Friday, 6 February 2015

OSHA VIZURI VYAKULA KABLA YA KUVIPIKA

Mara nyingi vyakula vibichi kutoka shambani au mahali vilipohifadhiwa huwa vina uchafu, kemikali, vijidudu vinavyosababisha maradhi au vitu vingine visivyoliwa.

Kwa hiyo, kuosha vyakula kabla ya kuvipika au kuvisindika ni muhimu sana kwa afya za walaji.
Kwa sababu kuosha vyakula ni kuondoa uchafu na vitu vingine ambavyo siyo vyakula au sehemu ya kile unachokiandaa kwa ajili ya kuliwa.
Hiyo inasaidia kuondoa vitu ambavyo vinavyoweza kudhuru afya ya mlaji au vinaathiri mwonekano mzuri wa chakula.
Kuosha vyakula ni kudhibiti kuzaliana kwa wingi vijidudu vinavyoozesha vyakula na kusababisha maradhi kwa walaji.
Ubora na usalama wa chakula kilichopikwa au kusindikwa kiwandani unategemea sana chakula hicho kilivyo oshwa.
Kwa mfano, chakula kisichooshwa vizuri kinaweza kuwa na kiwango kikubwa cha vijidudu vinavyosababisha maradhi.
Vijidudu vingine huwa havifi kirahisi kama chakula hakitapikwa kwa joto kubwa na kwa muda mrefu. Mara nyingi vyakula kama mboga hupikwa kwa muda mrefu ili viliwe vikiwa na virutubisho muhimu ambavyo hupotea baada ya kupikwa sana.
Kuna aina kuu nne za uchafu unaoweza kuingia katika vyakula vikiwa shambani wakati wa kuvuna, kusafirisha au kuvihifadhi.
Aina ya kwanza ya uchafu ni ule unaotokana na udongo, mchanga, mawe, vipande vya chuma, plastiki, grisi na mafuta.
Kwa mfano, katika Jiji la Dar es Salaam, dagaa wa Mwanza hawapendwi sana ukilinganisha na wale wa Kigoma licha ya bei yake kuwa ndogo. Moja ya sababu ni kuwa wale wa Mwanza wana michanga mingi.
Hii inaonyesha wazi kuwa wafanyabiashara wa Mwanza hawako makini katika kutunza na kuandaa vizuri dagaa.
Ndiyo kusema wasimamizi wa biashara hii hawako makini. Inawezekana kabisa biashara hii inadumazwa na kasumba ya uzembe huu.
Aina ya pili ya uchafu unaoingia katika vyakula ni ule unaotokana na mabaki ya mimea kama vile pumba, mchele usiokobolewa (chuya), kamba, mizizi, majani, magome na vipande vya miti.
Mchele wa Mbeya unapendwa sana na una bei kubwa katika Jiji la Dar es Salaam. Mara nyingi mchele huo hauna chuya wala mawe kama ilivyo mingine.
Aina ya tatu ni uchafu unaotokana na mabaki ya wanyama kama vile vinyesi, mayai ya wadudu, manyoya, mabawa, kiwiliwili au vichwa vya wadudu.
Aina ya nne ni kemikali zilizoingia katika vyakula wakati wa kupulizia dawa, kuweka mbolea shambani au wakati wa kuhifadhi chakula.
Mbogamboga na matunda kama vile nyanya, kabichi, spinachi, mchicha, matango na matikiti yanawekwa dawa ili kudhibiti magonjwa.
Wakulima wanakumbushwa kuzingatia siku wanazotakiwa kujizuia kuvuna mazao yao kama wametia dawa mazao hayo.
Mahindi hasa ya mbegu za kisasa yanaharibika haraka kutokana na kuwa na wadudu. Kwa hiyo, yanawekwa dawa wakati yakihifadhiwa katika ghala au hata yakiwa sokoni.
Watu waoshe vizuri mahindi kabla ya kuyatumia au kuyasaga kwa ajili ya kupata unga ulio bora. Wale wanaotumia dawa wanahimizwa kufuata maelekezo ya wataalamu ili dawa hizo zisilete madhara kwa walaji.
Aina ya tano ya uchafu unaoingia katika vyakula ni vijidudu vinavyoozesha vyakula na kusababisha magonjwa kwa walaji.

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!