Mwisho mwa wiki nilipata fursa ya kusafiri kuelekea mikoa ya kaskazini kwa shughuli maalum za kijamii. Tulisafiri kwa barabara, kuanzia Dar es Salaam kupitia Bagamoyo – Msata kuelekea Moshi.
Ilikuwa ni safari njema hasa kutokana na kuzidi kuimarika kwa barabara za lami. Kuna ujenzi mkubwa umefanyika kuijenga upya barabara ya kaskazini hasa kuanzia mkoa wa Tanga kuelekea Kilimanjaro. Kipande kirefu kimekamilika.
Kwa macho tu, muonekano wa barabara ambayo imekamilika kati ya Tanga na Kilimanjaro unafanana na ule wa kati ya Morogorogo na Iringa barabara ya kueleka Mbeya. Ninathubutu kusema kuwa hizi ni kati ya barabara bora kabisa ambazo zimejengwa katika kipindi cha hivi karibuni. Pongezi sana.
Ingawa siyo sawasawa kuzungumzia barabara kwa kuitazama kwa macho tu na kusema ni bora, muonekano hata hivyo unaweza kabisa kukupa picha halisi juu ya ubora wake.
Ukiendesha barabara kwenye barabara ya lami unaisikia lami kama iko sawa, gari linatulia barabarani, hakuna mawimbi, upana unaonekana kuwa mzuri kabisa, ukibahatika kuona eneo ambalo bado ujenzi unaendelea unaona ni kwa jinsi gani malighafi za kujengea barabara kama vile kokoto na kifusi vilivyo vya ubora. Siyo hayo tu, hata tabala la kokoto inayomiminwa na kushindiliwa inakupa imani kwamba kuna kitu cha maana kinafanyika.
Hata hivyo, ukifananisha barabara hizi, yaani kipande cha Tanga kwenda Kilimanjaro na ile ya Morogoro kwenda Iringa kwa upande mmoja na kipande cha barabara mpya ya Bagamoyo - Msata, unapata tatizo kama kweli wasimamizi wa barabara zote hizi ni wale wale, yaani Wakala wa Barabara (Tanrods) na Wizara ya Ujenzi kwa ujumla wake.
Ingawa barabara ya Bagamoyo – Msata ina changamoto nyingi na nzito hasa ujenzi wa madaraja mengi kuvuka bonde la mto Ruvu, bado ujenzi wa barabara hiyo una walakini mkubwa.
Ni kweli kwa muonekano madaraja yanayojengwa yanaonekana kuwa ni ya kiwango cha juu kwa maana ya ubora, lakini nachelea kusema kuwa barabara nayo ni ya ubora wa juu kama yalivyo madaraja hayo au kama zilivyo barabra za Tanga- Kilimanjaro au Morogoro –Iringa kuelekea Mbeya.
Barabara ya Bagamoyo - Msata ingawa haijazinduliwa rasmi kwa sasa inapitisha magari mengi yanayotoka Dar es Salama kwenda kaskazini. Hali hii inachangiwa pamoja na mambo mengine kero ya foleni ya barabara ya Morogoro kuanzia Ubungo -Kibaha, na ubovu wa eneo la Mlandizi-Chalinze.
Kwa mtu yeyote anayejali kushughulisha ubongo wake, barabara ya Bagamoyo – Msata ni bomu. Wakati bado haijazinduliwa rasmi, tayari imejaa mipasuko na kazi inayofanywa kwa sasa ni kuweka viraka.
Pengine ninaposema viraka watu hawaelewi vizuri, ngoja nizungumze lugha ya kueleweka. Jaribu kufikiria kuwa umekwenda kwa fundi wa nguo kupima suti mpya, ukachagua kitambaa, mkapatana bei, ukalipa kisha mkapeana ahadi siku ya kuchukua suti yako.
Sasa siku ya kuchukua suti unagundua kwamba pamoja na upya wake imejaa viraka. Upya wa hii suti unakuwa wapi katika mazingira hayo?
Kwa hakika barabara ya Bagamoyo – Msata haina tofauti na ukweli huu.kwamba ni suti mpya yenye viraka. Najua wapo watakaosema kuwa ni vema ikawekwa viraka kabla ya kuzinduliwa au kukabidhiwa, lakini suala la kujiuliza kama imewezekana kuwa na barabara bora ya Morogoro- Iringa kuelekea Mbeya na Tanga – Kilimanjaro katika kipindi cha utawala huo huo na wasimamizi wa wizra hiyo hiyo, tatizo ni nini kwa Bagamoyo - Msata?
Hakuna kitu kinauma kama kujengewa barabara ‘kanyaboa’, kwamba wananchi wanasadikishwa kwamba sasa wamepata ukombozi kwa kujengewa barabara ya kudumu ya lami, lakini baada ya muda mfupi tu usiozidi miaka mitano, barabara husika inakuwa mashimo matupu.
Haya tulipata kushuhudia hapa jijini Dar es Salaam katika barabara ya Kilwa. Ilijengwa, lakini hata kabla ya kukabidhiwa ikawa imeumuka kama unga wa ngano uliowekwa amira. Hadi leo bado barabara ya Kilwa ni miongoni mwa barabara za ovyo kabisa katika jiji la Dar es Salaam.
Tunapozunguzia habari ya barabara za kudumu za lami, tunazungumzia matumizi ya matrilioni ya shilingi kodi za wananchi.
Tunazungumizia jasho la wananchi. Tunazungumzia juhudi za kila mwananchi katika kuchangia gharama za miundombinu hii. Hata kama kuna mikopo kutoka nje, uhakika ni kwamba watakaolipa mikopo hiyo ni wananchi wa Tanzania, iwe kesho, keshokutwa au miaka mingi ijayo. Kwa maana hiyo tunapotafakati ubora wa barabara zetu tujielekeze kwenye uhalisia huo. Jasho la wananchi kupitia kodi.
Mwaka jana gazeti la NIPASHE liliandika ripoti maalum juu ya ujenzi wa barabara ya Morogoro katika mradi wa magari ya mwendo kasi (Darts). Katika uchunguzi wake gazeti liligundua kuwa barabara hiyo ilikuwa imepunguzwa upana. Yaani kwa sasa hivi hailingani na ile ya awali iliyokuwako ikabomolewa na kujengwa upya.
Habari ya gazeti hilo ilisema kuwa zaidi ya Sh. bilioni 4 zilikuwa ama zimechukuliwa na wajanja au zimemezwa na mkandarasi katika ujenzi wa barabara yenye urefu wa kilometa 15 tu. Kiasi hicho cha fedha ni kadirio la chini kabisa.
Inajulikana kwamba watendaji serikalini walisema kuwa ujenzi wa barabara ya Darts ungekwenda sambamba na kuhamisha barabara ya Morogoro ilivyokuwa awali, yaani kubakia na upana ule ule. Leo hii kila mtu ni shahidi, asimame mtu adai kwamba upana wa barabara ya Morogoro leo ni ule ule wa awali kama ilivyojengwa miaka ya 90 chini ya utawala wa Rais Benjamin Mkapa.
Ninatoa mifano ya barabara hizi kama kielelezo tu kuonyesha kwamba pamoja na kazi nzuri ya ujenzi wa barabara unaoendelea kila kona katika nchini hii, pia kuna ulaji wa ‘kufa mtu’ unaoendelea vivyo hivyo. Wasimamizi wanajua, wanaona, lakini wamekaa kimya.
Maandiko ya Wakristo yanasema kuwa kukaa kimya wakati maovu yanatendekea mbele yako ni sawa kabisa na kushiriki kutenda uovu huo. Ndiyo maana tunashauriwa kutoutazama uovu. Ni wajibu kuukemea, kusema wazi ili kuchochea chembechembe za mabadiliko na wongofu unaostahili mbele ya jamii.
Haifai, hakubaliki na ni fedheha kupokea barabara mpya iliyojaa viraka. Ni fedheha na uporaji uliopindukia kujenga barabara chini ya kiwango kwani kufanya hivyo siyo kukiibia kizazi cha sasa tu, bali hata kijacho kwa kuwa nyingi ya barabara hizi ni mikopo kutoka nje italipwa kwa miaka mingi ijayo na vizazi vijavyo.
NA JESSE KWAYU
No comments:
Post a Comment