Saturday 21 March 2015

MAAJABU YA MAPANGO YA AMBONI



NI umbali wa kilometa nane kutoka Tanga Mjini kwenda mapango ya Amboni yaliyoko eneo la Kiomoni, kata ya Kiomoni.
Njia za kufika kwenye mapango hayo yaliyoko Tarafa ya Chumbageni katika Mkoa wa Tanga, zinapita katikati ya kijiji cha Kiomoni . 


Nikiwa miongoni mwa watalii wa ndani; ambao ni kundi la wadau wa Muungano wa Utepe Mweupe na Uzazi Salama (WRATZ) waliokuwa mkoani Tanga, tunapita barabara ya changarawe iliyo upande wa kushoto, meta 200 baada ya kuvuka daraja la Utofu kwenda kwenye mapango hayo.
Njia nyingine kwenda mapango hayo, iko kilometa 1.5 kutoka Daraja la Utofu katika kituo cha zamani cha ukaguzi wa mazao ya misitu. Licha ya eneo la mapango kuwa zuri kwa kupumzikia, Mhifadhi Mambo ya Kale, Mapango ya Amboni, Jumanne Gekora anasema pia ni zuri kwa utafiti wa kihistoria, kijiografia na kijiolojia.
Mapango hayo ya utalii yana milango miwili ya kuingilia. Inachukua takribani nusu saa kutalii kupitia mlango mkubwa kabla ya kufika mlango mwingine wa kutokea nje . Ndani ya pango kubwa, viko vituo vipatavyo 13 vyenye visamkasa na maajabu katika historia . Pango dogo, lina mlango mmoja na haichukui dakika zaidi ya tano kuingia na kutoka.
Maeneo maalumu yaliyotengwa kwa ajili ya kuomba au kutambikia mizimu, ni miongoni mwa vivutio vya utalii. Mtembeza watalii wa mapango hayo, Peter Wambura anaonesha vitu vingi vinavyohusiana na imani za kijadi vilivyowekwa na watu mbalimbali kama matambiko.
Hayo yanashuhudiwa kwenye kituo cha kwanza ndani ya mapango hayo yaliyotokana na mabadiliko ya nguvu za asili zilizobadilisha maumbile ya miamba ya chokaa takribani miaka milioni 150 iliyopita. Zinashuhudiwa chupa zenye marashi, sahani na hata vipande vya nguo. “Wapo ambao huja na fedha taslimu na kuziweka eneo hili la matambiko,” anasema Wambura .
Iingawa haijulikani mapango yaligunduliwa lini, taarifa zilizopo ni kwamba, watu wa makabila yaliyoishi jirani na eneo hilo; Wabondei, Wasambaa, Wadigo na Wasejeju inaelezwa wamekuwa wakiyatumia kwa ajili ya matambiko ya mizimu tangu karne ya 16. “Eneo hili la mapango kwa wakati huo, lilijulikana kama eneo la mzimu wa mabavu,” anasema Mhifadhi Gekora.
Watu wanaoamini habari za nguvu za mizimu katika kutatua matatizo ya uzazi, kuongeza kipato, kutibu magonjwa, hutoka sehemu mbalimbali za Afrika Mashariki kwenda kuomba au kutambika mzimu katika vijipango mbalimbali. Mtembeza wageni, Wambura anaonesha pia miamba yenye maumbo ya kuvutia yanayofanana na kochi, meli, mamba, tembo, sanamu ya Bikira Maria.
Iko pia michoro inayofanana na unyayo wa mguu wa binadamu na wanyama kadhaa ikisadikiwa kutokana na uchafu uliosababishwa na popo ambao wamekuwa wakitumia mapango hayo kama makazi yao kwa kipindi kirefu. Katika kituo cha tisa, lipo umbo mithili ya kibra cha msikiti. Vile vile ipo herufi inayotafsiriwa neno la Kiarabu lenye maana ya Mungu.
Jiwe kubwa lenye muundo wa ramani ya Afrika ni kivutio kingine ndani ya pango hilo. Linaonesha lilidondoka kutokana na sehemu ya juu kuonesha hilo. Ipo pia miamba inayokua au kuongezeka kutokana na mabadiliko ya kikemikali katika miamba ya chokaa. Inaonekana miamba inayokua kutoka juu kuelekea chini ikiwa imeota kwenye kuta za pango au miamba inayoongezeka kwa kuelekea juu.
Wakati huo huo simulizi mbalimbali zinaongeza mvuto wa kutembelea mapango hayo. Mojawapo, ni inayotaja kuwahi kuwapo kwa njia za kwenda Mombasa, Kenya kupitia mapango hayo. Katika kituo cha sita, inaonesha kuwapo njia panda. Mojawapo ikisadikiwa kwenda eneo la Maweni, mkoani Tanga na nyingine ikienda Mombasa.
Wambura anasema, hata hivyo, hakuna aliyewahi kupita njia hizo kuhakikisha ukweli juu ya hilo. Simulizi nyingine inahusu wazungu wawili na mbwa wao walioonekana mwaka 1941 wakielekea mapangoni. Inadaiwa wenyeji waliwashauri wasiingie na mbwa. Walishauriwa waingie na mwongozaji anayejua njia za mapangoni.
“Ushauri huo ulipuuzwa na walivyoingia, hawakuwahi kuonekana tena wakitoka katika eneo hili bali mbwa wao alikuja kuonekana kandokando ya mlima Kilimanjaro huko mkoani Kilimanjaro,” anasema Wambura akionesha shimo ambako watu hao wanadaiwa kutumbukia ambalo hadi sasa, hakuna aliyewahi kuingia.
Simulizi nyingine maarufu ni kuhusu watu wawili waliotumia kituo namba tatu ndani ya pango kubwa kama sehemu yao ya kujificha kati ya mwaka 1992 na 1956 wakiendesha harakati za kupambana na walowezi waliokuwa wamewekeza katika maeneo ya Tanga. Watu hao ni Osale Otango (Samuel Otango) na Paulo Hamis wanaodaiwa, walipora mali na kutishia maisha ya walowezi.
“Serikali ya kikoloni iliwatambua kama wahalifu na kujaribu kuwakamata bila mafanikio kwa kipindi kirefu,” Wambura anakariri simulizi hizo. Pango ambako watu hao walidaiwa kuishi, linaonekana mithili ya chumba kidogo chenye urefu kwenda juu ambako ndani yake,walitengeneza chanja na kujificha humo kiasi cha wakoloni kutowaona walipoingia mapangoni kuwasaka.
Simulizi zinaonesha, mwaka 1957, Hamisi alipigwa risasi maeneo ya Lushoto na kufariki na mwaka uliofuata (1958), Otango naye alipigwa risasi na kufariki huko huko Lushoto ambako makaburi yao yanadaiwa kuwako. “Wananchi wa kawaida wanawakumbuka kama mashujaa walioendesha harakati za ukombozi wa watu wanyonge kutoka katika mikono ya walowezi na watawala wa kikoloni,” inaelezwa.
Simulizi juu ya watu hao, zinapatikana katika kituo cha mwisho ndani ya pango hilo kubwa kabla ya kuwasili eneo maarufu kama Uwanja wa Ndege. Katika uwanja wa ndege, iko sura mithili ya ndege ya abiria ambako watalii huongozwa kupanda ngazi kwenda tundu dogo la kutokea nje ya pango hilo na kuhitimisha utalii.
Watembeza wageni wanafahamisha kwamba, yako mapango mengi ndani ya pango hilo kuu isipokuwa yatumikayo kwa utalii ni machache kwa ajili ya usalama. Yeyote anayetembelea mapango hayo na kukamilisha vituo vyote, hawezi kusahau njia nyembamba. Eneo hilo ni gumu hasa kwa watu wanene au warefu kutokana na kichochoro kilivyo chembamba sana kabla ya kutokea eneo lingine.
“Ukimsimulia mtu kwamba umekwenda mapango ya Amboni, kwa aliyewahi kutalii hapa, lazima atakuuliza umepita njia nyembamba?,” anasema Wambura. Pamoja na visamkasa na maajabu ndani ya mapango hayo ya utalii, kasi ya ujio wa watalii unatajwa kutoridhisha. Wizara ya Maliasili na Utalii inashauriwa kuyatangaza kikamilifu badala ya kuelekeza nguvu kwenye mbuga za wanyama pekee.
Kwa mujibu wa Mhifadhi wa Mambo ya Kale wa Mapango ya Amboni, Gekora, wastani wa watalii 65 ndani 65 na mmoja wa nje ya nchi, hutembelea mapango hayo kwa mwaka; idadi inayotajwa kuwa ni ndogo. Gekora anakiri eneo hilo la kitaifa la utalii kutotangazwa na kunadiwa kama ilivyo maeneo mengine ya utamaduni yaliyo chini ya urithi wa dunia kama vile mji mkongwe wa Zanzibar, Bagamoyo na Olduvai Gorge .
“Urithi wa utamaduni unaotangazwa na kutembelewa zaidi ni ule wa urithi wa dunia. Maeneo haya ya utalii yaliyo katika hadhi ya kitaifa, bado kiwango cha kutembelewa na watalii ni kidogo,” alisema Gekora. Lydia Kamwanga, ni mmoja wa watalii wa ndani katika mapango hayo anayeshauri yatumike kuvuta uwekezaji mkoani Tanga ikiwemo ujenzi wa hoteli.
Lydia ambaye ni Ofisa Mawasiliano wa Muungano wa Utepe Mweupe wa Uzazi Salama (WRATZ) aliyeongozana na wadau wa utepe huo kufanya utalii wa ndani, anashauri “Watengeneze wavuti, vipeperushi maalumu vinavyohusu mapango haya.” Anashauri pia waajiriwe wafanyakazi wenye weledi kwa ajili ya eneo hilo la utalii.
Suala lingine linalosisitizwa kuzingatiwa, ni usalama. Inashauriwa huduma ya kwanza na wataalamu wa masuala ya afya, wawe karibu kukabili dharura zinazoweza kujitokeza kwa watu wanaoingia ndani ya pango hilo. “Inawezekana mtu akapata tatizo ndani ya pango kama vile kukosa hewa ya kutosha au shinikizo la damu.
Inatakiwa awepo mtu wa huduma ya kwanza na hata hawa watembeza watalii, wawe na vifaa vya huduma ya kwanza,” mtalii mwingine anashauri. Mapango ya Amboni, yametokana na mabadiliko ya nguvu za asili zilizobadilisha maumbile ya miamba ya chokaa kama miaka milioni 150 iliyopita

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!