Sunday, 30 November 2014

RAIS JK ALIFICHA SIRI YA KUUGUA SARATANI



RAIS Jakaya Kikwete, amerejea nchini akiwa mzima wa afya na kuelezea Watanzania namna alivyoficha siri ya kuugua saratani kwa zaidi ya mwaka mmoja, huku akihamanika moyoni na siri hiyo.



Akizungumza katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere, jijini Dar es Salaam mara baada ya kuwasili jana, Rais Kikwete alisema Septemba 27 mwaka jana aligundulika kuwa na saratani katika hatua ya kwanza, ambayo inatibika.
Akifafanua alisema kabla ya ugunduzi huo, alifanyiwa uchunguzi mkubwa wa afya Septemba 24 mwaka jana, ambao ulikuwa ni sehemu ya mazoea yake ya kufanya uchunguzi wa afya, lakini ndio ikagundulika kuwa ana tatizo katika tezi dume, ambayo ilikuwa ikikua.
Kwa mujibu wa Rais Kikwete, madaktari walimwambia ni kawaida kwa tezi dume kukua, lakini kipimo chao chenye tarakimu moja mpaka 10 kikionesha hali iko juu ya nne, wanakuwa na mashaka na tezi dume hiyo.
“Kwangu kwa miezi sita, ilikuwa ikipanda kutoka 3, 4, 5,” alisema na kufafanua kuwa kupanda kwa kipimo hicho, kulionesha kuwa tezi dume yake ilikuwa na tatizo.
Kipimo cha saratani
Rais Kikwete alisema alifanyiwa kipimo kingine kwa kutoa nyama ndogo 14, ambapo Septemba 27 mwaka jana majibu yalitoka na kubainika kati ya nyama hizo, nyama mbili zilikuwa na seli za saratani na 12 zikakutwa salama.
“Niliwauliza sasa kinachotakiwa ni nini? Wakasema ni upasuaji unaofanywa kwa roboti tu, ambayo inatoboa mwili na kutoa kiungo chenye maradhi,” alisema Rais Kikwete.
Alisema alishauriwa kwenda kutafuta wazo la pili kwenye hospitali ya John Hopkins iliyopo Baltimore, nchini Marekani, ambapo kuna madaktari bingwa wa kupima hatua za saratani.
Katika hospitali hiyo pia, walimwambia ana saratani katika hatua ya kwanza ambayo inatibika kwa kufanyiwa upasuaji na kuondoa sehemu yenye tatizo, lakini hatua ya nne na tano ndiyo haitibiki.
Apiga kalenda upasuaji
Rais Kikwete alisema baada ya kuambiwa kuwa anatakiwa afanyiwe upasuaji, alishauri madaktari wasubiri mpaka Julai mwaka huu, kwa sababu alikuwa na majukumu yaliyokuwa mbele yake, hasa Desemba 30, mwaka jana ambapo alikuwa akitakiwa kupokea ripoti ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba Mpya.
“Walisema ni upasuaji mdogo tu lakini nikafikiria, hii inaweza kuwa dhana tu ya madaktari maana hujui watakuta nini, unaweza ukakaa sana… nikawaambia wasubiri tufanye Julai, wakashangaa,” alisema.
Alisema ilipofika Julai, muda aliokubaliana na madaktari hao kwenda kufanyiwa upasuaji, alitarajia Bunge Maalumu la Katiba liwe limeisha, lakini kwa kuwa alilazimika kuongeza siku 70 akashauriana na madaktari hao kwa mara nyingine kusogeza muda mbele hadi Novemba.
Kwa mujibu wa Rais Kikwete, madaktari hao walikubali, lakini hawakufurahia na walimwambia wazi kuwa anachezea maisha yake na kumuonya kuwa anayo nafasi ya kuondoa saratani hiyo, hivyo asisogeze mbele tena.
Mbali na onyo hilo, madaktari hao pia walimwambia kuwa saratani hiyo ikitoka nje, itashambulia mifupa hasa ya nyonga, ushauri uliosababisha afanye uchunguzi wa mifupa yake mara kwa mara.
“Ilikuwa hata nikiumwa kidogo tu, ninahofu isije ikawa ndio imetoka nje,” alisema Rais Kikwete. Siri Kwa muda wote huo, Rais Kikwete alisema alitunza siri moyoni mwake na hakumwambia mtu kuwa ana saratani na mara zote alikuwa akitabasamu na kucheka, huku akijua kuwa anaugua saratani.
“Nilikuwa nafanya kazi, lakini ndani ya moyo wangu, nilikuwa na mzigo mkubwa. Nilikuwa natabasamu wakati wote nikiongoza Baraza la Mawaziri, Halmasahauri Kuu ya Chama, huku moyoni nikiwa nimebeba mzigo.
Mke, familia “Sikumwambia mtu yeyote. Hata mke wangu tulikuwa tunaulizana mpenzi vipi, namjibu salama lakini najua huyu mama nimemficha kitu…nilikuja kumwambia baada ya miezi nane kwamba unajua ninaugua saratani, lakini usimwambie mtu. Namshukuru mke wangu, alikuwa na moyo wa ujasiri, akaniambia pole Mungu atakusaidia,” alisema Rais Kikwete.
Rais Kikwete aliongeza kuwa alimuomba mkewe amuombee dua kwa kuwa yeye ni mcha Mungu zaidi yake. Alisema ndugu zake, akiwemo kaka yake aliyemtaja kwa jina la Mzee Suleimani Kikwete na dada zake, aliwaambia siku nne kabla ya kuondoka nchini kwenda kutibiwa, na baada ya kuwaambia walionesha woga na kumtakia heri.
Pia alisema alimwita mwanawe Ridhiwani na kumwambia akae nalo asimwambie mtu kabla ya kuwaeleza wanawe wote. Siku tatu kabla ya kuondoka, ilikuwa siku ya Jumanne, Rais Kikwete alisema aliongoza kikao cha Baraza la Mawaziri na baada ya kumaliza kikao, kabla ya kutawanyika aliomba mawaziri wabaki, ili awaeleze jambo lake ambalo ni binafsi zaidi.
“Niliwaambia jamani kesho kutwa natarajia kusafiri kwenda kutibiwa saratani, wakaogopa wengine wakasema hata Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, aliondoka akitembea kwa miguu yake. “Niliwaambia nina mpango baada ya kuzungumza na wazee wa Dodoma, nitangazie Watanzania ugonjwa unaonisumbua na kwamba nakwenda kutibiwa Marekani,” alisema.
Hatua hiyo ya kutaka kuwaeleza Watanzania, Rais Kikwete alisema iliibua ubishani huku mawaziri wakipinga vikali asiwaeleze Watanzania ambapo Waziri wa Ujenzi, Dk John Magufuli, alimwambia ingawa Rais hapewi agizo, lakini katika hilo anaona mawaziri wampe agizo asiwaambie Watanzania.
“Mama Kabaka, (Gaudentia, Waziri wa Kazi na Ajira) tu ndiye alihoji kuna madhara gani kuwaeleza Watanzania, lakini wenzake walimtaka akae kimya,” alisema Rais Kikwete. Alisema baada ya kuzungumza na wazee wa Dodoma na kuelezea Sheria ya Kura ya Maoni, wengi walifurahia na busara ikamuelekeza kuwa angewaambia, angeharibu furaha yao.
Matibabu
“Kabla ya upasuaji nilikuwa na mzigo mkubwa sana moyoni na woga, nilijiuliza hivi watakuta nini, au watakuta imesambaa katika viungo vingine,” alisema.
Alisema alipofika katika hospitali hiyo ya John Hopkins, alifanyiwa upasuaji kwa kupigwa ganzi eneo la tatizo pekee na kushonwa kwa kutumia pini za chuma kama za kubania makaratasi, kwa kuwa wao wameacha kushona kwa nyuzi.
Baada ya siku tano, Rais Kikwete alisema uchambuzi wa kiungo kilichotolewa ulifanyika na kubainika kuwa saratani hiyo ilikuwa haijasambaa kwenda kwenye kiungo kingine.
“Habari hizi zilitia matumaini kwani kabla ya kufanyiwa upasuaji nilikuwa na mzigo mkubwa wa hofu kwani nilijiuliza iwapo nikipasuliwa watagundua nini,” alisema na kuongeza kuwa saratani hiyo ilikuwa imeshambulia asilimia 20 ya tezi.
Mapumziko
Alisema ingawa amepona kwa nje, lakini madaktari wamemwambia apumzike kwa wiki nne na kufanya shughuli ndogo na nyepesi na kupona kabisa ni baada ya miezi mitatu.
Rais alishauri Watanzania kuwa na tabia ya kukagua afya zao, kwani ni muhimu kwa ugonjwa wowote, kwani hata saratani ikiwahiwa inatibika na hapa nchini vipimo hivyo vinafanyika katika hospitali mbalimbali ikiwemo Hospitali ya Taifa ya Muhimbili.
Pia aliwataka wanaume wenye umri wa miaka 40 na kuendelea, kupima saratani ya tezi dume, kwani inasababisha vifo vya saratani kwa asilimia 9.7, huku saratani ya shingo ya kizazi ikisababisha vifo vya saratani kwa asilimia 26.5 na saratani ya matiti asilimia 11.3.
Shukrani
Rais aliwashukuru Watanzania wote waliomuombea dua wakiwemo viongozi wa dini zote, na kusema Mungu alisikia dua zao na atawalipa kwa neema na upendo wao.
“Watanzania walinifariji kwa kunitumia ujumbe wa maneno… nilipata zaidi ya ujumbe elfu tano pamoja na marafiki wote duniani,” alisema.

CHANZO: HABARI LEO

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!