Tuesday, 9 June 2015

ENEO ALILOPEWA DANGOTE LAZUA MJADALA



Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, imetaka serikali kuweka wazi kama mwekezaji Mnigeria, Bilionea Alhaji Aliko Dangote (pichani), kama alipewa kisheria ardhi yenye ukubwa wa hekta 2, 500 kwa kubadilishana na ujenzi wa shule na hospitali katika Kijiji cha Mgao, Kata ya Maumbu, wilayani Mtwara vijijini.



 
Waziri Kivuli, Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Halima Mdee, akiwasilisha maoni ya kambi hiyo, kuhusu bajeti ya Wizara hiyo, alisema bilionea huyo alikabidhiwa eneo la ufukwe wa Bahari ya Hindi, kwa ajili ya kujenga bandari yake ya kisasa ili kusafirisha saruji yake atakayozalisha kwenye kiwanda chake kikubwa katika kijiji cha Msijute.
 
"Katika taarifa zilizozagaa kwenye vyombo vya habari ambazo hazijakanushwa, zinaeleza kuwa Mwenyekiti wa Kijiji cha Mgao, Abdulrahman Shaa, ndiye aliyemkabidhi mfanyabiashara huyo ardhi, hekta 2,500 sawa na ekari 6,600... zilitolewa bure kwa ahadi kwamba wanakijiji hao watajengewa shule na hospitali," alibainisha na kuongeza:
 
" Ni aibu kwa serikali kutoa ardhi yenye thamani kubwa, iliyopo ufukweni (prime area) bure kwa kubadilishana na ujenzi wa shule na hospitali. Hii haina tofauti na kubadilishana dhahabu na kipande cha kanga au haitifoutiani na wale waliopokea vipande vichache vya kaniki wakawauza mababu zetu utumwani, kweli karne hii ya 21 serikali inafanya bater trade? Serikali imeshindwa kutoa huduma za jamii kwa wananchi wake hivyo inagawa ardhi yetu ili iwezeshwe na wageni kutoa huduma," alisema.
 
Mdee alisema suala la utwaaji wa ardhi barani Afrika, hususan Tanzania, linazungumzwa, idadi ya Watanzania inaongezeka na ardhi yenye rutuba inapungua na  mahitaji ya chakula nayo yanaongezeka. Alisema kwa mujibu wa taarifa ya makisio ya idadi ya watu duniani ya mwaka 2012, inatarajiwa ifikapo 2050, mahitaji ya chakula duniani yataongezeka kwa asilimia 70 kutokana na ongezeko la watu duniani kutoka bilioni 7.2 hadi bilioni 9.6.
 
Alisema sheria ya ardhia ya kijiji ya mwaka 1999 inatoa mamlaka kwa halmashauri ya kijiji kusimamia ardhi yote ya kijiji na kwamba, halmashauria ya kijiji siyo mmiliki wa ardhi ya kijiji bali mdhamini aliyepewa wajibu wa kusimamia ardhi hiyo.
Alifafanua kuwa mkutano wa kijiji una ukomo wa mamlaka wa kugawa ardhi, baada ya kupokea maombi ya ardhi kwa mujibu wa sheria namba 5 ya mwaka 1999 na ina uwezo wa kugawa kati ya ekari 100-500 sawa na hekta 38 - 190.
 
Kambi hiyo ilitaka serikali kulieleza Bunge kama utaratibu uliotumika kumpatia Dangote ardhi ya uwekezajj ulikuwa ni wa kisheria au la, kama kulikuwa na mahitaji halisi katika ekari 6,600 ya ardhi ya wananchi kama hoja ilikuwa ni kujenga bandari binafsi ya kumuwezesha kusafirisha saruji kutoka kiwandani kwenda nje ya nchi kwani eneo lililochukuliwa ni kubwa kuliko mahitaji halisi.
 
Akichangia mjadala wa Wizara hiyo, Mbunge wa Mtwara Vijijini, Hawa Ghasia, alisema taarifa alizotoa Mdee hazina ukweli na kwamba, jina la kata inayotajwa siyo sahihi bali ni Naugwi, ikiwa ni eneo la Ghuba ya Sudi lenye ukubwa wa hekta 867.
Alisema tajiri huyo wa kimataifa aliomba hekta 25 kwa ajili ya ujenzi wa bandari ndogo kwa ajili ya kusafirishia saruji na siyo eneo kubwa kama ilivyoelezwa na Mdee katika hotuba yake.
 
"Dangote ni muelewa na makini. Anafuata sheria ya nchi, maombi yake ya ardhi yamepita kwenye mamlaka zote hadi Kituo cha Uwekezaji Tanzania ( TIC), alitembelea kijiji cha Mgao, wananchi waliridhia ardhi kuchukuliwa, serikali imefanya tathmini ya mali na ardhi, wananchi watalipwa fidia na Dangote atamilikishwa kwa utaratibu," alifafanua.
 
Ghasia ambaye pia ni Waziri wa Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, alisema kinachofanyika ni utafiti wa baharini kama kina kitatosha kujenga bandari hiyo, na kwamba aliahidi kuchangia maendeleo kwa kujenga shule mbili za kisasa na kituo cha afya.
Alisema hadi sasa ameshatoa Sh. milioni 450 kupitia benki ya CRDB kwa ajili ha miradi ya maendeleo ya wananchi, hususani vijana na vyote vinafanyika kabla ya kiwanda cha saruji kuanza uzalishaji.
 
CHANZO: NIPASHE

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!