Friday 5 December 2014

KUKU TOKA MAREKANI NA CHANGAMOTO KWA WATANZANIA

Mfanyakazi wa ZanChick akiingiza kipande cha kuku katika sehemu ya kuwekea viungo.

BIASHARA ya kuku visiwani Zanzibar ni moja ya biashara ambazo zinakua kwa kasi.


Kukua huko kunatokana na kuongezeka kwa uhitaji wake, kuanzia watu binafsi pamoja na hoteli za kisasa, hususan za kitalii ambazo zinaendelea kujengwa katika fukwe mbalimbali siku hadi siku. Hata hivyo, soko la kuku visiwani humo kwa sasa limetekwa na kampuni ya ZanChik, hatua ambayo imeleta pia changamoto kwa wafugaji wa wadogo visiwani humo.

Ingawa kampuni hiyo haijachukua soko lote la kuku visiwani, lakini kwa sasa ndio inayotamba kwa kuuza kuku wengi. Hata hivyo, uwekezaji wa kampuni hii umesaidia pia suala zima la ajira kwa vijana visiwani. Kampuni hii haiuzi kuku wa kisasa wanaofugwa hapa Tanzania isipokuwa wanatoka Marekani.
Kwa nini? Meneja Uendeshaji ZanChick, Andre De Lange, anajibu kwamba wangetamani sana kutumia kuku wanaofugwa hapa Tanzania, kwa sababu wanasaidia pia kupunguza gharama za usafiri, lakini tabu ni kwamba kuku wa hapa ni wadogo kwa kimo.
Anasema kuku wao ambao wamekuwa gumzo na kukubalika katika soko la Zanzibar kwa haraka sana, ni wakubwa na ladha yao ni nzuri pia. “Kuku wa hapa wa kisasa wana wastani wa kilo moja na nusu, lakini hawa kuku tunaoleta (kutoka Marekani) paja lake tu linaweza kufika kilo moja na nusu,” anasema.
Nini kinawashinda Watanzania kufikia viwango hivyo? Lange ambaye kampuni yake inatarajia siku za baadaye kuanzisha shamba darasa hapa nchini, anajibu kwamba, kuku wa Tanzania hawalishwi ipasavyo lakini wenzetu wa Marekani wanawalisha chakula kilichoboreshwa zaidi na cha kutosha.
Anasema watakapoanzisha ufugaji hapa Tanzania, mwanzoni watakuwa wanaleta chakula kutoka Marekani wakati mikakati ikifanyika ili kizalishwe hapa Tanzania. Mwandishi wa makala haya alitembelea ofisi za kampuni hiyo, ZanChick, ambapo alishuhudia mitambo ya kuwakatakata na kuwahifadhi kulingana na uhitaji.
Baada ya kuwakatakata, shingo zinawekwa katika paketi zake, firigisi, vipapatio, mapaja na hata vidari, kila kitu na paketi yake. Meneja huyo uendeshaji anasema kuku wakishawasili kutoka Marekani wanakuwa kwenye makasha maalumu, ndani ya ubaridi wa kutosha kisha wanalainishwa katika mashine kabla ya kuwekwa viungo.
Mwandishi aliona mashine kubwa ya kuwasafisha kuku hao, ambapo wakitoka kwenye mashine hiyo ndipo wanalainishwa. Kuhusu msaada wa kampuni kwa wafugaji wadogo, Lange anasema wameshaanza taratibu za kuwapatia chanjo, lakini lengo la baadaye ni kuona wafugaji wanazalisha kuku wakubwa.
Anafafanua kwamba chanjo mbalimbali zinatolewa kwa wafugaji hao wadogowadogo hupitia Wizara ya Mifugo na Uvuvi ambapo kwa mwaka huu pekee wameshatoa chanjo takriban laki sita. Mkurugenzi wa ZanChick, Issa Kassim ndiye anayefafanua kuhusu mkakati wa kuanza kuleta chakula cha kuku kutoka nje ya nchi na kukigawa kwa wafugaji wa kuku kwa bei nafuu, kabla hatua ya kuzalisha chakula bora kwa kuku haijafanyika hapa Tanzania siku za baadaye.
Imani ya kampuni hiyo ni kwamba chakula bora wanachotumia kuku hao wanaoagizwa kutoka Marekani kikitua visiwani utakuwa mwanzo wa kupatikana kwa kuku bora, wakubwa na wa kisasa zaidi. Lange anasema awali walikuwa wakiuza kontena mbili kwa miezi kadhaa lakini kwa sasa kwa mwezi wanauza kontena hadi tano, si kwa mahoteli pekee ya kitalii bali pia kwa wananchi wa kawaida wanaouza mitaani na kupata faida kubwa.
“Wateja wetu wakubwa ni hoteli za watalii. Yaani wanaagiza sana hawa kuku kwa kuwa wanawapenda kwani tunawaunga kwa viungo na pilipili manga,” anasema Lange. Fatma Said anasema kuwa amekuwa akifanya biashara ya kununua kuku hao na kisha kuwauza kwa vipande kwa rejareja.
“Kwanza unajua kuwa hawa kuku ni wakubwa sana, yani unakuja kuona kuwa paja moja ni kubwa. Sasa ninachofanya ni kwamba nikichukua, nakatakata vipande vidogovidogo na kuuza mishikaki ya kuku,” anasema Fatma. Anaongeza: “Mshikaki mmoja nauza kwa shilingi 500 au ikiwa mikubwa nauza sh 700.
Sasa hapo kama nimenunua paketi mbili za Sh 9,000 ina maana kuwa napata faida ya kutosha.” Musa Haji, Mzanzibari anayefanya shughuli zake Magomeni, Dar es Salaam lakini kwa sasa anafanya biashara ya kuku Zanzibar kwa mafanikio makubwa anasema kuwa kwake anaona kuwa ni vema ZanChick wakafungua pia tawi upande wa Bara.
Anasema biashara ya kuuza kuku hao wa ZanChick ni nzuri na imempatia faida lakini alipokuwa akitaka kuanza kuuza kwa upande wa bara amekuwa akikumbana na vikwazo mbalimbali, hususan ushuru.
Anasema ana imani kutokana na ukubwa wa kuku hao, akipata nafasi ya kuwauza bara anaweza kupata faida kubwa kwa kuwa akichukua paja la kuku analikata vipande viwili na bado mtu anakula anaridhika kuliko hata kuku wa kawaida wanaouzwa Dar es Salaam. “Mwanzoni sikujua kwamba hawa kuku wanatoka nje...
Lakini ninachotamani ni kuona utaalamu wa kufuga kuku wakubwa unafika Bara kwa sababu ninaamini ni kuku wale wale isipokuwa tunachozidiana ni utaalamu,” anasema Haji. Bila shaka, kama ZanChick wakifungua tawi Tanzania bara inaweza ikawa si habari njema kwa wafugaji wadogo, lakini ni changamoto kwao kuhakikisha kwamba wanaweza kufuga kuku bora na wakubwa. Kwa maelezo ya Lange, hilo linawezekana.

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!