Friday 12 December 2014

WATAHINIWA KIDATO CHA NNE KUANZA MITIHANI RASMI

Wanafunzi 297,488 wa kidato cha nne katika shule mbalimbali nchini, wanaanza mtihani wa kuhitimu utakaokamilika baada ya siku 20 huku watahiniwa wakionywa kujiepusha na vitendo vya udanganyifu.
  
Idadi ya watahiniwa wa mwaka huu ni pungufu ikilinganishwa na ya mwaka 2013 uliokuwa na watahiniwa 367,399.

  Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Jenista Mhagama alisema juzi kwamba kati ya idadi hiyo, watahiniwa wa shule ni 245,030 na watahiniwa wa kujitegemea ni 52,458.
  Kati ya watahiniwa wa shule, wavulana ni 132,244 sawa na asilimia 53,97 na wasichanani 112,786 sawa na asilimia 46.03.
 Mhagama alisema  kati ya watahiniwa wa kujitegemea 52,458, wanaume ni 25,458 na wanawake ni 26,684.
  Alisema kati ya watahiniwa hao, 51 ni wasioona wakiwemo wavulana 37 na wasichana 14 na kwamba wenye uoni hafifu ambao huhitaji maandishi makubwa ni 356.
  Alisema kundi jingine ni la watahiniwa waliojiandikisha kufanya mitihani ya maarifa ni 14, 723 wakiwemo wanaume 5,940 na wanawake 8,783.
  Mhagama alizitaka mamlaka mbalimbali kuhakikisha kwamba zinazuia udanganyifu katika mtihani huo. 
  “Maofisa elimu na mikoa na kwenye halmashauri hakikisheni taratibu zote za mitihani zinafuatwa, zuieni mianya yote inayoweza kusababisha udanganyifu,” alisema.
  Mhagama alisema wanafunzi watakaobainika kufanya udanganyifu watachukuliwa hatua ikiwemo kufutiwa mtihani.
MWANANCHI.

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!