ajali hiyo ilitokea juzi majira ya saa tano asubuhi katika Kijiji cha Shaurimoyo kata ya Lugarawa wakati ndugu hao walipokuwa wakitoka Lugarawa kwenda Shaurimoyo.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Njombe, Willbroad Mutafungwa jana aliwataja waliopoteza maisha kuwa ni dereva, Aaron Haule (40), Wenslaus Tweve (40) Pendo Mbawala (29), Editha Mtega (35) na Paschal Mlwilo (22) wote wakazi wa Lugarawa.
Aiwataja waliojeruhiwa kuwa ni Huruma Mwinuka na Gerado Mwinuka ambao wamelazwa katika Hospitali ya Misheni ya Lugarawa.
“Dereva alishindwa kulimudu gari kwenye kona, likatumbukia mtoni,” alisema Kamanda Mutafungwa na kuongeza kuwa chanzo cha ajali hiyo ni mwendo kasi.
Katika tukio jingine, mtoto wa miaka miwili, Joshua Sepi katika Kijiji cha Malemburi kata ya Mang’oto wilaya ya Makete amefariki dunia baada ya nyumba aliyokuwa amelala kuchomwa moto.
Kamanda Mutafungwa alisema chanzo cha tukio hilo ni wivu wa kimapenzi.
Alisema mtuhumiwa alikuwa anamtuhumu mama wa mtoto huyo kuwa anatembea na mumewe.
No comments:
Post a Comment