Wednesday 18 March 2015

WAPENDEKEZA UANZISHWE MFUKO UGONJWA WA FIGO



Wagonjwa wa figo nchini wameiomba serikali kuanzisha mfuko maalum wa kusaidia kifedha matibabu ya ugonjwa huo ambao matibabu yake yana gharama kubwa ndani na nje ya nchi.


 Wagonjwa hao walitoa rai hiyo wakati wa sherehe fupi iliyoandaliwa na Hospitali ya TMJ, jijini Dar es Salaam, kwa ajili ya kuadhimisha Siku ya Figo Duniani juzi.  
“Tunaiomba serikali kuanzisha mfuko maalum ambao utasaidia matibabu ya figo na magonjwa mengine ambayo matibabu yake wagonjwa wengi hawawezi kuyamudu kutokana na gharama kubwa,” walisema.
 Mmoja wa wagonjwa hao, Robson Mashamba, alisema mgonjwa mmoja wa figo anatumia Sh. milioni moja kwa wiki kwa ajili ya kusafisha damu, wakati  wagonjwa wengi wanaohitaji huduma hiyo ni maskini wasio na uwezo wa  kumudu gharama hizo kubwa.
 “Serikali lazima isaidie wagonjwa wa figo ambao wanaongezeka kwa kasi nchini,” alisema.
 Mgonjwa mwingine, Kabuchi Enock, aliitaka serikali itoe kupaumbele kwa wagonjwa wa figo, kwa kuweka utaratibu maalum wa kusaidia matibabu yao na kushauri kuwa wagonjwa wote wa ugonjwa huo waingizwe katika utaratibu wa Mfuko wa Bima ya Afya.
Pia alitoa pendekezo kwa mamlaka husika kujenga vituo vya kutolea huduma kwa wagonjwa wa figo nchi nzima katika ngazi za kanda ili kuwapunguzia adha wagonjwa hao, pamoja gharama kubwa za matibabu na umbali mrefu kutoka vijijini kwenda Dar es Salaam kufuata tiba. Charles Mdoe, mgonjwa mwingine alishauri serikali na wadau wa sekta ya afya kuweka mikakati ili kuhakikisha wagonjwa wa figo wanatibiwa ndani ya nchi badala ya kuwapeleka nje.
Akizungumza na wagonjwa, Mganga Mkuu mstafu, Dk. Gabriel Upunda, alisema kuna dalili njema kwamba matatizo mengi ya figo yataanza kutibitiwa ndani ya nchi. 
“Kwa jinsi ninavyoona mwelekeo, ndani ya miaka miwili au mitatu, tiba ya magonjwa ya figo itapatikana hapa nchini na kutoa mfano wa Kituo cha Kubadilisha Figo (Kidney Transplant) kinachojengwa na Hospital ya TMJ.
 Akizungumza kuhusu mradi huo, Mkurugenzi Mkuu wa hospitali ya TMJ, Dk. Tayabali Jafferji, alisema maabara ya kubadilisha figo itakamilika ndani ya mwaka mmoja na nusu na kuongeza kuwa hospitali hiyo itatoa matibabu yote yanayohusu figo.
CHANZO: NIPASHE

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!