Saturday 21 February 2015

KIONGOZI WA VIJANA JKT ATEKWA AOKOTWA

Utata umezingira suala la kijana George Mgoba, ambaye amekuwa akijitambulisha kuwa kiongozi wa wahitimu wa mafunzo ya Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) baada ya habari kuwa alitekwa na baadaye kutupwa kwenye Msitu wa Pugu, nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam.

Si Jeshi la Polisi mkoani Pwani wala Dar es Salaam lililokuwa tayari kuzungumzia tukio la kijana huyo kutekwa, kupigwa na kutekelezwa kwenye msitu huo, lakini msemaji wa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MHN) alithibitisha kuwapo kwa kijana huyo hospitalini hapo kuanzia jana saa 10:30 jioni, ingawa hakutaka kutoa maelezo mengi.
Mgoba amekuwa akihamasisha vijana wenzake waliohitimu ya JKT kukusanyika jijini Dar es Salaam na kuandamana hadi kwa Rais ili kumweleza masikitiko yao ya kutopatiwa ajira baada ya kumaliza mafunzo kama walivyoahidiwa wakati wakienda kwenye kambi za jeshi hilo.
“Ndio aliletwa hapa majira ya saa 10:30 akitokea Hospitali ya Amana,” alisema ofisa uhusiano wa MHN, Aminiel Aligaeshi.
“Lakini waganga walipotaka kumtibu alikataa kwa sharti kwamba atibiwe wakati ndugu zake wakiwapo. Ndugu zake walipofuatwa nje, hawakuonekana. Anaonekana ana maumivu sehemu ya mgongoni na anapumua kwa shida.”
Habari zinasema kuwa kuanzia saa 1:00 jioni madaktari walikuwa wakijaribu kumshauri akubali kutibiwa, lakini akakataa na hivyo kuwalazimu madaktari kumtaka asaini fomu ya kukataa matibabu. Hata hivyo hadi saa 2:00 usiku hakuwa amesaini.
Kijana huyo anasemekana kutekwa juzi jioni na watu ambao hawajajulikana na aliokotwa na msamaria mwema ambaye baadaye aliungana na watu wengine kumpeleka Hospitali ya Tumbi.
Hata hivyo, aligoma kutibiwa kwenye hospitali hiyo akitaka ndugu zake wawepo.
Habari zinasema baadaye alisafirishwa kuhamishiwa Hospitali ya Amana kabla ya kuhamishwa tena na kwenda Muhimbili jana saa 9:00 alasiri.
Mfanyakazi mmoja wa Hospitali ya Amana aliiambia gazeti hili kuwa kabla ya askari wa Jeshi la Polisi kumfuata na gari mbili aina ya Land Rover, kundi la vijana wanaosadikiwa kuwa ni wahitimu wa mafunzo ya JKT, liliwasili Amana na kutaka kushinikiza kumchukua Mgoba, lakini uongozi uliwakatalia kwa maelezo kuwa wangetoa ruhusa hiyo kama wangekuwapo ndugu zake.
Alivyotekwa
Mwandishi wetu kutoka Kibaha anaripoti kuwa kijana huyo, anayejielezea kuwa ni mtetezi wa vijana waliohitimu JKT, aliokotwa kwenye kichaka kilichopo Picha ya Ndege mjini humo akiwa amejeruhiwa maeneo mbalimbali ya mwilini.
Kwa mujibu wa mwandishi wetu, kijana huyo aliokotwa asubuhi ya Februari 19 na msamaria mwema ambaye hakutaka jina lake akiwa kwenye kichaka hicho kilicho jirani na baa ya River Road na Shule ya Sekondari ya Tumbi.
Alisema wakati msamaria huyo akipita karibu na kichaka hicho alisikia sauti ya mtu akigugumia na ndipo alipoenda kichakani na kumkuta Mgoba akiwa amefungwa kamba miguuni huku akionekana kuwa na maumivu makali.
Msamaria huyo alisema alipomhoji kilichompata, kijana huyo alimwambia anahisi amepigwa na mhusika wa ajira za JKT kwa sababu alipigiwa simu na mtu anayemfahamu kuwa akafuate majibu ya maombi yake na akiwa njiani alipishana na watu wawili na ghafla alihisi kulewa na baadaye kupoteza fahamu hadi mtu huyo alipomzindua.
“Wakati nashangaa, watu wengine waliokuwa wakipita hapo na baadhi ya waliokuwa wakipata huduma mbalimbali kwenye baa hiyo, nao walisogea jirani tulikokuwa na tukakubaliana tutoe taarifa polisi na askari kweli walifika na gari na kumchukua hadi kituoni cha Polisi cha Tumbi,” alisema msamaria huyo.
Alieleza kuwa baadaye walichukua maelezo ya kijana kisha akapelekwa hospitali ya Tumbi kwa matibabu.
Wakati tukio hilo likiendelea, ndipo taarifa zikaanza kusambaa katika maeneo kadhaa ya mji wa Kibaha zikieleza kuwa kiongozi wa vijana waliohitimu JKT nchini, amelazwa Tumbi baada ya kupigwa.
Taarifa hizo zilisababisha vijana kadhaa wanaodaiwa kuhitimu JKT, ikiwamo kambi ya Ruvu kufika hospitalini hapo kwa lengo la kumjulia hali mwenzao.
Taarifa zilizopatikana ndani ya hospitali hiyo zimeeleza kuwa kazi ya kutoa huduma ya kwanza kwa Mgoba ilikuwa ngumu kwa madaktari kutokana na kwanza majeruhi mwenye kuwa anachunguza kila kitu alichokuwa anafanyiwa, na pili kusisitiza kuwa hayupo tayari kuchomwa sindano wakati huo hadi hapo watakapofika ndugu zake.
“Ni kweli kama unavyosema huyu kijana kweli hata mimi nilikuwa nashangaa alivyokuwa msumbufu, maana ukichukua tu bomba la sindano anahoji hiyo sindano ya nini, nikamwambia tulia tunakutibu. Nilishangaa alinisihi nisimchome sindano, bali nifanye usafi wa majeraha,” alisema daktari mmoja ambaye pia hakutaka jina lake litajwe.
Aliendelea kusema kuwa kama tiba ni muhimu kwa wakati huo, basi aruhusiwe aende nyumbani akatibiwe huko na kwamba hadi wakati huo hakujua kuwa majeruhi huyo ni Mgoba.
Taarifa za uhakika zinabainisha kuwa majeruhi huyo alifikia wodi ya wagonjwa wa dharura na alifanyiwa vipimo mbalimbali, ambavyo vilionyesha kuwa hakuwa madhara makubwa ndani ya kichwa.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Pwani, Ulrich Matei alisema hawezi kuzungumzia suala hilo na akamtaka mwandishi kuwasiliana na msemaji wa polisi wa Mkoa wa Kinondoni.
“Nakuambia mimi sijui kama huyu ni mwenyekiti wa vijana waliohitimu wa JKT, bali ninachoweza kukuambia ni kwamba kweli kijana huyo aliokotwa katika kichaka Picha ya Ndege na kama ilivyo ada tulimpeleka Tumbi akapate tiba kwanza kama ilivyo kwa majeruhi wengine, kwa hiyo suala ya yeye kusema yupo kwa ajili ya kuwatetea vijana wenzake waliopita mafunzo JKT ni jambo jingine. Amekuambia wewe mimi sijui… kama wewe unajua basi ni wewe,” alisema Matei.
Mbali ya baadhi ya vijana kutinga Tumbi wakati alipofikishwa hapo, pia taarifa hizo zilisababisha shughuli za biashara katika baadhi ya maeneo kusimama kwa dakika kadhaa ambapo watu walikuwa wakijikusanyika kuulizia ukweli wa suala hilo.
Mganga Mkuu wa Hospitali ya Amana, Meshack Shimweta hakutaka kuzungumzia suala hilo kwa maelezo kuwa alikuwa nje ya ofisi.
Tukio la utekaji lilimtokea mwenyekiti wa Jumuiya ya Madaktari, Dk Steven Ulimboka mwaka 2012 wakati akiongoza mgomo wa matabibu hao kudai maboresho ya maslahi yao.
Ulimboka alichukuliwa na mtu mmoja kwenye klabu ya Viongozi Kinondoni na baadaye kupigwa na kutupwa kwenye msitu wa Mabwepande ambako aliokotwa na msamaria mwema.
Katika hatua nyingine, Serikali imesema haikuwahi kuahidi kwamba kila anayepita Jeshi la Kujenga Taifa(JKT) lazima apate ajira.
Mkurugenzi wa Idara ya Habari Maelezo, Assah Mwambene alisema vijana hao walidai ajira Ikulu kwa kisingizio kwamba Katibu Mkuu Kiongozi Ombeni Sefue aliahidi kupatiwa ajira alipokutana nao.
Mwambene alisema siyo nia ya Serikali kupeleka vijana JKT kwa lengo la kupata ajira ila kuwajenga kimaadili na uzalendo kwa nchi yao ili wawe raia wema.
MWANANCHI

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!