Monday, 15 June 2015

RIPOTI MAALUMU: MUHIMBILI YAKAUKIWA DAMU


Wakati utoaji huduma za afya ukizidi kuzorota katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH), ukosefu wa damu umekuwa tatizo sugu linalosababisha mateso na vifo kwa wagonjwa.

Hospitali hiyo inahitaji wastani wa chupa za damu 70 hadi 100 kwa siku kwa ajili ya kuwawekea wagonjwa mbalimbali, lakini imekuwa na uwezo wa kupata chupa 20 hadi 30 pekee kwa siku. 
Baadhi ya madaktari wa hospitali hiyo waliliambia NIPASHE kuwa ukosefu wa damu MNH ni wa muda mrefu, hivyo `kujenga’ mazingira ya kuamini kuwa uongozi wake umeshindwa kulipatia ufumbuzi wa kudumu.
Daktari bingwa wa watoto hospitalini hapo ambaye hakutaka jina lake litajwe gazetini, alisema ni kawaida kwa wagonjwa wanaohitaji damu kukaa wodini hadi siku tatu na wengine kufa kutokana na kukosa damu.
Kwa mujibu wa chanzo hicho, baadhi ya wagonjwa wanawekewa damu kidogo ya mahitaji kama sharti la kuwashirikisha ndugu, jamaa na marafiki kuchangia, na inapotokea wasijitokeze kufanya hivyo, madaktari wanasitisha kumuongezea (mgonjwa) damu iliyobaki.
Lengo la hatua hiyo linaelezwa kuwa ni hamasa kwa walio karibu na mgonjwa kuchangia ili irejeshwe kwenye benki ya damu kwa vile wakati mwingine, damu inayotolewa inaweza isiwe kundi la ile inayohitajika kwa mgonjwa.
Uchunguzi wa gazeti hili umebaini kuwa inapotokea dharura kwa mgonjwa kuhitaji damu, MNH inamkopesha (mgonjwa) kiasi kidogo cha damu kuokoa maisha kwa wakati husika, huku ndugu wakitakiwa kuchangia ili kufidia kiasi halisi kinachohitajika.
“Kama mtu amezidiwa wakaona anaweza kufa, wanamkopesha damu kidogo kama unit moja ambayo ni nusu lita na haitoshi, lakini lengo ni kuwalazimisha ndugu wa mgonjwa kuchangia kiasi cha damu inayohitajika,” kilieleza chanzo kingine katika wodi ya wanawake.
Wakati hali ikiwa hivyo, taarifa zinaeleza kuwa baadhi ya vifo vikiwamo vinavyotokea kwenye wodi vinahusishwa na ukosefu wa damu.
Taarifa za kitabibu kutoka kwa madaktari wakiwamo wa MNH zinaeleza kuwa mgonjwa anayehitaji kuongezewa damu akikaa muda mrefu bila kupata huduma hiyo, moyo unashindwa kufanya kazi na hivyo kusababisha kifo.
UKUSANYAJI DAMU
Vyanzo tofauti vimebaini kuwa uongozi wa MNH unalaumiwa kwa hali hiyo kutokana na kushindwa kukusanya damu kwa wingi kwani hakuna jitihada zozote zinazofanyika kama vile kuhamasisha wananchi kujitolea damu kwenye kitengo cha damu.
Watu wanaoathirika kutokana na ukosefu wa damu ni wanaofanyiwa upasuaji, wenye matatizo yanayohusiana na tumbo, wanaoharisha na kutapika damu, wenye saratani ya damu, upungufu wa damu na magonjwa ya kuambukiza.
Daktari anayezungumza na NIPASHE kwa sharti la kutotajwa jina gazetini, alisema upungufu wa damu unasababishwa na uzembe wa kitengo cha damu kushindwa kufanya kazi yake ipasavyo kama kuhakikisha kunakuwa na akiba ya damu ya kutosha, hivyo kuweka rehani maisha ya wagonjwa wanaohitaji damu.
MWAMKO
Wakati MNH ikidaiwa kushindwa kufanikisha upatikanaji damu, mwamko wa umma bado ni mdogo katika kutoa damu inayohitajika kwa maisha ya wagonjwa.
Idadi kubwa ya wanaofika MNH kuchangia damu wanafanya hivyo ili kuwasaidia ndugu, jamaa ama rafiki wanaohitaji na si vinginevyo.
Pia kuna dhana potofu inayochochea hofu kwa watu kuchangia damu, wakielewa kwamba watapimwa magonjwa kama maambukizi ya Virusi Vya Ukimwi (VVU) bila ridhaa yao.
Hivyo ipo haja kwa kitengo cha damu kuhamasisha na kutoa elimu kwa umma kutambua umuhimu wa kuchangia damu.
MNH YATHIBITISHA
Msemaji wa MNH, Aminiel Aligaesha, anathibitisha hospitali hiyo ‘kukaukiwa’ damu kiasi cha kuwategemea ndugu, jamaa na marafiki wa mgonjwa.
Aligaesha alisema huduma iliyopo ni kutoa damu (kidogo) kwa vile MNH inapata kiasi kidogo kutoka Mpango wa Taifa wa Damu Salama, hivyo haitoshi kwa mahitaji yaliyopo.
Kwa mujibu wa Aligaesha, hivi sasa MNH ina uwezo wa kuwahudumia wagonjwa wanaohitaji damu kwa asilimia 60, hivyo kuwa na ‘pengo’ la asilimia 40 ya mahitaji ya damu.
Alisema Hospitali ya Taifa Muhimbili ni mnufaika wa damu na kwamba mwenye dhamana kisheria ya kukusanya (damu) na kusambaza kwenye hospitali ikiwamo MNH ni Mpango wa Taifa wa Damu Salama.
“Wigo wetu ni kukusanya damu ndani ya hospitali kwa ndugu na jamaa wa wagonjwa ambao mgonjwa wao anapolazwa anahitaji damu. Hatuwezi kuvuka nje ya uzio wa MNH kuchukua damu maana haturuhusiwi kisheria,” alisema.
Alisema hospitali hiyo inategemea kupata damu kutoka vyanzo vikuu viwili ambavyo ni ndani ya hospitali kupitia ndugu wa wagonjwa wanaohitaji kufanyiwa upasuaji na watu wengine wanaokwenda kujitolea damu.
Chanzo cha pili cha damu hospitalini hapo ni Mpango wa Taifa wa Damu Salama (NBTS) ambao kisheria ndiyo wenye dhamana ya kukusanya damu na kusambaza kwenye hospitali ikiwamo MNH. 
Kuhusu hali halisi ya upatikanaji damu kwa sasa, Aligaesha alisema makusanyo ya damu kutoka vyanzo vya ndani ni kati ya chupa 20 hadi 40 kwa siku zinazoweza kutumika kwa wagonjwa.
Aidha, alisema upatikanaji wa damu kutoka NBTS umekuwa wa kiwango cha chini na hata wakati mwingine wanashindwa kupata damu kutoka huko. 
Alisema bado jitihada za watu, vikundi, mashirika ya umma na shule zinahimizwa kwenda hospitalini hapo kujitolea damu ili kuwezesha uwapo wa akiba kubwa ya damu.
Aligaesha alisema baada kutoa tangazo la kuwaomba wananchi kufika kujitolea damu mwezi Mei, idadi ya watu waliokwenda kujitolea damu iliongezeka kutoka watu 20 hadi 40 kwa siku na kufikia kati ya watu  60 hadi 70 kwa siku. 
Alisema damu hiyo imekuwa ikitumika sana kwa wagonjwa wa dharura, kina mama wajawazito, wagonjwa waliofanyiwa upasuaji, watoto pamoja na wagonjwa wa saratani.
Alisema kila mgonjwa wa upasuaji wa moyo anahitaji kiasi cha chupa tano mpaka sita za damu na kwamba matumizi hayo yanafanyika kabla, wakati na baada ya kufanyiwa upasuaji.
“Endapo kwa siku ukifanyika upasuaji wa moyo (kwa kufungua kifua) kwa wagonjwa sita kuna matumizi ya damu chupa 36 sawa na nusu ya akiba tuliyonayo,” alisema.  Alisema wenye mamlaka kisheria ya kukusanya na kusambaza damu ni NBTS kwani wao wanapaswa kukusanya na kuipeleka MNH kadri ya mahitaji ya hospitali hiyo.
Hata hivyo, Aligaesha alisema hospitali hiyo imekuwa ikitenga fedha kwa ajili ya kazi hiyo kila mwaka ili pale Damu  Salama wanaposhindwa kuwapelekea ya kukidhi mahitaji, waendelee kutoa huduma kama kawaida.
Alisema MNH hairuhusiwi kisheria kukusanya damu nje ya ukuta wake (premises) kwa kuwa mwenye mamlaka hayo ni NBTS.
NBTS walitaka NIPASHE kuwasiliana na Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii juu ya hali ya upatikanaji wa damu salama nchini.
Gazeti hili lilifanya jitihada kumpata Katibu Mkuu wa Wizara hiyo bila mafanikio lakini Msemaji wa Wizara hiyo, Nsachris Mwamaja, alithibitisha kwamba hali ya upatikanaji wa damu salama ni mbaya.
Alisema hali hiyo imesababishwa na kujitoa kwa mfadhili mkuu wa mpango huo, hivyo kuifanya kubaki katika hali mbaya kifedha.
Mpango wa damu salama kwa kiwango kikubwa ulikuwa ukigharimiwa na Kituo cha Kudhibiti na Kuzuia Magonjwa (CDC), ambayo iligharimia mishahara, vifaa vya kuhifadhia na kusafirishia damu.
Msemaji wa Wizara ya Afya alisema serikali imejipanga kukabiliana na changamoto hiyo ya kugharimia shughuli za ofisi hiyo ili kuhakikisha damu inapatikana katika maeneo mbalimbali.
Alisema ni kweli kuna tatizo kubwa la damu, hivyo alitoa wito kwa Watanzania kujitokeza kwenda kujitolea damu kwenye hospitali mbalimbali nchini ili kuokoa maisha ya wagonjwa wanaohitaji kuongezewa damu.
WAGONJWA WALIOKOSA DAMU:
Mmoja wa watu waliokumbwa na mkasa wa kukosa damu katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH), Ayubu Kagirwa (43) aliyekuwa akisumbuliwa na maumivu ya tumbo alisema bila ndugu zake huenda angeshafariki.
Alisema alifikishwa hospitalini hapo kwa mara ya kwanza Machi mwaka huu na kulazwa wodi ya Kibasila na baada ya vipimo mbalimbali ilikuja kubainika kuwa anahitaji kufanyiwa upasuaji.
Alisema madaktari walimweleza wazi kuwa hakukuwa na damu ya kutosha kumwekea hivyo ilimlazimu yeye na ndugu zake kupiga parapanda kwa ndugu na jamaa mbalimbali waende kujitolea damu.
“Bila ndugu zangu sijui ingekuwaje maana niliambiwa benki ya damu imekaukiwa, hivyo nisubiri michango ya watu mbalimbali ndipo ndugu zangu wakaanza kuitana huku na kule na kwa kweli namshukuru Mungu waliitikia wito na kufika kwa wingi, nilipata chupa za kutosha nikawekewa,” alisema.
Tabu Shaibu ( 34), mkazi wa Gongo la Mboto, yeye alipata mkasa wa kukosa damu mara baada ya kujifungua mtoto wake wa pili katika wodi ya wanawake Hospitali ya Taifa ya Muhimbili lakini upatikanaji wa damu ya kumwongezea ilizua taharuki kwa ndugu zake.
“Nilikuwa nimelazwa kwa siku tatu na mama yangu muda wote alikuwa akija mara tatu kwa siku. Siku ya nne nilijifungua mtoto wa kiume, nikaishiwa damu kabisa kiasi nikawa napoteza fahamu, damu ilikuwa shida sana na ndugu walipopata taarifa walikuja kwa wingi ndipo nilipopata damu,” alisema.
Aidha, alisema ameshuhudia wanawake wengi wanaojifungua wakihitaji kuongezewa damu lakini wakikosa huduma hiyo hadi pale ndugu na jamaa kama ilivyokuwa kwake wanapojitokeza na kuchangia chupa za damu.
“Hili ni tatizo kubwa, halijaanza leo wala jana, kwa muda mrefu watu wanalalamika lakini ni kama vile hakuna hatua zinazochukuliwa, fikiria wanawake wanajifungua kila siku hapa lazima waweke damu ya akiba kwa wanaoweza kuhitaji kuongezewa damu,” alishauri

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!