MATUKIO mengi ya kikatili dhidi ya watoto yanayotokea katika Wilaya ya Mpwapwa mkoani Dodoma yanasababishwa na migongano katika familia.
Ukatili dhidi ya watoto ni miongoni mwa mambo ambayo yamekuwa yakipigiwa kelele ili kuhakikisha kuwa Tanzania inazingatia mikataba ya kimataifa ya watoto na Sera ya Taifa ya Maendeleo ya Mtoto ambayo inasisitiza haki ya mtoto kuishi kwa furaha bila kubughudhiwa. Mkuu wa Dawati la Jinsia katika kituo cha polisi wilayani Mpwapwa mkoani Dodoma, Elfrida Mapunda anasema jamii inatakuwa kupinga kwa nguvu zote vitendo hivyo ili kuweza kuvitokomeza.
“Jamii inatakiwa kupunguza migogoro ya kifamilia kwa njia ya mazungumzo ili kuweza kuepusha madhara mbalimbali katika suala zima la malezi ya watoto na hata vitendo vya ukatili kwa watoto,” anasema. Pia anasema ni muhimu kwa jamii kubadilika na kuwa na utamaduni wa kufanya mazungumzo ili kuweza kuepukana na madhara katika malezi na makuzi ya watoto. Anabainisha kuwa migongano ya kifamilia mara nyingi imekuwa ikisababisha vitendo vya ukatili kwa watoto.
Mapunda anasema matukio ya kupigana katika migogoro ya kifamilia yamekuwa jambo la kawaida katika wilaya hiyo jambo linalosababisha watoto kujeruhiwa wakati wa ugomvi. Migogoro ya kifamilia inachochewa na unywaji wa pombe kupindukia na mfumo dume uliojengeka miongoni wa jamii. Anahimiza jamii jamii kubadilika na kuona kuwa vitendo kama hivyo havikubaliki katika jamii kutokana na kuwa na athari nyingi.
Mapunda anataja baadhi ya matukio yaliyopokelewa kwenye dawati la jinsia mapema mwaka huu kuwa ni pamoja na tukio la mtoto mwenye umri wa mwaka moja kupigwa na mchi kichwani na baba yake mzazi Fabian Chigoda kutokana na ugomvi wa kifamilia. Mtoto huyo aliyejeruwa kwa mchi ambao ulikuwa umerushwa na baba yale mzazi kwa lengo la kumpiga mama yake Caroline Mnyawani lakini kwa bahati mbaya mchi huo ukamfikia mtoto ambaye alikuwa amebebwa mgongoni.
Pia mwaka huu alipokea tukio la mtoto mmoja wa miaka miwili, kumwagiwa maji ya moto na mama yake kwa kile kinachodaiwa kuwa ni ugomvi wa kifamilia. Vile vile alipokea tukio la mtoto mmoja wa kike mwenye umri wa miaka minne kumwagiwa uji wa moto na mama yake aliyekusudia kumwagia mume wake baada ya kugundua kuwa alikuwa na mahusiano nje na mwanaume mwingine.
Mapunda anasema matukio kama hayo yanadhihirisha ni kwa kiasi gani wananchi wanatakiwa kubadilika ili kupunguza vitendo vya ukatili kwa watoto. Pia kuna tukio la mtoto mwenye umri wa mwaka moja na miezi minne ambaye alilazimika kulazwa katika hospitali ya Wilaya ya Mpwapwa akiwa na hali mbaya baada ya kupigwa na mchi kichwani na baba yake mzazi. Kwa mujibu wa Mganga Mkuu wa Wilaya ya Mpwapwa, Saidi Mawji, mtoto huyo alikuwa amepata jeraha kichwani na likuwa ameumia sana kichwani huku uchunguzi wa awali ukionesha kulikuwa na mpasuko kwenye fuvu lake la kichwa.
Mama mzazi wa mtoto huyo Caroline Mnyawami (32) ambaye ni mkazi wa Kijiji cha Mingui kata ya Lumuma anasema siku ya tukio majira ya saa nne mume wake, Fabian Chigoda alikuwa akimpiga kaka yake na ndipo akajaribu kuamulia ugomvi huo. Anasema katika juhudi za kumnyang’anya mumewe fimbo aliyokuwa akimpigia kaka yake ndipo mumewe aliamua kuchukua mchi wa kinu na kumrushia kichwani ambapo alikwepa na kisha mchi huo kumgonga mtoto aliyekuwa amembeba mgongoni.
Mkuu wa Wilaya ya Mpwapwa mkoani Dodoma, Antony Mavunde anasema Serikali wilayani humo inandaa mazingira rafiki kwa Asasi za kiraia wilayani hapa ili kuongeza wigo mpana ili shughulikia vitendo vya ukatili dhidi ya watoto. Mavunde anasema vitendo vya kikatili dhidi ya watoto vimekuwa vikiongezeka siku hadi siku na kadri siku zinavyosonga mbele ndivyo vitendo vya ukatili kwa watoto vinavyo pamba moto katika maeneo mbalimbali hapa nchini.
Anasema vitendo hivyo vikizidi kushamiri katika taifa vitasababisha chukizo mbele za Mungu na jamii kwa watoto wasio kuwa na hatia kuzidi kuumizwa kutokana na kutokuwa na uwezo wa kujitetea na hata kupambana. Ubakaji, mauaji ya watoto wenye ulemavu wa ngozi, utupaji wa watoto vyooni, utoaji mimba ni vitendo vya ukatili ambavyo binadamu anavitenda kwa mtoto ambae ni kiumbe dhaifu asiye na uwezo wa kupambana wala kujitetea.
Mkuu huyo wa wilaya anasema kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 ibara ya 13 kifungu cha sita inaweka usawa wa kijinsia ambao watoto ni miongoni mwa kundi nyonge linalohitaji kutetewa na kulindwa kwa ajili ya maslahi ya taifa na jamii yenye usawa na Amani. Anasema vitendo hivyo husababishwa na kumomonyoka kwa maadili katika jamii, maendeleo ya kiteknolojia na imani potofu vinavyosababishwa na watu kupungukiwa na hofu ya mungu ndani mwao.
Askofu Mkuu wa Kanisa la Angilikana Tanzania, Dk Jacob Chimeledya anasema jamii na viongozi wa serikali na viongozi wa dini kuchukua hatua kutokana na vitendo vya ukatili kwa watoto vinavyoendelea katika maeneo mengi nchini. Anasema wana wajibu wa kuchukua hatua dhidi ya vitendo vya ukatili kwa watoto na si kupiga kelele tu bila kuchuka hatua za makusudi za kupambana na vitendo hivyo kwa ajili ya uendelevu wa taifa na kizazi kijacho.
Askofu Chimeledya anasema pindi taifa lolote ambalo damu isiyo na hatia ikizidi kuinuka juu ya ardhi yake inaisababishia taifa laana na kuvurugika kwa amani. Mwijilisti Dickson Paul anasema katika kuhakikisha wanaanza kuchukua hatua za makusudi za kupinga vitendo vya kikatili dhidi ya watoto wamepanga kuzunguka nchi nzima kwa lengo la kuimarisha uelewa kwa jamii juu ya madhara yanayoweza kusababishwa na kukidhiri kwa vitendo vya ukatili kwa watoto.
Pia anasema watatumia matamasha ya uimbaji wa nyimbo za injili ili kuweza kupambana na vitendo vya ukatili kwa watoto wasiokuwa kuwa na hatia wala uwezo wa kujitetea. Aidha anaitaka serikali na jamii kuweza kuisimamia kwa ipasavyo sheria ya mtoto ya mwaka 2009 ambayo ipo lakini imeonekana kutosimamiwa ipasavyo na hivyo kuchangia kuongeza vitendo vya ukatili kwa watoto ambao hufanyika waziwazi pamoja na kuwepo kwa sheria zote kumlinda mtoto.
Kwa mujibu wa Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto, Sophia Simba, takwimu za idadi ya watu na makazi nchini ya mwaka 2012 inaonesha sasa Tanzania inakadiriwa kuwa na watoto 24,377,052 chini ya miaka 18 ambao kati yao 12,201,122 ni wasichana na 12,175,930 ni wavulana sawana asilimia 50.1 ya Watanzania. Anasema kundi hilo linahitaji mipango madhubuti ili kuweza kuwalea na kuwaendeleza katika nyanja za afya,elimu, lishe bora na ulinzi ili waweze kushiriki katika ujenzi waTaifa.
Waziri Simba anasema katika kuhakikisha watoto nchini wanapata haki yao ya ulinzi, Wizara imeendelea kuratibu shughuli za Kikosi Kazi cha Taifa cha Kuzuia na Kupambana na Ukatili Dhidi ya Watoto ambacho kinasimamia utekelezaji wa Mpango Kazi wa Taifa wa Mwitikio na Kuzuia Ukatili Dhidi ya Watoto kuanzia mwaka 2013 hadi 2016 kwa kushirikiana nawadau. Aidha haki ya watoto ya kushiriki ni muhimu kwa kuwa inampa fursa ya kujadili na kutoa maoni kwa uhuru kuhusu mambo yanayowahusu na hivyo kumjengea uwezo wa kujiamini na kujieleza.
Anasema kutokana na hilo Wizara hiyo imeendelea kuratibu shughuli za Baraza la Watoto la Jamhuri ya Muungano waTanzania ambapo vikao vyote vya Baraza Kuu na Kamati kuu vilifanyika. Simba anasema hadi sasa mabaraza ya watoto katika ngazi ya Mikoa yameongezeka kutoka 12 mwaka 2005 hadi kufikia 22 mwaka 2014 na Wilaya kutoka mabaraza 57 mwaka 2005 hadi mabaraza 93 mwaka 2014.
Anasema licha ya mafanikio hayo, Wizara inakabiliwa na changamoto mbalimbali katika kusimamia utoaji wa haki za watoto hapa nchini, ikiwemo kuongezeka kwa vitendo vya ukatili dhidi ya watoto ambapo kuanzia mwaka 2000 hadi 2014 matukio 150 ya ukatili dhidi ya watu wenye ulemavu wa ngozi yameripotiwa na kusabaisha vifo 74 ambapo asilimia 45 ni watoto.
Simba anasema pia kushuka kwa kiwango cha ukeketaji kusikoridhisha kwa asilimia tatu kutoka 18 mwaka 1999 hadi 15 mwaka 2014, kuwepo kwa tatizo kubwa la ndoa na mimba za utotoni ambazo zinasababisha matatizo makubwa katika maendeleo ya kielimu na afya kwa wasichana hapa nchini. “Vitendo vya ukeketaji watoto wa kike bado vinaendelea na juhudi ya kuzuia ukatili huo hazijafanikiwa kama ilivyotajariwa,” anasema Simba.
Pamoja na juhudi zinazofanywa na serikali, bado kuna changamoto mbalimbali katika kusimamia utoaji wa haki za watoto, ikiwa ni pamoja na kuongezeka kwa vitendo vya ukatili dhidi ya watoto. Simba anakiri kuwa ndoa mimba na ndoa za utotoni bado ni tatizo kubwa miongoni mwa jamii ya Watanzania kwa kuwa zinakwamisha maendeleo ya watoto wa kike kielimu na afya. Takwimu zinaonesha kuwa wasichana wawili kati ya watano wanaolewa wanakuwa bado hawajafikisha umri wa miaka 15.
Tafiti za maendeleo ya mtoto zinaonesha kuwa mikoa ya Kanda ya Ziwa inaongoza kwa ndoa za utotoni ambapo Mara ina asilimia 43 ya ndoa za utotoni ikifuatiwa na Tabora asilimia 38 na Shinyanga asilimia 37. Kwa mujibu wa takwimu za mwaka 2014 asilimia 43 ya wasichana wanazaa kabla hawajafika umri wa miaka 18. Simba anasema kuwa ajira hatarishi kwa watoto ni miongoni mwa changamoto zinazolikabili taifa na Wizara yake inajitahidi kuhakikisha kuwa linakomeshwa ili watoto waweze kupata haki ya kusoma na kuishi katika maisha salama.
Inakadiriwa kwamba asilimia 28 ya watoto nchini wenye umri kati ya miaka 5 hadi 17 wanafanyishwa kazi katika mashamba, migodi, viwanda, uvuvi na majumbani. “Watoto hao wanakosa haki ya msingi ya yakupata elimu na msingi wa makuzi bora na matokeo yake wakiwa watu wazima wanakuwa wategemezi katika taifa lao,” anasema Simba. Idadi ya watoto wanaoishi na kufanya kazi mitaani imeongezeka kwa kasi hasa katika majiji, miji mikubwa, maeneo ya mipakani na katika mikusanyiko ya watu.
Simba anataja sababu kubwa zinazochangia matatizo ongezeko la watoto wanaoishi mitaani na ajira za watoto kuwa ni uelewa mdogo wa jamii kuhusu haki za mtoto, mamlaka mbalimbali kushindwa kuchukua hatua zinazostahili kukabiliana na matatizo punde yanapotokea na kuendelezwa kwa mila na desturi zenye madhara katika jamii.
Ili kukabiliana na changamoto serikali imedhamiria kudurusu Sera ya Mtoto ya 2008 ili kuingiza masuala ya malezi, makuzi na maendeleo ya awali ya mtoto katika kuimarisha misingi ya malezi ya watoto hasa katika umri mdogo; kuimarisha mikakati ya ulinzi wa mtoto na kuboresha uratibu wa masuala ya watoto.
No comments:
Post a Comment