Mkoa wa Kigoma umekuwa kivutio kikubwa kwa wawekezaji wa ndani na nje ya nchi.
Hiyo imetokana na mikakati madhubuti iliyoibuliwa na viongozi wa mkoa kuanzia 2007, kwa lengo la kuufanya uwe kitovu cha biashara katika ukanda wa nchi za Maziwa Makuu.
Ikizingatiwa kuwa kuna tatizo la miundombinu ya usafiri, Serikali ilianza ujenzi wa miradi mikubwa ya maendeleo hasa barabara, madaraja na kiwanja ili kuwezesha ndege kubwa za abiria na mizigo kutua Kigoma bila matatizo.
Hivyo, ili kuutangaza mkoa kimataifa, aliyekuwa mkuu wa mkoa, Kanali mstaafu Joseph Simbakalia alianzisha utaratibu maalumu wa kuifanya Kigoma kuwa ukanda maalumu wa kiuchumi (KISEZ). Pia, mkoa ulibatizwa jina la ‘Dubai ndogo’ kwa vile ulitarajiwa kuwa na bidhaa zote zinazofuatwa Dubai na wafanyabiashara wa Tanzania.
Dosari zaanza
Awali, mradi huo ulioonekana ungekuwa ni sawa na ukombozi wa kiuchumi kwa wakazi wa Kigoma na eneo zima la Maziwa Makuu, lakini ulianza ‘kumegwa’ na kupanuliwa hadi katika mikoa ya Rukwa na Katavi kwa kile kilichosemwa kuwa hali za kijiografia ya mikoa hiyo inafanana na Kigoma.
Inawezekana ni kweli, japokuwa baadhi ya watu walihusisha upanuzi huo wa eneo la KISEZ na ushawishi wa Waziri Mkuu Mizengo Pinda ambaye pia ni mmojawapo wa viongozi wanaohimiza maaendeleo ya mikoa ya ukanda huu wa magharibi yenye utajiri mwingi wa rasilimali. Kadiri miaka inavyosonga mbele ndivyo jitihada za kuendeleza KISEZ kwa ajili ya kuinua uchumi wa Kigoma na maeneo mengine, zilivyoonekana kufifia kwani hata ile kasi ya wawekezaji waliokuwa wanakuja Kigoma na kupewa mamia ya ekari za ardhi kwa ajili ya kuwekeza kwenye kilimo, imepungua.
Mkakati wa kibiashara pia unakwamishwa na hali ya usafiri wa barabara kwani siyo nzuri. Hivyo ujenzi wa Barabara ya Mwandiga hadi Manyovu yenye urefu wa kilomita 60 kwa kiwango cha lami ilijengwa sambamba na barabara ya Kigoma hadi Kidahwe yenye kilomita 32.
Barabara ya Kidahwe hadi Uvinza ya kilomita 76 ilijengwa pamoja na daraja la Mto Malagarasi lenye bonde kubwa linalofikia urefu wa kilomita mbili na ambalo lilikuwa kikwazo kikubwa cha usafiri kati ya mikoa ya Kigoma na Tabora, limejengwa. Pia barabara ya lami ya kilomita 48 kwa ajili ya kuimarisha daraja hilo, imejengwa.
KISEZ ilikusudiwa kuwa eneo litakalojengwa maduka makubwa ya kuuza bidhaa za aina mbalimbali kama vile magari, samani za nyumbani na ofisini, zana za uvuvi, kilimo, mavazi, vipodozi, vito vya madini na nyingine nyingi.
Pia, vingejengwa viwanda vikubwa na vya kati kwa ajili ya kusindika mazao ya chakula na biashara pamoja na kutengeneza malighafi za aina tofauti.
Mkakati huo ulikusudiwa kufanikishwa kwa kujengwa majengo maalumu katika eneo la Buhanda, Businde, Kagera na Ujiji ambalo ndiyo hasa lilikusudiwa kujengwa miundombinu hiyo kwa ajili ya kukuza biashara kati ya Kigoma na eneo zima la nchi za Maziwa Makuu ambazo ni DR Kongo, Burundi, Zambia, Burundi, Rwanda na Uganda zilizolengwa kununua na kuuza bidhaa katika soko la Kigoma au Dubai ndogo. Moja ya changamoto iliyoanza kujitokeza ni baadhi ya wawekezaji kuchukua ardhi, lakini wanachukua muda mrefu kuiendeleza.
Katibu tawala msaidizi wa mkoa anayehusika na huduma za uchumi, Georges Busungu aliwahi kukemea tabia ya baadhi ya wawekezaji wanaojitwalia ardhi bila kuiendeleza.
“Inawezekana baadhi ya watu wanaamini kwamba kuna wawekezaji wanaofanya kazi ya udalali kwa kuja kwetu kuomba ardhi na wakishapewa wanaitelekeza bila kuiendeleza, lakini Serikali ipo makini itamchukulia hatua mwekezaji yeyote atakayeshindwa kutimiza masharti ya mkataba aliopewa wa kuendeleza ardhi,’’ alisema.
Wawekezaji na ardhi
Wapo wawekezaji waliokuja na kupewa ardhi ya kuwekeza kwenye kilimo cha miwa, ujenzi wa kiwanda cha saruji na kilimo cha michikichi, lakini hadi sasa ikiwa ni zaidi ya miaka mitano hakuna yeyote aliyeanza kazi.
Kigoma ambayo ni maarufu kwa kilimo cha michikichi, imeendelea kudumaa huku wakulima wengi wakiamua kukipa mgongo kilimo hicho.
Ikumbukwe kwamba Malaysia iliyokuwa maskini kama Tanzania katika miaka ya 70, imefanikiwa kupaa kiuchumi kutokana na kulima zao la michikichi na mbegu zake zikitoka Kigoma.
Katibu wa Chama cha Wafanyabiashara wenye Viwanda na Kilimo (TCCIA) mkoani hapa, Hamisi Nkuluzi anasema uchumi wa Kigoma bado haujaimarika kutokana na wafanyabiashara wazawa kuwa na mitaji midogo hivyo inawawia vigumu kukua. Anasema changamoto kubwa ni pamoja na upatikanaji wa mikopo na riba kubwa zinazotolewa na taasisi za kifedha, kodi na ushuru mkubwa wa bidhaa pamoja na ukosefu wa elimu ya kutosha kuhusu kufanya biashara kwa mafanikio. “Ipo haja ya kuwaelimisha wafanyabiashara ili waweze kuendesha biashara zao kwa ufanisi, walipe kodi kwa uwiano sawa na biashara wanazofanya. Pia, tupewe unafuu na fursa ya kufanya biashara kubwa kadiri inavyowezekana badala ya kuonekana kwamba wazawa hawana uwezo wa kuwekeza kwenye biashara kubwa,’’ anaeleza.
No comments:
Post a Comment