SERIKALI ya China itadhamini wanafunzi bora 10 wa kidato cha sita watakaofanya vizuri katika somo la hisabati kwa kuwa inaamini maendeleo yatategemea ukuaji wa sayansi na teknolojia miongoni mwa vijana.
Kauli hiyo ilitolewa juzi na Balozi wa China hapa nchini, Dk Lu Youqing wakati akikabidhi hundi zenye thamani ya Sh milioni 50 kwa Waziri Mkuu, Mizengo Pinda kwa ajili ya kusaidia shule ya wasioona ya Mvumi na ujenzi wa maabara katika Wilaya ya Chamwino mkoani hapa.
Alisema hakuna nchi iliyoendelea bila kukazania vijana kujifunza sayansi na teknolojia na sasa kutaanzishwa mashindano ya hisabati na watakaoshinda vizuri watapata udhamini na tuzo.
Aliitaka Tanzania kuzingatia sekta ya sayansi na teknolojia ili vijana wajifunze kwa wingi kozi hizo na kuwawezesha kuendesha maendeleo katika sekta ya sayansi.
Alisema tayari nchi hiyo ina programu nzuri ya kutoa udhamini kwa ajili ya Watanzania na wameamua kulipa nafasi eneo la sayansi na teknolojia kwa kuwapa udhamini wanafunzi 10 bora wa kidato cha sita watakaofanya vizuri katika somo la hisabati. Pia alisema kutatolewa tuzo kwa wanafunzi bora 10 wa shule za msingi watakaofanya vizuri katika somo la hisabati.
“Ni vizuri kutumia nguvu zote kuhakikisha sekta ya elimu inaleta ufanisi, China itaunga mkono juhudi za Tanzania na itatoa nafasi zaidi kwa wanafunzi kujifunza China na kutoa msaada ili kuinua elimu ya sayansi na teknolojia,” alisema.
Kwa upande wake, Pinda alisema wazo la kuwapa udhamini wanafunzi wa kidato cha sita ni zuri, lakini tuzo kwa ajili ya wanafunzi wa shule za msingi zianze kwanza na shule za Mkoa wa Dodoma na baadaye kusambaa nchi nzima.
Waziri Mkuu alisema atakuwa kiranja wa jambo hilo kuhakikisha kunakuwa na mafanikio kwa wanafunzi wanaojifunza hisabati.
Alisema kuna kampuni nyingi rafiki wa Kichina ambayo kuna umuhimu wa kukutanishwa ili kuweza kuanzishwa mfuko maalumu wa elimu wa sayansi na teknolojia Mkoa wa Dodoma.
Katika msaada huo, Ubalozi wa China ulitoa jumla ya Sh milioni 33.6 huku wafanyabiashara wa China wanaofanya kazi zao Kariakoo wakitoa Sh milioni 8.3 na Kampuni ya Sunshine Industries ikatoa kiasi kama hicho cha Sh milioni 8.3.
HABARI LEO.
No comments:
Post a Comment