Mtoto Careen Mpombo (4) (pichani), mkazi wa Gongo la Mboto jijini Dar es Salaam, yuko katika mateso makali kufuatia kusumbuliwa na figo moja ambayo haifanyi kazi.
Licha ya kuugua figo, mtoto huyo pia ana ugonjwa wa mafindofindo (Tonsillitis) unaomfanya akose raha kutokana kuwa na maumivu makali yanayosababisha ashindwe kula.
Akizungumza na gazeti hili, mama mzazi wa mtoto huyo ambaye pia huitwa Careen, alisema mwanaye alianza kuumwa kwa kuvimba mashavu akadhani ana mafindofindo hivyo aliamua kumpeleka katika Hospitali ya Kisarawe iliyopo mkoani Pwani.
“Hospitalini walimpa dawa ya PEN V na kumchoma sindano wakijua ni mafindofindo lakini kadiri siku sinavyozidi kusonga mbele ndivyo anavyozidi kuumwa.“Imefikia sasa anashindwa kulala kabisa, tulimrudisha hospitali baada ya kuona tumbo limeanza kuvimba, tukashauriwa kumpeleka Hospitali ya Taifa Muhimbili.
“Madaktari waliniambia nimpeleke Hospitali ya Regency kwa vipimo zaidi ambapo waligundua kuwa figo yake moja haifanyi kazi na ana mafindofindo, wakaniambia anatakiwa kupima kipimo ambacho atakatwa nyama gharama yake ni Shilingi 140,000,” alisema mama huyo.
Aliongeza kuwa, baada ya kuambiwa hivyo aliumia sana kwa kuwa alijua mtoto wake atazidi kuteseka kwa kuwa hana uwezo ya kupata kiasi hicho cha fedha kwa sababu mume wake alipata ajali ya gari na bado ni mgonjwa na yeye hana kazi na isitoshe anaumwa.
“Nilivyoambiwa nahitaji kutoa shilingi laki moja na elfu arobaini niliumia na kutoka machozi kwa kuwa nilijua wazi mtoto wangu atazidi kuteseka kwa kuwa sina fedha hizo, sasa nashinda nikilia, naomba Watanzania wanisaidie,” alisema mama huyo.
Kama umeguswa na habari ya mtoto Careen na unapenda kumsaidia, wasiliana na mama yake kwa namba 0657 628 889, KUTOA NI MOYO SIYO UTAJIRI.
No comments:
Post a Comment