Wednesday 18 March 2015

UKEKETAJI UNACHANGIA WAJAWAZITO KUJIFUNGUA KWA UPASUAJI


Ukeketaji, ni tatizo ambalo bado linaikabili dunia na hapa nchini, hali bado tete, hasa katika Mikoa ya Mara, Arusha, Manyara, Kilimanjaro, Dodoma na Singida, inayoelezwa kuwa, vitendo hivyo vimeendelea kushamiri kila siku.

Kukithiri kwa unyama huo, unadaiwa kuchangiwa na mambo mengi, ikiwemo ubunifu mpya unaofanywa na ngariba, wazazi, bibi wa mtoto husika na baadhi ya wahudumu wa afya, wasiokuwa waaminifu, mbele ya umma.
Kati ya njia zinazotumika katika kukeketa ni, wakati mtoto wa kike akiwa mchanga, kwa kufunga vyema uzi kwenye sehemu yake ya siri, kukata uke kwa kutumia kucha na kupaka sehemu hiyo kwa kutumia tumbaku; ili mradi tu, ngariba anahakikisha ametimiza lengo lake.
Asha Munjoli, ni mmoja wa washiriki wa kongamano la kitaifa la kupiga vita ukeketaji kwa wasichana na wanawake, lililofanyika Mkoani Singida hivi karibuni, anabainisha kuwa, miaka ya nyuma mila hiyo iliweza kudumu, kutokana na imani ya kabila lao.
Kongamano hilo, lililoandaliwa na chama cha wanahabari wanawake Tanzania (Tamwa) na kushirikisha wadau mbalimbali kutoka mikoa ya Mara, Dodoma, Manyara, Kilimanjaro, Arusha na Singida, lilikuwa la aina yake kufanyika mkoani Singida.
Mama Munjoli, anayetoka katika wilaya ya Ikungi, Mkoani Singida, ni wa kabila la ‘Kinyaturu’, ambalo anadai kuwa tangu enzi na enzi za mababu, msichana alikuwa lazima kwanza apitie hatua ya kukeketwa, ndipo anapata sifa ya kuitwa mwanamke.
Anasema, kutokana na mabadiliko duniani, mila hiyo hivi sasa imepitwa na wakati, kwani inamdhalilisha mwanamke, na anatoa wito kwa jamii inayoendeleza mila hiyo, kuachana nayo, ili kulinda utu wa binadamu.
“ Zamani kabisa, sisi hapa wanawake bila kukeketwa, ilikuwa mwanamke hajakamilika, lazima apitie hatua hii, akitoka kwenye unyago, basi hapo anakuwa mwanamke kamili, lakini leo hii mila hiyo imepitwa na wakati…nawaomba wanawake waachane na hii mila,” alisema.
Wakati serikali, mashirika, taasisi na vikundi mbalimbali vikipiga vita ukeketaji, mwakilishi mkazi wa shirika la umoja wa mataifa la idadi ya watu ( UNFPA ), Dk. Natalia Kanem, kupitia mwakilishi wake, Tausi Hassan, anasema, UNFPA inaunga mkono mapambano dhidi  ya ukeketaji.
Anasema, kulingana na taarifa ya Shirika la Afya Duniani (WHO), wanawake waliofanyiwa ukeketaji, wapo kwenye hatari kubwa zaidi ya kukumbwa na vifo, vitokanavyo na uzazi.
Anabainisha kuwa, kutokana na ukeketaji hivi sasa kuna ongezeko la wajawazito kujifungua kwa njia ya upasuaji, wanaofikia asilimia 31, kati yao asilimia 55 kutoka kundi hilo, watoto wao wapo kwenye hatari ya kufa, baada ya mama zao kujifungua.
“ Hali hii ni mzigo kwa sekta ya afya, ambayo pia inazo changamoto nyingine nyingi. Hivyo ili kutokomeza hali hii, hatuna budi kuingiza suala la ukeketaji katika kazi zetu, zinazohusiana na haki ya binadamu,” alisema Dk. Kanem.
Aidha kutokana na hali hiyo, Dk. Kanem, anaiasa jamii ambayo bado inaendekeza vitendo vya ukeketaji, kuhakikisha inaachana na mila hiyo, sambamba na kuwafichua wote ambao bado wanaendeleza mila ya kukeketa binadamu wenzao.  
Lakini je ukeketaji ni nini hasa, daktari bingwa na mshauri wa magonjwa ya wanawake na uzazi, katika hospitali ya mkoa Singida, Dk.Suleiman Muttani anasema, ukeketaji ni mila au desturi inayomdhalilisha mwanamke kwa kukata, kuondoa kipande kwenye sehemu ya siri (ukeni).
Hata hivyo baadhi ya makabila, hudai hufanya hivyo kutibu ugonjwa wa lawalawa na hupunguza hamu ya tendo la ndoa, ili kuachana na tabia ya umalaya.
Baadhi ya wanawake akiwemo Pili Idabu anasema kuwa, hata hivyo, sababu hizi zimeanza kutolewa katika miaka ya hivi karibuni, baada ya vyombo mbalimbali kupaza sauti zaidi, juu ya ukeketaji.
Dk. Muttani anafafanua kuwa, ili kudhihirisha tatizo la ukeketaji bado kubwa kwa baadhi ya mikoa nchini, asilimia 20.3 ya wanawake wanaokwenda hospitalini na vituo vya kutolea huduma ya afya mkoani Singida, wamebainika kukeketwa.
Anasema kuwa, kukeketwa ni kuondoa kidole kwenye uke, kukata mashavu madogo ili njia ya uzazi iwe ndogo, na hutekeleza zoezi hilo kwa kutumia zana mbalimbali ikiwemo mkasi, wembe, kisu, vipande vya chupa na mawe, jambo ambalo ni hatari sana kwa afya zao.
“ Wanawake wanne au hata zaidi hushika miguu na kuanza kukeketa, halafu wanampaka mafuta au mavi ya ng’ombe…ngariba hufanya kazi hii kwa watoto wenye umri wa miaka minne hadi kumi, pia mtoto mchanga hadi miaka mitano nao wanakeketwa,”anafafanua Dk. Muttani.
Ili kukomesha tabia hiyo, Mkurugenzi mtendaji wa TAMWA, Valerie Mssoka aliwaomba washiriki wa kongamano hilo, kukabili mila hiyo, ikiwemo kuwafuata wazee, ngariba na wote wanaojihusisha na zoezi hilo vijijini, ili wafikishwe kwenye vyombo vya dola.
“Wazee wetu, wazee wa mila wote wanaohusika na zoezi hili bovu, wafuatwe huko waliko, wadhibitiwe, ili kuondoa tatizo hili ndani ya jamii,” anasema Mssoka.
Hata hivyo Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto, Sophia Simba, akifungua kongamano hilo, anabainisha wazi kuwa serikali inayapa umuhimu wa pekee, matatizo yanayohusiana na ukatili dhidi ya binadamu, nchini.
Anasema, miongozo mbalimbali imeandaliwa, ikiwemo ule unaozuia na kudhibiti ukatili wa kijinsia, kupitia kamati za vijiji/mtaa, kata, na wilaya, unaohusisha uratibu na usimamizi wote unaohusisha masuala ya ukatili wa kijinsia.
Anafafanua kuwa, ukeketaji duniani unadhoofisha afya na ustawi wa wasichana takribani milioni tatu  kila mwaka, jambo ambalo ni hatari kwa ustawi wa maendeleo yao, familia, nchi na dunia kwa ujumla.
Aidha waziri Simba anasema zaidi ya wasichana na wanawake milioni 130 katika nchi 29 barani Afrika na Mashariki ya Kati, vitendo vya ukeketaji bado vimekithiri, huku athari kwa maisha yao zikiwa kubwa zaidi.
Ujumbe wa kimataifa, siku ya kupinga ukeketaji mwaka huu, umewalenga zaidi wahudumu wa afya, ukisema; ‘Uhamasishaji na ushirikishwaji wa wafanyakazi wa afya ili kuharakisha kutokomeza ukeketaji’. 
Kwenye kongamano hilo ilielezwa kuwa, asilimia 34 ya ukeketaji duniani, hufanywa na wahudumu wa afya, hali ambayo ni hatari katika kutokomeza vitendo hivyo, vilivyopitwa na muda

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!