Monday, 23 March 2015

MVUA YAUA 5 DAR ES SALAAM YAJERUHI



HALI ni tete katika jiji la Dar es Salaam, kutokana na mvua ya masika iliyonyeshwa kwa siku tatu na kusababisha vifo vya watu watano, huku nyumba nyingi zikiwa zimezingirwa na maji.



Maeneo yaliyoathirika zaidi ni Buguruni kwa Mnyamani na eneo la Jangwani katika Manispaa ya Ilala, ambako nyumba nyingi na barabara zimeathirika.
Sehemu nyingine za jiji zimezingirwa na maji kutokana na kuziba kwa mitaro na mifereji, ikiwa ni athari ya utupaji taka ovyo na pia miundombinu duni.
Hata hivyo, kwa mujibu wa Mamlaka ya Hali ya Hewa nchini (TMA), mvua kubwa zaidi zinatarajia kuendelea kunyesha mpaka Jumatano.
Kutokana na athari za mvua zinazoendelea kunyesha, Mkuu wa Mko wa Dar es Salaam, Said Meck Sadiki (pichani) jana aliongoza kikosi cha uokoaji katika eneo la Buguruni kwa Mnyamani, ambako nyumba 250 zilizingirwa na maji, jambo ambalo vikosi vya uokoaji vililazimika kufanya kazi ya kuwanasua watu waliokuwa wamekwama katika nyumba zao.
Uokoaji huo ambao mpaka jana jioni ulikuwa ukiendelea, ulisaidiwa na wafanyakazi wa kampuni ya China Railway Jianchang Engineering (CRJE), inayojenga Daraja la Kigamboni, kwa kutoa vifaa na kushiriki katika uokoaji wa watu hao.
Sadiki alisema mpaka jana mvua hizo zimesababisha vifo vya watu watano, akiwemo mtu mmoja aliyesombwa na maji, mwingine aliyeangukiwa na ukuta na watatu ambao wamenaswa na umeme baada ya nguzo ya umeme kuanguka Mbagala Mzambarauni katika Manispaa ya Temeke.
“Wananchi wanatakiwa kuachana na tabia ya kutupa taka ovyo katika maeneo ya mitaro, kwani ndiyo yaliyochangia maji kuleta madhara, na walio mabondeni bado nawasihi kuondoka maeneo hayo,” alisema.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, Camillius Wambura alisema mtu mmoja ambaye hajatambuliwa mwenye umri kati ya miaka 45 hadi 50, anasadikiwa kusombwa na maji katika mto Goba.
Aidha, alisema katika eneo la Mwananyamala, mlemavu wa viungo Edward Warioba (22) aliangukiwa na ukuta usiku wa kuamkia jana akiwa amelala katika nyumba iliyokuwa imeingia maji na kulowanisha kuta zake.
Wambura alitaka wananchi kuchukua tahadhari kwa watoto wao na wahakikishe wanakwenda na kurudi kutoka shule wakiwa salama.
Eneo la Jangwani, kati ya Magomeni na Faya (Kariakoo), pia nyumba kadhaa zilizingirwa na maji huku baadhi ya wakazi wa maeneo hayo wakihamia barabarani ili kujinusuru.
Lakini eneo la Jangwani, karibu na klabu ya Yanga, walionesha kutokuwa na wasiwasi na mvua zinazoendelea kwa madai kuwa hazijafikia kiwango cha kuwa na athari kwao.
“Kipimo chetu ni hiki hapa, (wanaonesha alama) maji yakifika kimo hiki tunajua wakati wa kuhama nyumba zetu umewadia lakini kwa sasa maji haya hayana madhara yoyote,” alisema mkazi wa eneo hilo, Huseni Juma.
Akizungumza jana Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), Dk Agnes Kijazi alisema mvua kubwa zaidi ya milimita 50 ambazo zimenyesha sasa, zinatarajia kuendelea kunyesha ndani ya saa 24 zijazo huku mvua hizo kuendelea kunyesha hadi Machi 25, mwaka huu.
“Utabiri unaonesha kuwa mvua kubwa za zaidi ya milimita 50 zitaendelea kunyesha siku tatu zijazo. Hivyo ni vema wananchi wakaendelea kuangalia utabiri unaotolewa na mamlaka kila siku ili kujiepusha na madhara,” alisema.
Awali, TMA ilitoa mwelekeo wa mvua za masika kwa kipindi cha Machi, Aprili na Mei na kuwa kipindi hicho mvua zilitarajiwa kuwa ya kuridhisha katika maeneo mengi ya nchi.

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!