Nipo katika ubalozi wa Uturuki jijini Dar es Salaam, ambako Baraza la Mambo ya nje ya Uturuki ya Mahusiano ya Kiuchumi (DEiK) inaeleza kuhusu mpango wa nchi hiyo kushirikiana na Tanzania katika nyanja mbalimbali za kiuchumi na biashara.
Mwenyekiti wa baraza hilo, Atakan Giray ameelezea mpango wa kuimarisha biashara na Bara la Afrika.
Giray anasema tayari Uturuki na Tanzania zimesaini mpango wa kibiashara na kwa mwaka jana takwimu zinaonyesha kuwa biashara baina ya mataifa haya mawili iligharimu Dola 184 milioni za Marekani sawa na Sh324 bilioni.
Anasema Uturuki imetenga Dola 5 bilioni sawa na Sh9 trilioni kwa Afrika, ambazo sehemu yake itaelekezwa Tanzania.
Giray anasema wameiteua Tanzania kama lango la biashara kwa eneo la Afrika Mashariki. Kutokana na hali hiyo, alisema fedha nyingi zitatumika Tanzania ili kuanzisha miradi mbalimbali kwa lengo la kufanikisha azma hiyo.
Anasema tayari kampuni 45 za Uturuki ambazo tayari zipo kwenye harakati za kuanzisha shughuli za uwekezaji hapa nchini.
“Naamini, tunaweza kufanikisha miradi mingi pamoja na rafiki zetu Watanzania,” anasema Giray.
“Katika nafasi hiyo tumepanga kuongeza ubia na Tanzania kupitia uagizaji wa bidhaa zinazoingia Uturuki. Kwa sasa kuna bidhaa kama chai, kahawa na tumbaku zinaingia kwa wingi Uturuki.” Anasema kwamba kwa sasa idadi ya watu inaongezeka kwa kasi hapa duniani, hivyo, wamepanga kuongeza kasi ya uwekezaji wa kilimo nchini ili kuongeza uzalishaji wa chakula.
Anasema katika mpango huo, itaongeza uwezo wa Tanzania kuuza vyakula kwa wingi duniani.
Giray anasema mbali na kuvutiwa katika kilimo, Uturuki imevutiwa na mazingira mazuri ya Tanzania hasa katika nyanja ya utalii, madini, biashara za kibenki na nishati.
Makamu mwenyekiti wa baraza hilo, Nazim Yavuz anasema: “Katika biashara, tunachoangalia ni ubora wa bidhaa na bei nafuu ili kuingia kwenye ushindani wa masoko katika mataifa mengine.”
Anasema DeiK, imefanikiwa kujikita kwenye mabaraza ya kibiashara 121 katika kanda nane zinazounganisha Bara la Afrika.
Tanzania inasemaje?
Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania (TPSF) ndiyo iliyoingia kwenye makubaliano ya kukuza mahusiano ya kibiashara na Uturuki.
Mwenyekiti wa Umoja wa Maofisa Watendaji Wakuu wa Kampuni Binafsi Tanzania (CEO’s Roundtable), Ali Mufuruki anasema fursa hiyo kwa Watanzani itakuwa ni sehemu ya kujifunza zaidi mbinu za kibiashara kutoka kwa wafanyabiashara wakubwa walioshikilia uchumi wa nchi kwa zaidi ya miaka 50 sasa.
Anasema asilimia 80 ya uchumi wa Tanzania inashikiliwa na Wahindi. Asilimia 20 ya sehemu inayobakia inashikiliwa na Serikali, huku Watanzania weusi wakibakia na asilimia ndogo zaidi.
“Kwa hivyo, wanaponufaika Watanzania tunawazungumzia Wahindi. Mfano asilimia 90 ya biashara ya Wachina imewekezwa katika sekta ya ujenzi kwa hivyo wanaonufaika kupitia nafasi hiyo ni Wahindi,” anasema akidokeza: “Ni aibu Wahindi kumiliki asilimia 80 ya uchumi wetu.” Anasema ukweli ni kwamba uchumi wa Tanzania hauwafanani na hali halisi ya Watanzania.
Kwa sababu hiyo, anasema unahitajika ukombozi wa kisera na kimawazo ili kuziba pengo la Waafrika na wala kufanya hivyo siyo ubaguzi. Mufuruki anasema Waturuki wakishafanikiwa kuingia hapa nchini kupitia fursa hizo, watakuwa sawa na Kenya na Afrika Kusini ukiachana na mataifa makubwa ya Uingereza na Marekani.
Tanzania na biashara za nje
Kwa kuzingatia faida na masilahi yatokanayo na uhusiano mzuri kati ya nchi na nchi, Tanzania imesaini mikataba ya makubaliano ya ushirikiano wa kibiashara na nchi mbalimbali ulimmwenguni.
Wizara ya Viwanda na Biashara inaeleza katika taarifa yake ya mwaka 2012 kuwa makubaliano hayo yamekuwa yakiiwezesha Tanzania kupata fursa za masoko ya upendeleo.
Mfano wa baadhi ya nchi ambazo zimeipa Tanzania fursa hizo ni Jumuiya ya Ulaya (EU) chini ya mpango wa kuzisaidia nchi maskini. Katika mpango huo, nchi maskini zinaruhusiwa kuuza katika soko la Ulaya bidhaa mbalimbali.
Wizara hiyo inasema ili kukuza biashara na uwekezaji nchini, Serikali ilikubali kusaini makubaliano ya umoja wa kibiashara na nchi kadhaa na sasa Uturiki inaonekana kupania mpango huo kwa nguvu zaidi.
Mpango wa Uturuki umelenga kuifanya Tanzania kuwa kituo kikuu cha biashara Afrika Mashariki. Eneo hili linajumuisha nchi tano, Kenya, Uganda, Burundi, Rwanda na Sudani Kusini
MWANANCHI.
No comments:
Post a Comment