Serikali ya Burundi imekariri kuwa rais Pierre Nkurunziza hatajiondoa kutoka kinyanganyiro cha urais licha ya nchi hiyo kukabiliwa na wimbi la maandamano.
Waandamanaji wanapinga hatua ya rais Nkurunziza kuwania muhula wa tatu ambao ni kinyume na Katiba ya taifa hilo.
Rais Nkurunziza kwa upande wake anashikilia kukutu kuwa ana haki ya kuwania muhula wa tatu kwani muhula wa kwanza alichaguliwa na wawakilishi na wabunge wala sio raia kuambatana na mapatano ya amani.
Msemaji wa rais Philippe Nzobo-nariba amesema swala la rais Nkurunziza kuwania muhula mwengine si la kujadiliwa na kwamba tarehe ya uchaguzi haitaahirishwa tena.
Awali vyama vya upinzani vilikuwa vimepinga ratiba mpya ya uchaguzi iliyotolewa na tume huru ya uchaguzi nchini humo wakihoji uhalali wa ratiba hiyo inayotarajiwa kutekelezwa katika kipindi cha majuma mawili yajayo.
Wakati huohuo, afisa mmoja wa ngazi ya juu katika umoja wa mataifa ameonya kuwa kundi la wanamgambo wanaounga mkono serikali wamekuwa wakiendeleza ukatili dhidi ya wale wanaopinga uamuzi wa rais Nkurunziza kuwania awamu ya tatu madarakani.
Kamishna huyo wa kitengo cha umoja wa mataifa kinachohusika na haki za kibinadamu, Zeid Ra'ad Al Hussein amesema wanamgambo hao wanaoiuunga mkono serikali wametuhumiwa kuhusika katika vitendo vya mauji , kuwapiga na kuwanyanyasa baadhi ya wapinzani na kuitaka serikali kukemea na kukomesha vitendo hivyo.
Kitengo hicho cha umoja wa mataifa chasema kimekuwa kikipokea simu kutoka pande mbalimbali za Burundi kulalamikia vitendo kama hivyo na hasa kutishwa na wanaosemekana kuwa wafuasi wa kundi hilo linalojiita Imbone-rakure.
Kiongozi wa Imbone-rakure amekuwa akisema kundi lao halihusiki na vitendo vya kutumia nguvu, lakini umoja wa mataifa unasema umekuwa ukipokea msururu wa ushahidi wa watu wanaolalamikia kundi hilo la kuwa pia limekuwa likipokea silaha, magari na wakati wengine hata sare za vikosi vya usalama kama vile polisi na shirika la kijajasusi nchini humo.
Umoja huo unasema vitendo vya kundi hilo vinazidi kuhatarasha usalama na iwapo vitaendelea vitalipeleka pabaya taifa hilo .
Kwa upande wao serikali imekana kulihami kundi hilo na kuongeza kuwa Burundi ina utulivu wa kutosha kuweza kuendelea na uchaguzi wake.
BBC.
No comments:
Post a Comment