Tuesday, 28 July 2015

BOMBA LAKAMILIKA, USAFIRISHAJI GESI KUANZA

MRADI wa bomba la gesi kutoka Mtwara mpaka Dar es Salaam umekamilika na wiki ijayo gesi itakuwa na uwezo wa kufika jijini Dar es Salaam.


Aidha kazi ya kufua umeme kwa kutumia gesi asilia na kuuingiza katika mifumo ya Shirika la Umeme nchini (TANESCO) itaanza mwezi ujao.
Hayo yalisemwa na Kaimu Mkurugenzi wa Shirika la Maendeleo ya Petroli (TPDC), Kapuulya Musomba juzi wakati bodi ya shirika hilo ilipofanya ziara ya kutembelea mradi huo kwa lengo la kujionea hali halisi kabla ya gesi kuanza kusafirishwa kutoka Mtwara kuja Dar es alaam.
Musomba alisema kwamba Agosti mosi mwaka huu, gesi itakuwa na uwezo wa kufika katika mitambo ya kuzalisha umeme ya Kinyerezi One na Tegeta, Dar es Salaam.
Alisema licha ya kuwa na uwezo wa kufika wiki ijayo, lakini wanatarajia gesi kwa ajili ya kufua umeme kufika katika mitambo hiyo Septemba 6 au 7 kutokana na hoja za kitaalamu za hatua ya mwanzo ya kuchakata na kusafirisha gesi.
Musomba alisema hayo akiwa katika kituo cha Somanga Fungu ambapo kuna mitambo maalumu ya kupokea gesi kutoka Songosongo na Mtwara, kisha kusafirishwa kwenda jijini Dar es Salaam. Alisema hatua hizo zinafuatwa kwa siku 45 ili kuhakiki vifaa vyote kuwa havina tatizo kuanzia kuchimba, kuchakata na hata kusafirisha.
Alisema baada ya majaribio hayo ya kupeleka gesi Dar es Salaam kufanikiwa, Septemba 15 wataanza kuingiza umeme uliozalishwa kwa gesi asilia Tanesco ili watanzania waanze kuona matunda ya gesi na bomba lenyewe.
“Kwa sasa Tanesco wana mitambo ya kuzalisha megawati mia mbili za umeme, lakini hazifanyi kazi hivyo sisi tutaanza kuzalisha umeme kwa kutumia gesi na kuingiza Tanesco megawati mia moja hamsini za umeme”alisisitiza Alisema tayari mpaka sasa wameshaajiri wafanyakazi 30 katika vituo vya mitambo ya Kinyerezi na 11 Somanga Fungu tayari kwa kuanza usafirishaji na uzalishaji katika mitambo.
Alisema katika bomba hilo la kilometa 504 ambazo ni umbali wa mradi kutoka Mtwara hadi Dar es Salaam una valvu zaidi ya 100, lakini kuu zipo 16 na kukitokea tatizo kwenye valvu zinafungwa kwa ajili ya usalama.
Akizungumzia suala la usimamiaji wa usalama katika bomba hilo, alisema wameweka mikakati mbalimbali ikiwemo kuajiri watu wenye utaalamu wa ulinzi.
Pia alisema katika usalama wanakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo hofu ya ugaidi inayozidi kuongezeka, huku wakitumia vifaa vya kisasa katika ulinzi wa bomba hilo pamoja na kushirikisha wananchi.
Naye Mwenyekiti wa Bodi wa shirika hilo, Michael Mwanda alisema anajivunia sana kukamilika kwa mradi huo na kufikia hatua ya watanzania kuanza kuona matunda yake kwani awali kulikuwa na maoni na vipingamizi mbalimbali.
Alisema wameona na kuridhishwa na utendaji wa wataalamu wa ndani na nje ya nchi kwa ujenzi wa bomba hilo hivyo viwanda vitaongezeka kwa kuwa na umeme wa uhakika jambo litakaloongeza uzalishaji wa bidhaa pamoja na ajira.
Akizungumzia kushuka kwa gharama za umeme, Mwanda alisema anavyoona yeye kutakuwa na unafuu kwani sasa Tanesco wataoondokana na kuzalisha umeme kwa kutumia mitambo inayotumia mafuta. Mradi huo umegharimu pesa za Marekani Dola bilioni 1.2 sawa na fedha za Tanzania zaidi ya Sh trilioni 2.4.
Inaelezwa kuwa kukamilika kwa mradi huo kutaokoa zaidi ya Dola za Marekani bilioni moja sawa na Sh trilioni 2 kwa mwaka, fedha ambazo zinatumika sasa kuagiza mafuta kwa ajili ya kufua umeme kwa kutumia mitambo ambayo tayari ipo nchini.

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!