Sifa hiyo haitokani na ukweli kwamba ndiye mkurugenzi wa Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania (Tamwa), bali shuruba alizokutana nazo katika kutekeleza majukumu yake ya uandishi, hasa katika maeneo hatarishi ya vita kwenye nchi ambazo mwingine angefikiria mara mbili kwenda.
Iraq, Burundi, Congo, Sudan na Rwanda ni maeneo ambayo alipangiwa kwenda kutoa taarifa za mapigano baina ya wenyewe kwa wenyewe au nchi na nchi, na kote alitekeleza majukumu hayo kwa ujasiri na umakini na kujizolea sifa kama mmoja wa waandishi wa habari mahiri wa Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC).
Mbali na vita, alimudu kwenda kufanya utafiti uliohusisha mahojiano na waganga wa jadi na mangariba kuhusu mila potofu ya ukeketaji katika maeneo ambayo ni hatari kutokana na ukweli kwamba wanaotekeleza mila hiyo wanasakwa na Serikali na hivyo kumchukulia yeyote anayewafuatilia kuwa ni adui.
Na sasa, akiwa mkurugenzi wa Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake (Tamwa), Msoka amekubali kubeba jukumu jipya la balozi wa kampeni ya kupiga vita ndoa za utotoni inayoitwa CEFM, ikiwa ni tuzo aliyopewa na ubalozi wa Canada nchini Tanzania.
“Kwangu peke yangu itakuwa ni ngumu, lakini kwa kushirikiana na wadau na hasa waandishi wa habari, kazi hii itakuwa rahisi,” alisema Msoka katika mahojiano na jarida hili alipozungumzia jukumu hilo jipya la kupinga ndoa za utotoni ambazo sehemu kubwa ya jamii inaziona za kawaida na haziko tayari kushirikiana kufichua uovu huo.
“Nadhani nitaanzia katika Katiba Mpya Inayopendekezwa ambayo inasema umri wa kisheria wa mtoto uwe kuanzia miaka 0- 18. Na hili sitaliacha hivi hivi, kupita ama kutopita kwa katiba, kwangu haitaniathiri, nitaendelea kupambana mpaka nione tunafanikiwa,” alisema mwandishi huyo wa habari wa siku nyingi.
“Kazi hii nitaifanya sambamba na kuzuia aina zote za mila potofu zinazotekelezwa nchini ikiwamo ya ukeketaji unaofanywa na baadhi ya makabili kama hatua ya kumuingiza binti katika hatua ya utu uzima hata kama ana umri wa miaka minane eti anachukuliwa kuwa tayari anaweza kubeba majukumu ya ndoa. Hili sitalikubali nitapambana mpaka mila hizi zifutwe.”
Msoka, ambaye ni mama mwenye watoto watatu, anasema alianza harakati zake za kutetea haki ya mama na mtoto baada ya kuguswa na matatizo na changamoto mbalimbali zinazowakabili, akiwa na lengo la kutaka kuona siku moja usawa na haki katika makundi hayo unafikiwa.
Kwanini awe Valerie Msoka
CEFM inatambua mchango uliotolewa na mtu ambaye ametumia jitihada na muda wake mwingi katika kutetea haki za watoto na ambaye amekuwa akiunga mkono harakati za kuhakikisha taifa linakuwa mahali salama kwa watoto, hasa wa kike katika kizazi cha sasa na kijacho.
Msoka ndiye aliwezesha kuundwa kwa ukanda huru wa kukomesha ndoa za utotoni nchini Agosti, 2014, kwa kuwa mwezeshaji wa tukio hilo lililofanyika jijini Dar es Salaam mbele ya Rais wa awamu ya Tatu, Benjamin Mkapa, Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto, Sophia Simba, mke wa aliyekuwa Rais wa Msumbiji Samora Machel, Mama Graca pamoja na wakuu wa balozi mbalimbali nchini na mashirika ya Umoja wa Mataifa.
Pia, aliendelea na harakati hizo mwaka jana baada ya kuteuliwa kuwa mjumbe wa Bunge Maalumu la Katiba, kufikisha na kutetea hoja ya kuingizwa kwa umri wa mtoto unaotambuliwa kisheria ndani ya Katiba.
Aliweza pia kutetea masuala ya usawa ndani ya kamati ikiwa ni pamoja na haki ya kumlinda mtoto wa kike na wanawake dhidi ya mila potofu ikiwa ni pamoja na ndoa za utotoni, ukeketaji, haki ya kumiliki ardhi na uongozi.
Binafsi analizungumziaje jukumu hilo
Msoka anasema kutambuliwa kwake kuwa balozi wa kampeni ya Kupinga Ndoa za Utotoni, kumempa hamasa zaidi na kumfanya aongeze jitihada, nguvu na kutoa muda wake zaidi katika kutetea haki za watoto nchini.
Mama huyu, aliyewahi kufanya kazi Radio Tanzania, anasema ubalozi aliopewa ni mwanzo wa juhudi zinazoendelea kuchukuliwa ili kuwalinda watoto hasa wasichana kwa sababu ndoa za utotoni zinasababisha vifo na madhara makubwa kwao hata kuwatumbukiza katika dimbwi la umaskini.
Akizungumzia kazi yake ya uandishi wa habari, Msoka anasema ni kazi ngumu inayohitaji kuipenda na kujitoa ili upate mafanikio.
“Bila kuipenda na juhudi, utakuwa mtu wa kuikamata na kuiachia,” alisema akisisitiza kuwa juhudi zake na mapenzi kwa kazi hiyo ndizo zilizomfanya afikie hapo alipo.
“Kazi yangu imenifanya niyafikie hata maeneo mengine ambayo ni vigumu kwa mwanamke kwenda kufanya kazi kama yale ya vita kutokana na changamoto zake za kikazi na kimazingira,” anasema Msoka.
No comments:
Post a Comment