TAFITI Nchini zimeonyesha kuwa kila mwaka kumekuwa na ongezeko la kesi mpya za wagonjwa kansa ya tezi dume.
Utafiti uliofanywa na Taasisi ya Saratani ya Ocean Road (ORIC) umeonysha kuwa katika mwaka 2013 idadi ya kesi mpya za waliohudhuria taasisi hiyo ilifikia 115 kutoka 51 mwaka 2006.
Akizungumzia jana jijini Dar es Salaam, kuhusiana na uchunguzi wa hali ya tezi dume nchini, Mwenyekiti wa Hospitali ya Apollo yenye makao makuu nchini India, Dk. Prathap Reddy, alisema ugonjwa huo unaathiri wanaume wengi na kusababisha vifo kwa sababu ya ukosefu wa ufahamu wa kina juu ya ugonjwa huo.
Alisema utaratibu wa uchunguzi wa saratani ya tezi dume haufanyiki kutokana na gharama na ukosefu wa vifaa vya uchunguzi nchini.
“Watu wengi hufika hospitalini wakati ugonjwa huo upo katika hatua ya mwisho na hauwezi kuzuilika tena, hata hivyo, ugonjwa huo una uwezekano mkubwa wa kutibika endapo utagundulika mapema,"alisema.
Alisema licha ya kuwepo kifaa maalum cha utambuzi wa kansa ya tezi dume (PSA) duniani, Watanzania wachache ndio wenye uwezo wa kupata huduma hiyo.
“Tafiti zilizofanyika hivi karibuni zinaonyesha kuwa wanaume walio chini ya miaka 40 wana uwezekano wa kupata saratani ya tezi dume,”alisema.
Dk. Reddy, alisema kutokana na ugonjwa huo wameamua kuanzisha kampeni ili kukusanya fedha na kutoa mwamko wa ufahamu katika masuala ya afya kwa wanaume.
Kampeni hiyo itaitwa "masharubu" na "Novemba", ikiwa na lengo la kuongeza ufahamu na mwamko kwa kupima ili kugundua mapema kansa, utambuzi na matibabu ya ufanisi kwa lengo la kupunguza idadi ya vifo na hatimaye kuzuilika kabisa,”alisema.
Alizitaja sababu zinazosababisha saratani tezi dume ni miaka, historia ya familia, kabila, chakula, vinjwaji, uvutaji sigara, uzito, dawa na aina ya pili kisukari.
No comments:
Post a Comment