Friday, 20 February 2015

MWAKILISHI AFARIKI GHAFLA ZANZIBAR

Mnadhimu wa Baraza la Wawakilishi na Mwakilishi wa Jimbo la Magomeni (CCM), Salmin Awadh Salmin (57) amefariki dunia.

Salim ambaye alikuwa Mjumbe wa Bunge Maalumu la Katiba na mtetezi wa hoja ya serikali mbili, amefariki dunia huku akiwa na nia ya kuwasilisha hoja binafsi akitaka Kura ya Maoni kwa Wazanzibari kuhusu kuendelea ama kutoendelea kwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK).
Mwakilishi huyo (pichani) ambaye alikuwa mwanasiasa machachali, alikutwa na umauti  baada ya kuugua ghafla, akiwa kwenye kikao cha CCM katika ofisi kuu za chama hicho, Kisiwandui Zanzibar.
Naibu Katibu wa CCM Zanzibar, Vuai Ali Vuai alithibitisha kutokea kwa tukio hilo na taratibu za kuhifadhi mwili zilikuwa zimeanza kufanyika nyumbani kwake Magomeni, Mkoa wa Mjini Magharibi, Unguja.
Katibu wa Baraza la Wawakilishi, Yahya Khamis Hamad alisema alipokea taarifa za kifo saa nane mchana na tayari taratibu za maziko zilianza kufanyika.
Alisema Baraza lingetoa taarifa rasmi na taratibu za maziko baada ya wanafamilia na wajumbe wa Baraza kukamilisha mipango ya mazishi na kuutoa mwili wa marehemu hospitali.
Hata hivyo, alisema kwa mujibu wa sheria, hakutakuwapo na uchaguzi mdogo kuziba nafasi hiyo kutokana na kubaki kwa muda mfupi chini ya miezi 12.
Salmin amefariki dunia akiwa na msimamo wa kuwasilisha hoja binafsi katika Baraza la Wawakilishi kuitaka SMZ iitishe Kura ya Maoni kuwauliza Wazanzibari iwapo wanataka kuendelea na mfumo wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK) au wanataka kurejea kwa mfumo wa awali wa chama kinachopata ushindi ndicho kinachoongoza Serikali.
Akizungumza na Mwananchi wiki iliyopita, Salmin alisema malengo ya kuundwa kwa SUK bado hayajatimia kama ilivyokuwa imekusudiwa kwa kuwa baadhi ya viongozi wanaounda serikali wanafanya kazi ya kuwinda ili kuiangusha CCM badala ya kuitumikia Serikali kwa mujibu wa sheria na taratibu.
Salmin aliyekuwa mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM, aliwaongoza wajumbe wa Bunge la Katiba kutoka Zanzibar kupinga waraka uliowasilishwa na Kamati ya Uongozi ya Baraza hilo ukitetea mfumo wa Serikali tatu na kuibua mjadala mkali.
Alidai waraka huo uliandaliwa nje ya utaratibu kwa vile hakukuwa na msimamo wa pamoja wa Baraza wala Serikali katika suala la mabadiliko ya Katiba.
Salim aliyezaliwa Juni 26, 1958 aliwahi kuwa askari wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania kuanzia mwaka 1976 hadi mwaka 1986, na aliondoka jeshini akiwa na cheo cha sajenti.
Baadaye aliajiriwa kwenye hoteli ya Narrow Street na kushika wadhifa wa meneja kuanzia mwaka 2000 hadi mwaka 2005, alipoamua kwenda kugombea uwakilishi wa Jimbo la Magomeni.

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!