Jeshi la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, limemtaka Askofu wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, Josephat Gwajima kuripoti haraka Kituo Kikuu cha Polisi, Dar es Salaam kutoa maelezo kuhusu tuhuma za kashfa na matusi dhidi ya Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo.
Mapema wiki hii, mitandao mbalimbali ya kijamii kama vile WhatsApp ilisambaza sauti ya Askofu Gwajima akitoa maneno makali ya kumkashfu Kardinali Pengo.
Kamanda wa kanda hiyo, Kamishna Suleiman Kova kupitia taarifa yake kwa umma, alimtaka Askofu Gwajima kujisalimisha kituoni hapo na kuripoti kwa Mkuu wa Upelelezi wa Kanda Maalumu ya Dar es Salaam.
Kadhalika, taarifa hiyo ilieleza kuwa Kanda Maalumu ilipokea malalamiko ya kukashifiwa kwa Kardinali Pengo na jalada la uchunguzi limefunguliwa na upelelezi wa shauri hilo unaendelea.
“Baada ya tukio hilo juhudi mbalimbali zimekuwa zikifanyika katika hali ya kawaida ili kumpata Askofu Gwajima bila mafanikio, hivyo yeye mwenyewe sasa anatakiwa kwenda kuripoti kwa Mkuu wa Upelelezi wa Kanda Maalumu ya Dar es Salaam bila kukosa,” alisema Kamishna Kova.
“Ni muhimu sana kwa Askofu Gwajima kuripoti yeye mwenyewe badala ya kutafutwa au kukamatwa ili ajibu tuhuma hizo kutokana na nafasi yake katika jamii,” aliongeza.
Machi 14, mwaka huu, Kardinali Pengo akizungumza katika ibada ya Kwaresima kwa Wanawake Wakatoliki Tanzania (Wawata), alitofautiana na Jukwaa la Wakristo linalojumuisha Baraza la Maaskofu Katoliki (Tec), kuhusu aina ya kura inayostahili kupigiwa Katiba Inayopendekezwa.
Wakati Jukwaa la Wakristo liliwataka waumini wake kuipigia Katiba Inayopendekezwa kura ya hapana, Kardinali Pengo alisema waisome na kuielewa na kupiga kura inayostahili kwa jinsi watakavyoona wao.
Kardinali Pengo alisema wao wakiwa viongozi wa watu, hawana mamlaka wala uwezo huo, bali wenye uwezo ni wananchi wenyewe.
Kauli ya Pengo ndiyo iliyoamsha hasira ya Gwajima na kutoa matamshi makali.
MWANANCHI.
No comments:
Post a Comment