MKUU wa wilaya Temeke, DC Sophia Mjema, ameipongeza shule ya Sekondari ya Kiislamu inayojulikana kama Twayyaibat Islamic Seminary Secondary School kwa kufanya ada nafuu inayoweza kuwafanya wazazi na walezi wamudu gharama za kusomesha watoto kwenye shule binafsi.
DC Mjema aliyasema hayo alipofanya ziara katika shule hiyo na kukuta uongozi wa Twayyaibat, ukitoa ada ya Sh 200,000 tu kwa mwaka, jambo ambalo ni agharabu mno hususan kwa shule za kulipia na zinazomilikiwa na taasisi za kidini.
Akizungumza kwa mshangao mkubwa mbele ya wadau wa elimu, DC Mjema alisema ameshangazwa na shule hiyo kufanya ada nafuu, hivyo ni jukumu la wazazi na walezi kujitokeza kuwasomesha watoto wao kwa nguvu zote.
Alisema pamoja na ada hiyo kuwa nafuu, ni jukumu la serikali hususan Halmashauri ya Wilaya Temeke kupanga mbinu bora zinazoweza kuisaidia shule hiyo kwa hali na mali ili waweze kufanya kazi ya kutoa elimu kwa kiwango cha juu.
“Hii naweza kuiita shule ya sekondari ya mshangao hasa baada ya kuona unafuu wa ada yake, nikiamini kuwa Dunia ya leo kukuta unafuu wa namna hii unaonyesha namna gani kuna wadau wana mtazamo wenye maendeleo.
“Naomba wadau, walezi, wazazi na serikali kupanga namna wanavyoweza kuisaidia Twayyaibat ili waweze kuhakikisha kuwa vijana wetu wanasoma kwa bidii kwa ajili ya kujikwamua kiuchumi kwasababu Dunia ya leo elimu ni lazima,” alisema DC Mjema.
Naye Mkuu wa Shule hiyo, Juma Omari, alisema shule yao imekuwa na mafanikio makubwa kutokana na kutoa ufaulu wa kufurahisha, huku akiihakikishia serikali kuwa watajitahidi kuwapa mwanga wa kielimu watoto wanaosoma kwenye shule hiyo.
“Tangu shule hii ilipoanzishwa mwaka 1996 imekuwa na mafanikio makubwa kutokana na matokeo yake ya Taifa, hili linatufanya tuongeze bidii katika kufundisha wanafunzi wetu tukiamini ndio mpango sahihi,” alisema.
Katika hatua nyingine, DC Mjema alitumia muda huo kukabidhi vyeti vya kuthamini mchango wa wadau wanaoisaidia shule hiyo, huku waliopewa vyeti hivyo ni Skywards Construction, Yakubu Chamber&Associate, Mheshimiwa Adam Malima, Sheimar Kweigir, Zainabu Vulu, Alosco.
No comments:
Post a Comment