Sunday, 5 July 2015

SIKUTUMIA JINA LA MTUME KUMFANANISHA NA LOWASSA- MADABIDA




MWENYEKITI wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Mkoa wa Dar es Salaam, Bw. Ramadhan Madabida, amekanusha madai yaliyotolewa na Taasisi ya Kiislamu ya Imamu Bukhary iliyodai amemdhalilisha Mtume Muhammad (S.A.W), kwa kumfananisha na Waziri Mkuu   mstaafu, Bw. Edward Lowassa.



Taasisi hiyo imekitaka CCM, kumuwajibisha Bw. Madabida kwa kumvua cheo hicho ili Waislamu nchini wajiridhishe kwamba kitendo chake cha kumdhalilisha Mtume si maneno ya CCM.

Akijibu madai hayo, Bw. Madabida alisema tuhuma hizo si za kweli kama inavyodaiwa na taasisi hiyo ambapo Juni 6, mwaka huu, alimpokea Bw. Lowassa ambaye alikuwa akitafuta wadhamini kwa ajili ya safari yake ya urais na kuzungumza maneno bila kumfananisha na Mtume.

Alisema siku hiyo alimwambia Bw. Lowassa, katika safari yake ya kutaka kuingia Ikulu, atakutana na mitihani mingi ambayo ni kawaida kumkuta binadamu yeyote, manabii na mitume hivyo anapaswa kurejea kwa Mwenyezi Mungu amuelekeze cha kufanya ili kuishinda mitihani hiyo.

"Nilisema CCM ni chama makini chenye viongozi makini na wanachama wake hawajamsahau Lowassa, baada ya hapo nilimwambia asimame na kusalimia wana CCM...lipo gazeti moja linalotoka kila siku (si Majira), likaandika namfananisha Lowassa na Mtume jambo ambalo sikusema.

"CCM hakiwezi kunichukulia hatua kwa sababu hicho kinachosemwa sikukisema, hii taasisi haijaniita kunieleza malalamiko yao hivyo walichokifanya ni kinyume na mafundisho ya dini," alisema.

Aliongeza kuwa, katika Kitabu cha Quran, sura ya 48, aya ya sita, Mwenyezi Mungu anasema; "Enyi mlioamini, akikujieni mpotovu na habari yoyote ichunguzeni msije mkawasibu watu kwa kutokujua na mkawa wenye kujuta kwa mliyoyatenda", ambapo wao kama taasisi ya dini, ilipaswa kuzingatia hayo lakini haikufanya hivyo badala yake wamemtuhumu na kumhukumu.

Alisema madhara kwa taasisi hiyo yanapatikana kwenye maneno ya Mwenyezi Mungu sura ya 24, aya ya 15 inayosema; "Mlipoyapokea kwa ndimi zenu na mkasema kwa vinywa vyenu msiyoyajua na kufikiri ni jambo dogo, mbele ya Mwenyezi Mungu ni kubwa".

"Sura ya 16, aya ya 105, inasema wanaozua uwongo ni wale tu wasioziamini ishara za Mwenyezi Mungu na hao ndio waongo," alisisitiza Bw. Mabadiba katika majibu yake.

Awali Mwenyekiti wa Taasisi hiyo, Shekhe Khalifa Khamis, alilaani kitendo na kumtaka Bw. Madabida kutamka hadharani kwa kufuta kauli yake na asirudie kutumia Quran kwa kutunga tafsiri potofu.

Alisema haelewi kwanini Bw. Madabida aliamua kumdhalilisha Mtume ambapo taasisi hiyo ilikutana Juni 29, mwaka huu na kulijadili jambo hilo.

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!