Katika siku za karibuni, kumekuwapo na malalamiko ya ubovu wa mara kwa mara wa kivuko cha MV Magogoni kinachotoa huduma zake kati ya Kivukoni na Kigamboni jijini Dar es Salaam.
Malalamiko haya yamekuwa yakitolewa na wananchi watumiaji wa kivuko hicho ambacho ni tegemeo kubwa kwao kutokana na kutokuwa na mbadala mwingine.
Watumiaji wa kivuko hicho kinachomilikiwa na Serikali, wamekuwa wakidai kwamba kimekuwa kikiharibika mara kwa mara ikiwamo kuzima injini kikiwa majini na abiria pamoja na mizigo lukuki hususan magari.
Hali hiyo imekuwa ikisababisha hofu kubwa kwa watumiaji wa kivuko hicho ambao ni wananchi wa kawaida, wafanyakazi wa serikali, kampuni na mashirika mbalimbali, wakulima wanaosafirisha mazao yao kutoka upande wa Kigamboni kuja katikati ya Jiji la Dar es Salaam na wanafunzi wa Chuo cha Usimamizi wa Fedha (IFM) ambao wengi wao wamepanga Kigamboni pamoja na Chuo cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere.
Inavyoonekana ni kama serikali imeziba masikio kusikiliza kilio cha wananchi hao kuitaka ikifanyie marekebisho haraka kivuko hicho ili kuokoa maafa yanaoweza kutokea wakati wowote kutokana na ubovu wake.
Wahenga walisema `Tahadhari kabla ya hatari”, na pia “Usipoziba ufa, utajenga ukuta.'
Usemi huu wa wahenga wetu, una maana kubwa sana, hasa kuhusiana na namna ya busara zaidi katika kujiepusha na majanga yanayoepukika. Na sisi tuna kila sababu ya kuzingatia nasaha hizo za wahenga kupitia semi zao, nahau, methali, mafumbo na hata vitendawili.
Kwa bahati mbaya sana, sisi tunaona kuwa sasa imekuwa ni kama mazoea kwa mambo mengi yakiwamo yanayotishia usalama kutopewa uzito mapema. Mara tu yanapotokea maafa, ndipo hapo wakuu wa mamlaka mbalimbali, pamoja na watendaji wao huanza kuhaha huku na huko katika kutafuta visingizio vya kujitetea juu ya kutowajibika kwao kwa wakati.
Kwa ufupi, mamlaka zinazohusika hukurupuka na kutangaza hatua zisizofuata taratibu za kisayansi katika kushughulikia undani wa majanga husika. Mara nyingi, hatua za namna hii ambazo huwa ni kama za zimamoto, huishia kwa kuundwa kamati teule za kuchunguza majanga husika na zaidi huwa na lengo moja kubwa, ambalo ni la kupunguza machungu ya umma dhidi yao. Huwa hakuna kubwa linalofanywa. Hatua zaidi huchukuliwa baadaye sana, tena pengine baada ya kutokea janga jingine linaloweza kuepukika kungali mapema.
Mathalani, ajali ya kuzama kwa meli ya MV Bukoba, iliyotokea Mei 21, 1996 na kuua mamia ya ndugu zetu, kama chombo hicho kingekuwa kinafuatiliwa kwa karibu kabla ya tukio hilo, pengine lisingetokea janga kubwa kama hilo. Ilielezwa kuwa chombo hicho kilianza kuonyesha hitilafu siku kadhaa kabla ya kutokea kwa ajali hiyo, lakini kama ilivyozoeleka, mamlaka husika hazikufanya haraka kuchukua hatua za kukifanyia marekebisho.
Tusingependa kuwakumbusha machungu ndugu zetu ambao waliwapoteza wapendwa wao katika ajali hiyo mbaya kutokea katika historia ya nchi hii.
Tunachotaka kuikumbusha mamlaka inayohusika na usimamizi wa kivuko cha MV Magogoni, ni vema ikachukua tahadhari mapema kuyafanyia kazi malalamiko ya wananchi ili yasije yakatukuta kama yale yaliyotokea kwa MV Bukoba.
Sisi tunaamini kwamba mamlaka zinazohusika si kwamba hazijui lolote kuhusu kasoro za kivuko hicho, ila ni kutokana na ule utamaduni wetu tulionao wa kusubiri maafa yatokee, ndipo uwajibikaji uanze kuchukua nafasi yake.
Ikumbukwe kwamba kivuko cha MV Magogoni kwa kusaidiana na kivuko kingine cha MV Kigamboni, kina umuhimu wa kipekee katika utoaji huduma kwa wakazi wa Kigamboni.
Hata hivyo, tunafahamu juhudi za serikali zinazofanywa sasa za kujenga daraja la Kigamboni ambalo kwa hakika litakuwa mkombozi kwa wakazi wa eneo hilo na hivyo kuachana na matumizi ya vivuko ambavyo kwa sasa vinaonekana usalama wake kutia shaka.
Wakati huu tukisubiri kukamilika kwa ujenzi wa daraja hilo la Kigamboni, basi upo umuhimu wa kuhakikisha kwamba vivuko vilivyopo sasa, vinabororeshwa mara kwa mara ili kuwaondoa hofu watumiaji wake.
CHANZO: NIPASHE
No comments:
Post a Comment