Wednesday, 10 December 2014
TANZANIA YASUBIRI MAJIBU YA CHISSANO USURUHISHI WA ZIWA NYASA
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe (pichani), amesema, serikali inasubiri majibu kutoka kwa kiongozi wa jopo la usuluhishi wa mgogoro wa mpaka wa Ziwa Nyasa, Rais wa zamani wa Msumbiji, Joachim Chissano.
Chissano kupitia Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (Sadc) ndiye anayeongoza jopo la marais wastaafu wa Sadc kusukluhisha mgogoro huo wa mpaka kati ya Tanzania na Malawi.
Membe aliiambia NIPASHE kwamba wanamsubiri Chissano atoe taarifa kuhusu kikao kingine cha usuluhishi kama alivyoahidi Machi 21, mwaka huu.
Waziri Membe, alisema walimwandikia barua Chissano na kwa sasa kinachosubiriwa ni majibu.
Kwa mujibu wa Waziri Membe, katika barua hiyo, walimtaka Chissano kuitisha kikao cha usuluhishi kama alivyoahidi Machi 21, mwaka huu.
“Tumemwandikia barua mzee Chissano, msuluhishi wa mgogoro huo na tunasubiri majibu. Tumemtaka aitishe kikao cha usuluhishi kama alivyokuwa ameahidi tarehe 21 Machi mwaka huu,” alisema Waziri Membe.
Alisema mzee Chissano aliahidi kuzikutanisha pande hizo mbili kwa ajili ya kikao cha pili cha usuluhishi wa mgogoro huo baada ya serikali mpya ya Malawi kuundwa.
Hata hivyo, alisema kikao hicho hakikufanyika kama, hivyo waliona vyema kumwandikia barua hiyo kwa lengo la kumkumbusha kiongozi huyo.
Membe alisema kwa sasa wanasubiri majibu na baada ya kupewa taarifa wataeleza kuhusu kitakachoendelea.
Takribani miaka miwili iliyopita, aliyekuwa Rais wa Malawi, Joyce Banda, aliibua mgogoro huo baada ya kudai kuwa sehemu yote ya maji ya Ziwa Nyasa ipo upande wa nchi hiyo.
Hata hivyo, kwa mujibu wa sheria ya kimataifa, nchi mbili zinazotenganishwa na maji kila moja inamiliki asilimia 50 ya eneo la maji.
Hatua ya Banda ilizorotesha uhusiano wa kidiplomasia baina ya nchi hizo mbili na kulazimika kuwaomba marais wastaafu wa Sadc kupatanisha, baada ya upatanishi baina ya nchi hizo kushindikana
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment