Monday 8 December 2014

INTERPOL YAOMBA MSAADA KUMKAMATA JANGILI

Hatimaye Shirika la Polisi la Kimataifa (Interpol) imewapigia magoti Watanzania ikitaka msaada wao katika kumsaka mtuhumiwa wa kwannza katika kesi ya utoroshaji wanyamapori hai 100 kwa ndege ya jeshi la Pakistani kupitia Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro.

Hii ni mara ya kwanza kwa Interpol kuomba msaada huo baada ya mtuhumiwa huyo, Ahmed Kamrani kutoweka baada ya kubaini kuwa anasakwa kwa tuhuma za kutorosha wanyama hao kwa msaada wa raia wa Tanzania, ambao baadhi wamekamatwa na kesi yao inaendelea mjini Moshi.
Shirika hilo limetoa orodha ya watu tisa ambao limewaelezea kuwa ni waharibifu wa mazingira kwa kuhusika kwenye utoroshaji huo wa wanyama, wakiwemo twiga wanne na ndege wa aina mbalimbali, uliofanyika Novemba 24, 2014, tukio ambalo Interpol imelifananisha na hadithi ya Nuhu kuingiza viumbe kwenye safina kabla ya gharika.
“Hata tetesi ndogo tu, taarifa yoyote ndogo tu unayohisi itatusaidia ni ya muhimu na ina manufaa katika kuleta mwanga kwenye uchunguzi na ushahidi mwingine ambao polisi inao,” alisema Ioannis Kokkinis, afisa upelelezi wa masuala ya uharamia wa Interpol.
Interpol imefikia uamuzi wa kuwatafuta maharamia hao kwa udi na uvumba katika operesheni kubwa ya Infra Terra iliyoanzishwa Oktoba mwaka huu, ikiwalenga watuhumiwa wa uharamia zaidi ya 139 katika nchi 36 kote duniani, ikiwamo Tanzania.
Hata hivyo ni maharamia tisa tu, akiwemo Kamrani ndiyo wanaotafutwa zaidi kutokana na kuhusika katika uhalifu wa mazingira ambao unasababisha hasara kubwa kwa nchi husika. Akitoa maelezo hayo Novemba 21 mwaka huu, Kokkinis alisema taarifa itakayotolewa ni sawa na jozi mpya za macho ambazo zitatoa mwangaza mwingine katika uchunguzi huo.
Msemaji wa Interpol Tanzania, Kamishna Gustav Babile alisema Kamrani anatafutwa kwa kuwa alitoroka nchini baada ya kubainika kufanya uharamia huo.
“Tumemwekea bendera nyekundu katika mtandao, yaani popote pale duniani akionekana akamatwe,” alisema Kamishna Babile.
Alisema operesheni hiyo ni kubwa ambayo inajumuisha utafutwaji wa maharamia wengine tisa duniani. “Nia ni kuhakikisha kuwa tunawapata hawa na nchi zao zimeruhusu picha zao zitumike kwa umma ili wapatikane,” alisema
Baadhi ya wanyama hao ni twiga wanne, ndege filimbi wakubwa wanne, dik 20, ndege aina ya kori au tandawala wakubwa, wanaopaa umbali mrefu 10, swala 68 aina ya gazelle, na swala wengine 20 jamii hiyo, na swala 68 aina ya impala.
Utoroshwaji wa wanyama hao wenye thamani ya Dola 113,715 za Marekani, umelisababishia taifa hasara ya zaidi ya Sh170 milioni.
Interpol ilisema kuwa Kamran, ambaye ana umri wa miaka 29, anatafutwa kwa udi na uvumba kwa kufanya uharamia huo.
Mkuu wa kitengo cha Interpol cha wahalifu wanaotafutwa zaidi, Stefano Carvelli alisema Watanzania ambao wamemuona mtu huyo au wengine nane wanaotafutwa, watoe taarifa.
Alisema: “Kwa mfano, kama upo Afrika na mtu anakuambia mfanye biashara ya meno au hata kama iliwahi kutokea miezi sita iliyopita lakini mtu huyo anafanana na watu hao kwenye picha, basi atoe taarifa.”
Watu wengine wanaotafutwa ni Feisal Mohamed, raia wa Kenya, ambaye shehena yake ya meno 314 ya tembo (sawa na tani mbili) ilikamatwa, Adriano Giacobone (Italia) ambaye anatafutwa kwa kusambaza taka sumu, Ben Simasiku (Zambia), ambaye anatafutwa kwa kusafirisha pembe za ndovu.
Mwingine ni Bhekumusa Mawillis Shiba (Swaziland), anayetafutwa kwa ujangili wa faru, na Sergey Darminov, ambaye ni anatafutwa kwa kufanya biashara ya uvuvi haramu.
Interpol na Mpango wa Mazingira wa Umoja wa Mataifa, ulitoa ripoti yao inayoonyesha kuwa kwa mwaka huu, biashara haramu ya wanyamapori na uharamia wa mazingira kama uvunaji wa mbao kinyume na sheria umesababisha hasara ya Dola 70 hadi 213 bilioni kwa mwaka.
Kesi ya utoroshwaji wa wanyama ilisikilizwa kwa siku mbili mfululizo katika kipindi cha Machi 5 na 6 mwaka huu katika mahakama ya Hakimu Mkazi wa Mkoa wa Kilimanjaro, Simon Kobelo.
Sambamba na Kamrani, washitakiwa wengine katika kesi hiyo ya uhujumu uchumi ni pamoja na Hawa Mang’unyuka, Martin Kimath na Michael Mrutu ambao wote wako nje kwa dhamana.

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!