Shughuli za uchimbaji wa madini ya bati kwa wachimbaji wadogo mkoani Kagera sasa zinakabiliwa changamoto mpya ya kushuka kwa bei baada ya kuwapo kwa kile kinachoelezwa kuwa ni agizo la kuzuia wanunuzi binafsi wa bidhaa hiyo.
Wachimbaji kadhaa wa madini hayo wameiambia NIPASHE kuwa hali imezidi kuwa ngumu kwao kwani awali, licha ya kutumia nguvu nyingi kuchimba madini hayo kwa kutumia zana duni, lakini walikuwa wakifarijika kwa kujiingizia kipato kikubwa kutokana na ushindani wa wanunuzi kutoka nchi mbalimbali kama Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Uganda, Rwanda na kwingineko. Lakini sasa fursa hiyo imetoweka baada ya kuwapo kwa zuio dhidi ya wanunuzi kutoka nje na badala yake kujikuta wakiwa na mnunuzi mmoja tu, ambaye ni Shirika la Madini la Taifa (Stamico).
Waathirika wa mabadiliko hayo ya mfumo wa soko kwa madini ya bati ni pamoja na wachimbaji walioko katika machimbo ya madini yaliyopo eneo la Kabingo, Kijiji cha Nyakizumbula, Wilaya ya Kyerwa mkoani Kagera.
Fabian Fredy ni mmoja wa wachimbaji hao. Anasema kuwa hatua ya serikali kuzuia wanunuzi kutoka katika nchi za Rwanda, Uganda na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na kuwalazimisha kuuza madini hayo Stamico kumemuathiri kwa kiasi kikubwa.
Anasema kuwa awali, wakati wakiuza madini hayo kwa wanunuzi binafsi wakiwamo kutoka nje ya nchi, walikuwa wakiuza kilo moja ya bati kati ya Sh. 13,000 hadi 14,000, lakini hivi sasa bei imeshuka na kufikia kati ya Sh. 8,000 hadi 10,000 kwa kilo moja.
“Kuuza madini yetu kwa bei hii kunatuumiza. Hakuna tena ushindani kwa wanunuzi kama tulivyozoea na matokeo yake tunauza kwa bei ya chini wanayoitaka wao (Stamico). Naomba sera ya soko huria izingatiwe pia huku kwetu maana kazi tunayoifanya ni ngumu sana na wajue kwamba sisi hatuna vitendea kazi vya kisasa... tunatumia nguvu nyingi na tena katika mazingira hatari kwa uhai,” anasema Fredy.
Mchimbaji mwingine ni Clavery Marwa. Anasema kuwa kuuza kilo moja ya bati kwa Sh. 10,000 ni kuwapunja kulingana na ugumu wa kazi na kwamba, afadhali bei ya sasa ingefanywa kuwa Sh. 18,000 kwa kilo moja ya bati.
Marwa ambaye amekuwa akifanya kazi hiyo kwa miaka minne sasa, anasema kutokana na bei ya madini hayo kuwa ndogo, bado hajanufaika vya kutosha na kazi hiyo na kwamba, anachokipata ni fedha ya kula tu na matumizi mengine madogo ya familia yake.
“Naitegemea sana kazi hii maana sina kazi nyingine ninayoweza kufanya. Elimu yangu ni ya msingi … nina familia ya mke na mtoto mmoja, wote wananitegemea kutokana na matarajio ya kufanikiwa siku moja kupitia kazi hii,” anasema.
Anasema, mbali na changamoto hiyo, pia kuna wakati wanaingia machimboni lakini wanakosa madini hayo; au wakati mwingine hupata kilo moja tu baada ya kuhangaika sana kutoka asubuhi mpaka jioni.
Anakiri kwamba kuna baadhi ya siku, hali huwa nzuri kwani hupata kuanzia kilo tano hadi ishirini kwa siku.
“Kuna uwezekano wa kupata madini yenye thamani kati ya Sh. 200,000 hadi Sh. 400,000 kwa siku… hata hivyo, hali hiyo hutokea mara chache tu. Muda mwingi huwa tunaambulia kilo chache tu za madini haya,” anasema Marwa.
Wengine kadhaa waliozungumza na NIPASHE wamesisitiza kuwa kilio chao kikubwa ni bei ya sasa inayotumiwa na Stamico kununua madini ya bati kwao, wakidai kwamba ni ya chini na kutaka ushindani urejeshwe kama ilivyokuwa awali.
Wanasema ili kupata madini hayo, hulazimika kuingia katika mashimo yenye urefu kwenda chini wa zaidi ya mita 100, hali ambayo huwa inahatarisha usalama wa maisha yao kutokana na kutokuwa na vifaa vya kisasa kufanya kazi hiyo, lakini hawana namna nyingine ispokuwa ni kujitoa muhanga kwa nia ya kujitafutia maisha bora.
“Hivi sasa ni roho mkononi. Uchimbaji wa madini yenyewe (bati) ni mgumu na tena unaohitaji ujasiri mkubwa, lakini cha kusikitisha ni kwamba hata unapobahatika kupata, bado sasa hivi unakumbana na hofu nyingine ya kupata bei ya chini ambayo kwakweli haiendani na kazi kubwa tunayofanya. Ni bora waruhusu soko huru lenye ushindani wa bei ili tunufaike,” mchimbaji mwingine anasema.
KIONGOZI WA WACHIMBAJI
Mwenyekiti wa Umoja wa Wachimbaji Wadogo wa Madini ya Bati katika eneo hilo, Erick Ezekia, anasema kuwa wachimbaji walioko eneo hilo wanatoka katika maeneo mbalimbali nchini na kuwa, kwa mujibu wa sensa yao iliyofanyika hivi karibuni, hadi sasa kuna wachimbaji 800.
Ezekia anaiomba serikali kuboresha mazingira ya eneo hilo kwa kuwajengea miundombinu ya barabara ili kurahisisha usafirishaji wa madini hayo maana wakati wa mvua hupata shida kusafirisha bidhaa hiyo kutokana na barabara kutokuwa imara.
Aidha, anaiomba serikali kuwawezesha kupata maji safi na salama ili kuwaepusha na magonjwa ya mlipuko ambayo yanaweza kusababisha kudhoofika kiafya na kushindwa kupata nguvu za kuendelea na shughuli za uchimbaji.
AFYA ENEO LA MGODI
Akizungumzia changamoto ya afya, mwenyekiti huyo anasema wachimbaji walioko katika eneo hilo wanapata huduma za afya katika kituo cha afya kilichoko katika kata hiyo ya Kyerwa, lakini kutokana na ugumu wa mazingira wakati mwingine hutumia kliniki za mkononi (mobile clinic) kwa ajili ya wajawazito na watoto.
“Watoto wenye umri wa chini ya miaka mitano na kina mama wajawazito, angalau serikali imeweka utaratibu wa kutuletea kliniki ya mkononi ambapo watumishi wa afya huwafuata huku na kuwapatia huduma za vipimo… kwa hili tunashukuru,” anasema.
Kashunju Runyogote ni Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Kyerwa ambaye anasema, uchimbaji wa madini ya bati katika eneo hilo ulianza mwaka 1935.
Runyogote anasema kuwa siku za nyuma, walikuwapo wawekezaji katika eneo hilo lakini baada ya kushindwa kuelewana na wachimbaji hao, iliamuriwa waondoke na kazi hiyo ibakie mikononi mwa Stamico; maelezo ambayo hata hivyo yamekuwa yakipingwa na wachimbaji wadogo.
TISHIO LA UKIMWI
Kutokana na idadi ya watu kuongezeka kwa kasi katika eneo hilo, wakitokea maeneo mbalimbali huku tishio la ugonjwa wa ukimwi likiwa juu, mwenyekiti huyo anawaahidi wachimbaji hao kuwa serikali itahakikisha mipira ya kike na kiume (kondom) inapatikana kwa urahisi kwa lengo la kulinda afya zao.
“Sihamasishi mfanye ngono bila utaratibu, ila ninavyofahamu sehemu yenye mkusanyiko mkubwa wa watu kama ninyi, tena walioshiba, lolote linaweza kutokea. Kwa hiyo, ili msiathirike na kushindwa kufanya shughuli zenu, tutahakikisha mnapata huduma hiyo,” anasema.
Anasema sehemu kubwa ya wananchi walioko katika eneo hilo ni vijana, hivyo bado taifa linawategemea kama nguvu kazi ya kuinua uchumi wa jamii na taifa zima kwa ujumla na hivyo siyo rahisi serikali kuwaacha waangamie.
MKUU WA MKOA
Mkuu wa mkoa wa Kagera, John Mongella, ametembelea eneo hilo na kujionea hali halisi, hasa kuhusiana na changamoto wanazokabiliana nazo wachimbaji.
Mongella amesema serikali imesikia kilio chao na kuwa itajitahidi kuweka mazingira yatakayowezesha changamoto zinazowakabili kupungua.
“Serikali inawaangalia wachimbaji wadogo kuliko wakubwa, maana wakubwa tayari wana mitaji na wanaweza kufanya lolote. Sisi jicho letu liko kwenu, hivyo tutahakikisha mnawekewa mazingira bora ili hatimaye muweze kuchimba kisasa na kuachana na uchimbaji wa kizamani,” anasema.
Anasema uchimbaji mdogo kwa kutumia vitendea kazi duni mara nyingi hauna tija na unahatarisha maisha ya wachimbaji. Akawashauri pia kujiunga katika vikundi ili waweze kuwa na fursa za kupata mikopo kutoka katika taasisi za kifedha.
“Nimesikia mna umoja wenu hapa na mmekuwa mkifuatilia taratibu za usajili bila mafanikio. Sasa nawaahidi kuhakikisha unasajiliwa, watumeni viongozi wenu katika ofisi za madini nami niko nanyi. Nitawasaidia ili usajili ukamilike haraka,” anasema.
Anasema endapo umoja wao huo utasajiliwa, itakuwa rahisi kupata mikopo kwa ajili ya kununulia zana za kisasa, ambazo zitawawezesha kuchimba kisasa, ili kupata faida kubwa na kufanya maisha yao kuwa salama.
No comments:
Post a Comment