Friday, 5 December 2014
MAPACHA WALIOUNGANA WAHITIMU KIDATO CHA NNE
Watoto mapacha waliozaliwa wakiwa wameungana kiwiliwili wilayani hapa, mkoa wa Iringa, wamemaliza elimu ya kidato cha nne katika Shule ya Sekondari ya Mtakatifu Maria Consolata, iliyopo kijiji cha Ilamba .
Maria na Consolata Kikoti waliozaliwa miaka 17 iliyopita katika Hospitali ya Misheni ya Kanisa Katoliki la Ikonda wilayani Makete na kumaliza darasa la saba mwaka 2010 katika Shule ya Msingi Ikonda na baadaye kufaulu kwenda shule ya sekondari.
Mwaka 2011 walikwenda kujiunga kidato cha kwanza Shule ya Sekondari ya Mtakatifu Maria Consolata iliyopo wilaya ya Kilolo na kumaliza masomo yao ya kidato cha nne mwaka 2014.
Kutokana na maumbile yao, masista wa Shirika la Consolata waliamua kuwasaidia na kuwachukua kwenda kusoma Shule ya Nyota ya Asubuhi ambayo hivi sasa imepewa majina yao na kuitwa Mtakatifu Maria Consolata inayondeshwa na kanisa hilo.
Mbali na kufurahia kuhitimu kidato cha nne, Maria na Consolata siku ya mahafali yao ya kuhitimu elimu ya sekondari siku hiyo pia waliadhimisha siku yao ya kuzaliwa na kufikisha umri wa miaka 17.
Akizungumza kwenye sherehe za mahafali hayo juzi, Mkuu wa Wilaya ya Kilolo, Gerald Guninita, aliishukuru serikali na wasamaria wema waliojitoa kwa hali na mali kuwalea watoto hao hadi walipofikia na kuahidi kuwa pamoja nao katika kufanikisha ndoto zao, huku akitoa ahadi ya Balozi wa Kenya nchini atakayetoa usafiri kwa ajili ya kuwapeleka shuleni.
Naye Mkurugenzi wa Shule na Kituo cha Maria Consolata, Sista Zita Danzero alisema wanafunzi wa shule hiyo wanalelewa kama familia moja.
“Jamii isiwafiche walemavu ndani kwani nao wanahaki ya kupata maendeleo kama watu wengine” alisema.
Wakizungumza kwenye mahafali hayo, Maria na Consolata, waliwataka wanafunzi wengine kusoma kwa bidii na kumtanguliza Mungu katika maisha yao.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment