Friday, 20 March 2015

MGANGA WA KIENYEJI AKAMATWA NA FUVU LA BINADAMU


Wakati kamatakamata ya waganga wa kienyeji ikiendelea kupamba moto katika mikoa ya Kanda ya Ziwa, mmoja amenaswa akiwa na viungo vya binadamu, kikiwemo kichwa ambacho bado kilikuwa na nywele zake.



Mganga huyo, Nyamizi Makunga (70), mkazi wa Kijiji cha Igurubi wilayani Igunga, Tabora, alitiwa mbaroni juzi. Mbali na viungo hivyo, pia alikutwa na vifaa vingine, zikiwemo nyara za serikali.

Mwenyekiti wa Kijiji cha Igurubi, George Henry, alisema Makunga alikamatwa nyumbani kwake kutokana na msako mkali unaendelea kwa lengo la kuwabaini waganga wanaofanya ramli chonganishi.

Msako huo umetokana na kukithiri kwa mauaji ya watu wenye ulemavu wa ngozi, ambapo serikali katika kubaini chanzo, imekuwa ikisaka waganga wanaotuhumiwa kufanya ramli hizo.

Henry alisema polisi walifanikiwa kumnasa Makunga kutokana na taarifa kutoka kwa raia wema, ambapo walipofanya msako walikuta fuvu la kichwa la binadamu likiwa na nywele zake.

Mbali na fuvu hilo, polisi pia walikuta kipande cha mfupa wa binadamu, mkia wa nyumbu, gamba la kobe na ngozi za wanyama mbalimbali.

Wananchi wa Kijiji cha Igurubi, wamepongeza msako unaofanywa na polisi kuwatia mbaroni waganga ambao ndio chanzo cha kushamiri kwa mauaji ya albino.

Pia walisema kwa muda mrefu Makunga amekuwa kikwazo cha maendeleo kwenye eneo hilo kutokana na kufanya mambo kinyume na kwamba wananchi wamekuwa wakimwogopa.

Alipohojiwa, Makunga alikiri viungo hivyo ni vya binadamu na kuwa aliachiwa na baba yake ili kuendesha shughuli za uganga.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tabora, Suzana Kaganda, alithibitisha kukamatwa kwa mganga huyo akiwa na viungo vya binadamu.

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!