Sunday, 30 November 2014

POLISI MNAWEZA KUDHIBITI VITENDO VYA VIBAKA HAWA!-MDAU



KWA muda mrefu kumekuwepo na taarifa za vijana wadogo, wanaounda makundi na kutengeneza vijiwe na kujiita majina mbalimbali huku wakihusishwa na vitendo vya kiuhalifu, kama vile ukabaji, uporaji na wakati mwingine kuvunja na kuiba.



Mengi ya makundi hayo, yanaundwa na vijana wadogo ambao muda wao mwingi huutumia vijiweni na kazi yao kubwa katika makundi hayo ni kufanya uhalifu mdogo wa uporaji na ukabaji.
Makundi hayo yalianza kwa majina mbalimbali, ikiwemo jina maarufu la Panya Road, watoto wa mbwa au mbwamwitu, na yamekuwa yakijikusanya na kuvamia eneo moja na kupora kila wanayemuona, ikiwemo kujichukulia mali katika eneo husika.
Makundi hayo yanapovamia sehemu, hali ya amani katika eneo husika huvurugika na kinachoendelea ni uhalifu na unyang’anyi wa kutosha, kwani wakati mwingine huvamia hadi sehemu za biashara, kama vile maduka na kupora.
Wakati Polisi ikiendelea kupambana na makundi hayo, hasa hilo la Panya Road na kujitahidi kuyadhibiti, ukweli unabaki kuwa bado makundi ya aina hiyo, yamejaa maeneo mbalimbali jijini Dar es Salaam na mengi yakiwa na malengo mabaya.
Na si makundi tu, pia yapo maeneo yanayofahamika kwa kukithiri kwa vitendo vya uhalifu na uporaji, ambayo kwa kweli Polisi inabidi ikaze buti kuyadhibiti. Maeneo kama vile Daraja la Selander, Jangwani na barabara ya Mandela inayopita malori mengi, vibaka wanajulikana na kuonekana.
Wakati hayo yakijulikana, juzi katika eneo la Mbagala Kongowe Mzinga, hali ya utulivu na amani ilibadilika baada ya kundi la vijana wanaojiita Black Americans, kuanza kuvamia watu na kuwapora huku wakiwatishia kwa visu.
Vibaka hao hata baada ya kujaribu kudhibitiwa na wasamaria, waliishia kufanya fujo kwa kuvamia mtaa na baadaye kuua mtu mmoja, jambo lililosababisha hasira kwa wananchi nao wakalipiza kisasi.
Ukweli ni kwamba iko haja sasa kwa Polisi kufanya operesheni kabambe katika maeneo yote, yanayojulikana kuwa na wahalifu wa aina hiyo na kuwachukulia hatua madhubuti.
Uwezo wa kuwachukulia hatua na kusimamisha vitendo vya uporaji, watu kuumizwa kwa kukabwa au kuchomwa visu na wengine kuuawa, unawezekana kwa kuwa maeneo mengi walipo vibaka hao yanajulikana.
Kwa mfano, tukio la Mbagala, kijana Mwalami aliyeuawa alionesha kufahamiana na vibaka hao, kwani aliweza kusaidia wanaoibiwa na kurejeshewa mali zao. Watu wa aina hiyo wapo wengi mitaani.
Polisi wanaweza kuwatumia na kusambaratisha makundi yanayotishia amani wananchi. Lakini, pia maeneo ya wazi kama vile Jangwani au barabara ya Mandela, vibaka hao ni maarufu na wamekuwa wakionekana mchana kweupe wakivizia malori na magari ya abiria ili waweze kupora.
Kinachoshangaza ni kwanini wanaachwa waendelee na vitendo vyao, ilhali wanajulikana na kuonekana. Inafahamika kuwa Polisi ilianzisha programu ya ulinzi shirikishi.
Ni vyema ikaanzia na miradi ya elimu kwa wananchi juu ya umuhimu wa kuwa wawazi na kuwabainisha wale wote wanaokwenda kinyume cha sheria katika maeneo yao.
Ni ukweli usiopingika kuwa endapo Polisi watavalia njuga suala hili, watafanikiwa kuwakamata vijana wote wasio na kazi maalumu, wanaoanzisha makundi kwa nia ya uhalifu kwa kuwa katika mitaa wanayoanzishia makundi hayo wanajulikana.
Suala hilo linahitaji ushirikiano mkubwa baina ya pande zote mbili, Polisi na wananchi kwa kufanyakazi kwa pamoja na kuaminiana ikiwa ni pamoja na kuweka mikakati ya namna ya kupambana na kundi hilo la vijana na kuwafikisha katika mikono ya Sheria.
Wakati umefika sasa kwa Polisi kuanza kulichukulia hatua suala hilo mapema kabla hali haijawa mbaya kwa kuhakikisha vijiwe vyote vyenye vijana wasioeleweka, vinachunguzwa na ikithibitika wanahusika na uhalifu wachukuliwe hatua kali. Tusisubiri hali iwe mbaya, watu wauawe, waibiwe na kujeruhiwa ndipo hatua zichukuliwe.

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!