Friday, 27 March 2015

KCMC KCRI KUTUMIA TEKNOLOJIA MPYA KUTAMBUA VIMELEA VIPYA


Tangu kuanzishwa kwake mwaka 2009, Taasisi ya Utafiti ya Kilimanjaro (KCRI) ya Shirika la Msamaria Mwema (GSF), iliyopo KCMC, imekuwa ikijenga uwezo wake wa kufanya tafiti ambazo ni kipaumbele kwa taifa.

Imeweza kusomesha wataalamu wake sehemu mbalimbali duniani kama vile Marekani, Uingereza, Uholanzi na Denmark.
Imeweza pia kuongeza miundombinu ya kufanyia tafiti hizo, ili kupata vielelezo sahihi vya kufahamu zaidi magonjwa pamoja na matibabu.
Kuanzia mwaka 2013, KCRI ikishirikiana na washirika wake kutoka Denmark (DTU) ilianza kujijengea uwezo wa utambuzi wa magonjwa kwa kutumia teknolojia mpya ya vinasaba ambayo inajulikana kama Whole Genome Sequencing (WGS).
Ili kufanikisha kasi ya utambuaji wa magonjwa, KCRI ilifunga mashine kadhaa zenye uwezo na teknolojia za kisasa.
KCRI inatumia mashine ya miseq ambayo ni ya kwanza kuletwa na kuanza kufanya kazi hapa Tanzania. Pia ni mojawapo ya mashine chache sana ambazo zipo Afrika.
WGS ni njia bora zaidi kuliko njia nyingine katika uchunguzi na utafiti utumiao vinasaba (DNA) kwa ajili ya utambuzi wa vimelea vinavyosababisha magonjwa.
Katika nchi zilizoendelea, hutumia mashine za namna hiyo katika huduma za afya, utafiti, ufuatiliaji na udhibiti wa magonjwa ya milipuko, kama vile kipindupindu na kifua kikuu.
Uchunguzi wa kutumia WGS unawezesha kusoma mtiririko mzima wa vinasaba vya kimelea chote.
Mpangilio wa vinasaba ni mtiririko wa taarifa nyeti sana zinazotumiwa na kimelea kuishi ndani ya mwili wa binadamu.
Mojawapo ya changamoto zinazoikabili sekta ya afya ni ongezeko kubwa la vimelea vyenye usugu dhidi ya dawa zitumikazo.
Pamoja na adha za kuchelewa kupona au dawa kushindwa kufanya kazi, usugu wa vimelea huleta mzigo mkubwa hasa kiuchumi.
Shirika la Afya Duniani (WHO) linasema tatizo hili linazidi kuwa tishio na hatari kwa nchi zinazoendelea, kama Tanzania, tatizo la usugu dhidi ya dawa linaongezeka.
Moja ya visababishi vya usugu wa vimelea ni kushindwa kupata dawa sahihi na kuanzisha matibabu pasipo kujua asili ya kimelea. Tungekuwa tunatambua asili ya kimelea kinachosababisha ugonjwa, ingekuwa rahisi kufanya uamuzi sahihi wa dawa yenye uwezo wa kutibu kimelea husika.
Njia ya kawaida ya utambuzi
Mara nyingi sampuli zinazoletwa maabara za afya kwa utambuzi wa vimelea vya magonjwa ni pamoja na damu, mkojo, usaha, makohozi na kinyesi.
Mara baada ya sampuli hizi kupokewa maabara, mtaalamu wa maabara huchagua aina ya virutubisho vinavyofaa kwa ajili ya kuotesha vimelea kutoka kwenye hiyo sampuli. Hatua hii ni muhimu kwa maana siyo aina zote za kirutubisho zinafaa kuotesha kila aina ya kimelea.
Baada ya kutambua aina ya virutubisho vifaavyo kwa kila kimelea, mtaalamu wa maabara huzipanda hizi sampuli na kuziweka kwenye mashine yenye kiwango maalumu cha halijoto na hewa ya oksijeni au kabondayoksaidi. Viwango maalum vya halijoto na hewa ni muhimu kwa uoteshaji na ukuaji wa vimelea hivi.
Aina fulani ya vimelea huhitaji kiasi fulani cha oksijeni pekee au mchanganyiko fulani wa oksijeni na kabondayoksaidi au kiasi fulani cha kabondayoksaidi pekee kwa ukuaji wake.
Kutegemeana na aina ya kimelea, muda wa kusubiri majibu tangu sampuli kupokelewa maabara hadi vimelea kuota, unaweza kuwa ni siku mbili hadi wiki kadhaa.
Kiasi hiki cha muda ni kwa ajili ya vimelea vinavyoweza kuoteshwa maabara kirahisi. Hii ni kutokana na ukweli kwamba vimelea vingine kama virusi, haviwezekani kuotesha kwa kutumia virutubisho vya maabara.
Utambuzi wa vimelea hivi visivyooteshwa kwenye virutubisho vya maabara huleta changamoto kubwa zaidi kwa njia hizi za kawaida.
Utambuzi wake hutegemea zaidi RDT na njia zingine ambazo ni ngumu na za gharama kubwa zaidi kwa maabara zetu.
Baada ya vimelea kuota, hatua inayofuata ni utambuzi wa vimelea kwa njia iitwayo Gram stain.
Njia hii hutumika kama utambuzi wa awali na husaidia kujua mwonekano na umbile la kimelea.
Kimelea kikishatambulika umbo lake, hufuatia utambuzi mwingine unaoweza kubaini aina hasa ya kimelea na kujua uwezo wake akiwa ndani ya mwili wa binadamu. Kitaalam njia hizi kwa pamoja huitwa biochemical tests.
Baada ya kumtambua aina ya kimelea na uwezo wake akiwa ndani ya mwili wa mwanadamu, hatimaye hufanyika utambuzi wa dawa ambayo ina uwezo mkubwa wa kuviangamiza vimelea.
Kila kundi la vimelea huwa na namna ya pekee ya utambuzi wa dawa yenye uwezo wa kiviangamizi kirahisi apewapo mgonjwa.
Utambuzi wa dawa gani inafaa huchukua hadi siku mbili tangu vimelea vilipoota. Inahitaji utaalamu na uzoefu mkubwa sana ili kuweza kufikia hatua hii kwa ukamilifu na kwa ufasaha.
Imeandaliwa na Taasisi ya KCMC-KCRI, mkoani Kilimanjaro.

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!