Wednesday, 10 December 2014

WAFUNGWA 4,969 WAPATA MSAMAHA WA RAIS


Rais Jakaya Kikwete (pichani), ametoa msamaha kwa wafungwa 4,969 wanaotumikia adhabu zao katika magereza mbalimbali nchini.

Taarifa ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mathias Chikawe, iliyotolewa jijini Dar es Salaam jana, ilisema Rais Kikwete amechukua hatua hiyo katika kuadhimisha miaka 53 ya Uhuru wa Tanzania Bara.

Katika msamaha huo, wafungwa 887 wameachiliwa huru na wengine 4,082 wamepunguziwa vifungo vyao na kubaki gerezani hadi watakapomaliza kutumikia sehemu ya adhamu zao.
Taarifa hiyo ilieleza kwamba Rais ametumia nafasi hiyo kutokana na madaraka aliyopewa chini ya ibara 45 (1)(d)ya katiba ya nchi.

Wafungwa watakaohusika na msamaha huo ni wale waliopunguziwa vifungo vyao kwa utaratibu wa kawaida chini ya kifungu 49(1) cha sheria ya magereza, wenye matatizo ya ugonjwa kama Ukimwi, kifua kikuu na saratani iliyo hatua ya hatari.

“Wafungwa wenye matatizo haya watathibitishwa na jopo la waganga chini ya uenyekiti wa mganga mkuu wa mkoa au wilaya,” ilisema sehemu ya taarifa hiyo.

Kundi lingine la wafungwa waliosamehewa wametajwa kuwa wazee wenye umri wa miaka zaidi ya 70, wanawake waliofungwa wakiwa wajawazito au watoto wanaonyonyesha na wale wenye ulemavu wa akili au kimwili.

Hata hivyo, msamaha huo hautawahusu watu waliohukumiwa kifo au waliobatilishwa na kuwa kifungo cha maisha.

Wengine ambao hawatakuwa kwenye msamaha huo ni wale waliofungwa kwa makosa ya biashara ya dawa za kulevya, rushwa, unyang'anyi na kutumia silaha, kubaka, ulawiti na unajisi.

Aidha katika kundi hilo wapo wafungwa wenye makosa ya kuwapa ujauzito wanafunzi, matumizi mabaya ya madaraka na ubadhirifu wa fedha za umma, biashara haramu ya binadamu na makosa ya ugaidi.

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!