SHIRIKA la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC), limesema ujenzi wa mradi wa bomba la gesi kutoka Mtwara hadi Dar es Salaam, umekamilika kwa asilimia 94, ambapo umegharimu zaidi ya dola za Marekani bilioni 1.225.
Kaimu Meneja Mkuu wa Kampuni ya Gesi ya Taifa (GASCO), Kapuulya Musomba alisema hayo jana jijini Dar es Salaam wakati akitoa Taarifa ya Utekelezaji wa Ujenzi wa Miundombinu ya Gesiasilia kutoka Madimba-Mtwara, Songosongo-Lindi na Pwani hadi Dar es Salaam.
Alisema mradi wa bomba la gesi utakapokamilika, utapunguza gharama za utumiaji wa mafuta katika kuendeshea mitambo ya umeme. Alisema fedha za mradi wa gesi asilia ni za mkopo na mkandarasi ameshalipwa asilimia 81 ya ujenzi wa bomba hilo.
Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa TPDC, James Andilile alisema mradi wa bomba la gesi asilia utapokelewa Juni mwaka huu na kuanza kusambaza maeneo mbalimbali.
Lakini, alisema kikwazo cha usambaji wa gesi asilia kwa Dar es Salaam ni mipango miji. “Ujenzi wa vituo vya kupokelea gesi asilia Mtwara, Somanga Fungu Kilwa, Kinyerezi na Tegeta Dar es Salaam utakamilika mwishoni mwa mwezi huu,” alisema.
Alisema kwenye usambazaji kwa matumizi ya nyumbani, wanashirikiana na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na Taasisi ya Teknolojia Dar es Salaam (DIT).
Mwenyekiti wa Bodi ya TPDC, Michael Mwande alisema kukamilika kwa bomba la gesi asilia, kutasaidia usambazaji wa umeme vijijini katika maeneo mbalimbali.
Alisema mpaka sasa tayari magari 60 yanatumia gesi asilia. Nyumba 70 na baadhi ya taasisi pia zinatumia gesi. Pia, Megawati 300 za umeme huzalishwa kwa kutumia gesi asilia.
No comments:
Post a Comment