Friday, 6 February 2015

NJIA BORA YA KUKABILIANA NA SARATANI NI KUIBAINI NA KUITIBU MAPEMA



Saratani ni moja ya magonjwa yanayoisumbua sana fani ya tiba kutokana na kuwa na mikanganyiko mingi katika kuitibu.
Saratani ni ugonjwa unaotokea baada ya kuwapo mparajikano wa taarifa kwenye chembe za urithi ambazo hudhibiti mwenendo wa kuzaliana kwa seli katika organi fulani ili kuendelea kuifanya itende kazi kwa usahihi.

Wataalamu wa afya wanasema mparajikano huo husababisha seli zisizo za kawaida kuzaliana na kuongezeka idadi pasipo kudhibitiwa, hivyo kuifanya organi au viungo viwe na umbo tofauti na ilivyo kawaida.
Hali hiyo ya kuzaliana bila utaratibu inaweza kusababisha athari kuvamia sehemu nyingine za mwili na kuleta madhara. Saratani huweza kusambaa maeneo mengine ya mwili.
Saratani nchini
Taasisi ya Saratani ya Ocean Roard (ORCI), inasema kuwa idadi ya wagonjwa wapya wa saratani wanaofika kutibiwa inaongezeka kwa kasi toka wagonjwa 2,807 mwaka 2006 hadi kufikia 5,529 mwaka 2013.
Dk Julius Mwaiselage wa ORCI anasema ongezeko kubwa la maradhi haya hapa nchini linatokana na mfumo wa maisha ya Watanzania kwa sasa.
Kauli ya Dk Mwaisega inaungwa mkono na ripoti ya utafiti uliofanywa na Shirika la Afya Duniani (WHO) mwaka 2010, ilibainika kuwa miongoni mwa sababu za ongezeko la saratani hapa nchini ni pamoja na mtindo wa maisha usiofaa.
Miongoni ni matumizi ya kemikali zisizofaa kwenye vipodozi, matumizi ya dawa zisizothibitishwa, matumizi ya tumbaku na vyakula vilivyoathiriwa.
Utafiti huo ulibaini kuwa asilimia 20 ya saratani za koo na mdomo zinasababishwa na mtindo wa kufanya mapenzi kwa njia ya mdomo.
Mkurugenzi wa Taasisi ya Utafiti wa Saratani ya Shirika la Afya Duniani (IARC), Dk Christopher Wild anasema:
“Kuongezeka kwa tatizo la ugonjwa wa saratani, ni kikwazo kikubwa kwa ustawi na maendeleo ya binadamu.”
“Hatuwezi kudharau tatizo la saratani, jitihada za makusudi kuzuia saratani na kuigundua mapema zinahitajika ili kuboresha huduma za matibabu na kushughulikia ongezeko kubwa la ugonjwa huo duniani,” anasema Dk Wild.
Kinachosababisha saratani
Zipo zaidi ya aina 100 za saratani na zinapewa jina kutokana na mahali iliposhambulia mwilini na aina ya chembe zilizoathirika.
Utafiti wa Dk Catherine de Martel na wenzake uliochapishwa mwaka 2012 katika Jarida la The Lancet Oncology, unaonyesha kuwa katika nchi zilizoko Kusini mwa Jangwa la Sahara, asilimia 32.7 ya saratani zote hutokana na maambukizi ya vimelea vya magonjwa.
Miongoni mwa vimelea vya magonjwa hayo ni kama vile Virusi Vya Ukimwi (VVU) na homa ya ini vinasababisha asilimia 90 ya saratani ya mlango wa kizazi na virusi vya Epstein Barr vinavyosababisha saratani ya uvumbe wa taya kwa watoto.
Vimelea vingine ni Helicobacter pylori wanaosababisha vidonda vya tumbo na wadudu wa kichocho wanaosababisha saratani ya kibofu cha mkojo.
Kwa wanaume saratani zinazoongoza ni saratani ya mapafu, saratani ya Kaposi’s sarcoma, tezi dume na ile ya tumbo la chakula. Kwa wanawake, utafiti huo unaonyesha saratani zinazoongoza ni za mlango wa kizazi ikifuatiwa na ya matiti na ya utumbo.
Zipo sabuni na dawa za meno zenye kiambato cha Triclosan, ambazo zinauzwa nchini. Hizi nazo zinatajwa kuwa miongoni mwa vitu vinavyochochea saratani.
Kwa mujibu wa utafiti uliofanywa na Mei-Fei Yueh na wenzake na kuchapishwa katika Jarida la Sayansi la PNAS, mwaka 2014, kemikali ya triclosan inaweza kusababisha saratani kwa binadamu kupitia njia ile ile inayosababisha saratani kwa wanyama.
Msemaji wa Mamlaka ya Chakula na Dawa nchini (TFDA), Gaudensia Simwanza anakiri taasisi yake kupata taarifa za kuwepo kwa aina ya dawa ya meno yenye kemikali ya triclosan katika soko la Tanzania.
Simwanza anasema kuwa dawa hiyo yenye triclosan iliyoidhinishwa kutumika hapa nchini ina asilimia 0.3 tu ya kemikali hiyo hatari ambacho wataalamu wanaona hakina madhara kwa watumiaji wenye umri wa miaka zaidi ya 12.
Hata hivyo, Profesa Thomas Zoeller wa Chuo Kikuu cha Massachusetts Amherst anaelezea madhara ya kemikali ya triclosan
Anaonya: “Napenda wazo linalosema kuwa bidhaa zenye kemikali hii hazina madhara, lakini tulipozifanyia utafiti kwa wanyama, matokeo yanaonyesha mambo tofauti. Nafikiri tunajihatarishia maisha kwa kiwango kikubwa kwa kukubali kiwepesi kemikali hatari.”
Athari za saratani
Ingawa ugonjwa wa saratani ni tatizo la afya ya jamii ulimwenguni pote, mzigo mkubwa wa tatizo hili sasa unaanza kuzilemea nchi zinazoendelea.
Kwa mujibu wa ripoti ya Shirika la Afya Duniani (WHO) ya hivi karibuni, zaidi ya asilimia 60 ya wagonjwa wapya wa saratani duniani kote, yanatokea katika nchi za Afrika, Asia na Amerika ya Kati na Kusini. Pia, asilimia 70 ya vifo vyote vitokanavyo na saratani duniani kote hutokea katika nchi hizo.
Kwa mujibu wa ripoti kuhusu hali ya saratani duniani ya mwaka huu iliyotolewa na IARC, inakadiriwa kuwa ifikapo mwaka 2030 duniani kote kutakuwa na wagonjwa wapya wa saratani kiasi cha milioni 22 kwa mwaka na kati ya hao asilimia 60 hadi 70 watakuwa katika nchi zinazoendelea.
Saratani umeonekana ni moja ya magoinjwa yanayoongoza kwa kusababishia watu ulemavu wa viungo na kushindwa kutekeleza majukumu ya kuongeza kipato katika familia.
Mbali na kupoteza nguvu kazi ya jamii na kuacha mzigo mkubwa wa watoto yatima, matibabu ya saratani pia hupoteza fedha na rasilimali nyingi za familia na taifa.
Msemaji wa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii Tanzania, Nsachris Mwamaja akielezea kuhusiana na gharama kubwa za matibabu ya saratani anasema:
“Pale kwenye Taasisi ya Saratani ya Ocean Road (ORCI), wagonjwa wanatibiwa bure ni wengi na tiba yao inagharimu fedha nyingi. Kwa mfano mgonjwa mmoja wa saratani huweza kutibiwa kwa Sh2 milioni. Ndiyo maana kuna changamoto kubwa katika swala hili.”
Kutokana na maelezo ya wataalamu ni vigumu kwa mtu kusema anaweza kuepuka ama kuchukua tahadhari ya asilimia 100 ili asipate saratani.
Hii inatokana na ukweli zipo za kurithi, miale ya jua na zinazosababishwa na mazingira, dawa au ugonjwa mwingine alioupata binadamu.
Kinachopendekezwa na Taasisi ya Saratani ya Ocean Road, ni kila mtu kuchukua tahadhari za kufanya mara kwa mara uchunguzi wa mwili mzima ili kujua kama kuna dalili za kuanza kwa saratani.
Maelekezo ya taasisi hiyo yanahimiza mtu ajichunguze angalau kila mwaka. Tahadhari ya taasisi hiyo ni kwamba saratani ikigundulika mapema ni rahisi kuitibu na hata kuidhibiti isiendelee.
Wengi wa wagonjwa wanaofikishwa kwenye taasisi hiyo, inaelezwa ni wale ambao tayari wako katika hali mbaya kutokana na saratani kukomaa na matibabu yake yanakuwa magumu na yanayotumia muda mrefu.

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!