Serikali imeiagiza Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB), kuwapa wanafunzi 1,107 wenye sifa waliokosa mikopo kwa kutokidhi mahitaji ya Bodi, fursa ya kurekebisha makosa kwa kujaza upya fomu ya maombi ili wapatiwe mikopo.
Kati ya wanafunzi hao wanaotarajiwa kujiunga na elimu ya juu mwaka huu, 111 wanachukua masomo ya Sayansi ya Tiba, 20 Ualimu wa Hisabati, 164 Ualimu wa Sayansi, saba Uhandisi wa Umwagiliaji, 617 Ualimu, 20 Sayansi ya Kilimo, 70 Uhandisi na 98 Sayansi.
Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Philip Mulugo, alitoa agizo hilo katika kikao kati ya Kamati ya Bunge ya Huduma za Jamii, watendaji wa Bodi na viongozi wa wizara hiyo, kilichofanyika katika Ofisi Ndogo za Bunge, jijini Dar es Salaam jana.
Mulugo ameiagiza Bodi kufungua tovuti zake na kuwaruhusu wanafunzi hao kuchukua fomu hizo kwa ajili ya kuzijaza upya. Alisema wanafunzi hao hawakukidhi mahitaji ya Bodi kutokana na fomu zao za awali za maombi ya mikopo kutojazwa vizuri.
Mulugo alisema wizara itatumia jumla ya Sh. bilioni 1.9 kutoka kwenye fedha zake walizotengewa kwa ajili ya Matumizi Mengine (OC) na Bodi itatumia Sh. bilioni 21 kutoka kwenye marejesho ya mikopo na OC, kuhakikisha wanafunzi hao wanapata mikopo.
Hata hivyo, alisema fedha hizo hazitahusu ada kwa wanafunzi hao. “Ada tutawaombea kwenye vyuo husika, tutalipa mwakani,” alisema Mulugo.
Alisema Sh. bilioni 1.9 zitatumika kwa ajili ya mahitaji ya chakula na malazi, Sh. milioni 221.4 vitabu na viandikwa, Sh. milioni 686.3 kwa mafunzo ya vitendo na Sh. milioni 221.4 kwa mahitaji maalumu ya vitivo.
Kauli hiyo ya Mulugo ilitolewa baada ya Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Margareth Sitta, kumtaka Naibu Waziri huyo kueleza hatua zinazochukuliwa na serikali baada ya wanafunzi 36 kati ya waliokosa mikopo kuwasilisha kilio chao kwa wabunge na kulala kituo cha mabasi.
Katika hatua nyingine, wakati vyuo vikuu nchini vimefunguliwa kwa mwaka wa masomo 2013/14, imebainika kuwa baadhi ya wanafunzi hawajaingiziwa fedha za mikopo katika akaunti zao.
Uchunguzi uliofanywa na gazeti hili katika vyuo vikuu vya Mzumbe (MU), Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (Sua), Chuo Kikuu cha Waislamu na Chuo Kikuu cha Jordan vyote vya mkoani Morogoro, umebaini kuwa fedha za mikopo ya wanafunzi hazijatumwa katika vyuo hivyo kutoka HESLB.
Katika Chuo cha Mtakatifu Augustine (Saut) cha Mwanza wanafunzi waliingiziwa fedha Oktoba 12.
“Karibia wanafunzi wote wamepata mkopo, isipokuwa wale wa mwaka wa kwanza, ambao fedha zao zilipelekwa vyuo vingine kutokana na ‘selection’ ya Tume ya Vyuo Vikuu (TCU) na siyo kosa la Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu. Ni vijana wenyewe kutokwenda walipo chaguliwa, lakini chuo kinafanya mpango wa kuwasaidia,” alisema mmoja wa wanafunzi wa chuo hicho.
Katika Chuo Kikuu cha St John’s cha Dodoma wanafunzi wameshaingiziwa fedha hizo.
Kwa upande wake, Rais wa Chuo Kikuu cha Dodoma (Udom), Shashi Andrea, alisema wiki iliyopita wanafunzi wa mwaka wa kwanza walikuwa wanasajiliwa na kwamba wataanza kuingiziwa fedha zao wiki hii.
“Hawa wengine wa mwaka wa pili na kuendelea wanatakiwa kuripoti Jumamosi na baada ya hapo ndiyo tutajua kama kuna wanafunzi ambao hawajapata mikopo au la,” alisema.
Wanafunzi wa vyuo vikuu vya Iringa, Ruaha na Mkwawa wamesema hawajaingiziwa mikopo. Katika Chuo Kikuu cha Ardhi (Aru) wanafunzi hawajaanza kupata mikopo wakati Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) wanafunzi wa mwaka wa kwanza ndiyo waliopata mikopo hadi jana.
Katika Chuo cha Sayansi na Teknolojia cha Dare s Salaam (DIT) hadi jana wanafunzi hawakuwa wamepata fedha za mikopo.
Imeandikwa na Muhibu Said, Christina Mwakangale na Elizabeth Zaya, Dar; Idda Mushi, Morogoro; Augusta Njoji, Dodoma na Godfrey Mushi, Moshi.
CHANZO: NIPASHE
Friday, 10 October 2014
WALIOKOSA MIKOPO ELIMU YA JUU WAHURUMIWA
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment