WAZIRI Mkuu Mizengo Pinda amesifu juhudi za mifuko ya hifadhi ya jamii nchini inayomilikiwa na serikali kwa kazi nzuri iliyofanya ikiwemo ujenzi wa vyuo vikuu mbalimbali kikiwemo cha Dodoma,Nelson Mandela pamoja na jengo la Bunge la jamuhuri ya Muungano wa Tanzania.
Waziri Mkuu Pinda alitoa pongezi hizo alipokua akifungua mkutano wa tano wa wanachama wa mfuko wa jamii wa NSSF unaoendelea mkoani Arusha na kushirikisha viongozi wa mifuko mingine ya ndani ya nchi na ile ya nje ya nchi.
Alisema pasipo kuwepo kwa mifuko hiyo mambo mbalimbali ya maendeleo yakiwemo ya ujenzi huo kamwe yasingefanyika kutokana na ufinyu wa bajeti ya serikali jambo ambalo lilisababisha serikali kuitumia mifuko hiyo kwa makubaliano ya kulipa deni litakalotokana na shughuli hizo za maendeleo.
Alisema mbali na mchango huo wa ujenzi wa miundo mbinu pia mifuko hiyo imeweza kuchangia pato la taifa kwa kiasi cha asilimia 11 tofauti na sekta zingine ambazo bado zina michango midogo katika pato la taifa mbali na ile ya utalii na madini.
Pia alisema hadi hivi sasa mifuko hiyo ina mtaji wa kiasi cha shilingi trilioni tano na milioni miambili na arobaini na mbili mtaji ambao unampa uhakika wa kuendelea kuwepo kwa mifuko hiyo na kamwe haiwezi kutetereka kwa namna yoyote hata kutokana na misukosuko mbalimbali inayoonekana.
Aliahidi serikali kurejesha madeni yote yanayodaiwa na mifuko hiyo kutokana na kazi mbalimbali za maendeleo zilizofanywa nayo ili kuwezesha mifuko hiyo kuendelea kukua na kutoa michango yake katika ukuaji wa uchumi na maendeleo ya nchi.
Naye mkurugenzi mkuu wa NSSF Ramadhan Dau alisema mwaka huu shirika lake limekaa na kutathimini changamoto mbalimbali zinazoikabili jamii ya watanzania na kuja na kauli mbiu ya Hifadhi ya jamii na ujasiriamali yenye mikakati mbalimbali ya kuiondoa jamii dhidi ya changamoto hizo.
Alizitaja changamoto hizo kuwa ni ukosefu wa mikopo toka taasisi mbalimbali za kifedha kutokana na na kukosekana kwa mali za kuweka kama dhamana ambapo tayari shirika lake limeanza kutoa mikop yenye masharti na riba naafuu ya kiasi cha shilingi bilioni 55.6 ambapo watu 7000 mpaka sasa wameshanufaika.
Alitaja changamoto nyingine kuwa ni ukosefu wa ujuzi na nidhamu ya biashara kwa wajasiriamali kutokana na ukosefu wa elimu ambapo shirika lake tayari limeanza mazungumzo na taasisi za serikali ikiwemo Veta,Sido na nyinginezo ili kuweza kutoa mafunzo hayo kwa wajasiriamali hao.
Pia alitaja changamoto nyingine kuwa ni ukosefu wa uthubutu na woga kwa wajasiriamali katika kuanzisha biashara na kujiajiri ambapo katika mkutano huo wamewaalika watu mbalimbali ambao watatoa ushuhuda wao wa maisha yao ya kujiajiri kama chachu ya wajasiriamali kujiamini na kutuhubutu kufanya biashara.
Aliwataja watu waliowaalika kuwa ni pamoja na mfanyabiashara Patrick Mfugale anayemiliki kampuni za Pickkork,mfanyabiashara Salim Salum Bakhresa na mfanyabiashara maarufu afrika raia wa Nigeria Alhaj Aliko Dangote.
Pia alitaja mafanikio mbalimbali yaliyofikiwa na shirika lake hilo ikiwa ni pamoja na kuongeza idadi ya wanachama,ujenzi wa majengo mbalimbali ya kitega uchumi ambapo pia aliweza kutaja matarajio yao mbalimbali ikiwemo ujenzi wa hospitali ya Apollo katika mji ya Kigamboni jijini Dar es salaam.
Pia alitaja mradi mwingine wanaotaraji kuufanya ni ule wa ujenzi wa kituo cha michezo,ujenzi wa mradi wa kuzalisha umeme wa megawati 1000 utakaochangia katika gridi ya taifa utakaofanyika katika mji wa Kibaha mkoani Pwani pamoja na ujenzi wa viwanda vya bidhaa zitakazotumia rasilimali mbalimbali zitokanazo na wanyama na mimea.
No comments:
Post a Comment