Waziri Mkuu Mizengo Pinda amesema kuwa siyo jambo baya kwake kutajwa kutaka kuwania urais katika uchaguzi mkuu ujao 2015 na kwamba kujitokeza pia ni jambo jema.
Akizungumza katika mahojiano maalumu na gazeti hili nyumbani kwake mjini Dodoma juzi, ambapo alizungumzia mambo mbalimbali, Pinda alisema kuwa jambo la msingi kwa wote wenye nia ya kuwania nafasi hiyo ya juu ya uongozi nchini ni kutambua kuwa urais ni dhamana kutoka kwa wananchi na haupatikani kwa uamuzi wa anayegombea, bali taratibu za vyama na wananchi watakaopiga kura.
Pinda maarufu kama Mtoto wa Mkulima alisema pia kwamba ni muhimu kwa watu wanaotaka kuwania urais wasikiuke misingi ya haki kwa kuingilia mchakato na kuwadhoofisha watu wenye mamlaka ya kuchagua mgombea urais, bali waachwe ili wafanye uamuzi wa haki kwa manufaa ya taifa, huku akisisitiza kufuatwa kwa taratibu za Chama Cha Mapinduzi (CCM).(P.T)
"Kujitokeza ni jambo jema, kutajwatajwa nako pia ni jambo jema tu kwa maoni yangu. Ninachoweza kusema kikubwa, wote wanaotaka kwenda kwenye hiyo nafasi, rai yangu kubwa ni moja tu, watambue wanachotaka kwenda kufanya ni dhamana. Ni nafasi kubwa, lakini ni dhamana tu unapewa kwa niaba ya Watanzania wengine wote.
"Kwa hiyo basi, uamuzi wa nani atakuwa, hauwezi kuwa wa kwako wewe. Lazima tuuache mikononi mwa wale ambao kikatiba, kisheria na kadhalika, ndiyo wamepewa hilo jukumu. La msingi hapa sisi ambao tunataka kuingia kwenye dimba hilo, tuhakikishe hatuwadhoofishi katika kufanya uamuzi wao wa haki kwa vishawishi, kwa vivutio, tuache wafanye uamuzi kwa imani kwamba wanayemchagua atatufikisha pale ambapo tunataka," alisema Pinda.
Alifafanua: "Mimi sisomi sana mtandao, lakini wakati mwingine nalazimika kusoma, kwa msingi huo hakuna haja ya kurushiana maneno au kuchukiana kwa wanaotaka kugombea, kwani kati yao, hakuna mwenye uhakika wa nani atakuwa. Kila mmoja anasema nami nijaribu, unakwenda huko na moyo mweupe, kimtazamo ambapo unafanya kazi kihalali, kwa haki, kiuadilifu, lakini mwishowe tujue kwamba uamuzi unabaki kwa watu waliopewa dhamana ya kuteua mgombea katika hatua ya mwisho. Tukiwapa fursa hiyo, naamini tutapata kiongozi mzuri."
Hivi karibuni vyombo vya habari viliandika habari zilizodai kuwa Waziri Mkuu Pinda alitangaza nia ya kuwania urais katika Uchaguzi Mkuu ujao mwaka 2015, akiwa mkoani Mwanza. Wengine waliotangaza nia ya kuwania urais kupitia CCM ni January Makamba, ambaye ni Naibu Waziri wa Sayansi na Teknolojia, na Mbunge wa Nzega, Dk Hamisi Kigwangalla.
Wengine wanaotajwa katika mbio hizo ni pamoja na Waziri Mkuu wa zamani Edward Lowassa, Samuel Sitta (Spika wa Bunge Maalumu la Katiba), Waziri wa Sheria na Katiba, Asha Rose- Migiro, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais (Mahusiano na Uratibu), Steven Wassira, Waziri wa Mambo ya Nje na Uhusiano wa Kimataifa, Bernard Membe, Waziri Mkuu mstaafu, Frederick Sumaye na aliyekuwa Waziri wa Nishati na Madini, William Ngeleja.
Wingi wa wagombea
Akizungumzia wingi wa wanaojitokeza kutaka nafasi hiyo ya juu ya uongozi wa taifa kupitia CCM, Waziri Mkuu Pinda alisema kuwa siyo jambo baya akisisitiza kwamba jambo muhimu ni kuachia wenye dhamana ya kuchagua mgombea, lakini akasema tatizo linaweza kutokea iwapo makundi hayo yatagombana.
Alisema kwamba katika CCM siyo jambo gumu kurudisha pamoja makundi tofauti ya waliowania nafasi ya kuteuliwa baada ya mmojawao kuteuliwa na chama kukiwakilisha katika uchaguzi mkuu, huku akisisitiza kuwa kama makundi yatagombana na kutukanana ndipo ugumu hutokea.
"Changamoto zitakazojitokeza pengine kwenye chama ni namna ya kurejesha wale wote ambao walikuwa wana mtu wao waliyekuwa wakimfanyia kampeni. Hakuna tatizo kurudisha kundi, tatizo linaibuka tu kama kundi moja limekuwa linagombana na lingine," alisema na kufafanua:
"Kwa hiyo mnabaki kazi yenu kushambuliana, akija kupata mmoja, mwenzake anapata kigugumizi anasema; huyu si alikuwa akinishambulia, sasa nitawarudishaje kundini?
"Lakini kama wote tutakwenda na dhamira moja ni rahisi kusema, bwana mimi nilikuwa huku na sikufanikiwa, naomba tumuunge mkono bwana huyu ambaye amepewa dhamana na wenye mamlaka ambao ni wananchi, hapo ni rahisi. Tukifanya hili 'braza' hakuna mgogoro hata kidogo," alisema Pinda.
Nguvu yake ipo kwa Mungu
Alisema kwamba katika yote anayofanya siku hadi siku hana tumaini lingine zaidi ya kuwezeshwa na Mungu, akibainisha kuwa husali kila anapolala na kuamka salama, akikabidhi majukumu yake mbele ya Mungu ili amwezeshe kufanikiwa.
"Ni kweli mambo ni mengi, lakini kikubwa ambacho nasema, siku zote napata faraja katika kuamini nguvu za Mwenyezi Mungu. Mimi ndiyo imani yangu. Kila ukiamka salama unasema; ee Mwenyezi Mungu nashukuru leo umeniamsha salama, naomba leo unijalie niwezeshe kutekeleza majukumu yangu, hata kama nikitetereka lakini narudi kwa Mungu," alisema Pinda. Alitaja jambo la pili ambalo pia nguvu yake ni namna anavyoshirikiana na wenzake katika utendaji kazi wa siku kwa siku akiwa karibu na watendaji na wasaidizi wake aliowasifu kuwa wanamsaidia kwa kiasi kikubwa hata kubaini mambo na matatizo yanayojitokeza ambayo pengine yeye binafsi asingeweza kuyabaini. Pia ukaribu na watu mbalimbali na jamii ni mambo ambayo husaidia kujenga uwezo.
"La tatu, kwa sababu nimekulia serikalini, Ikulu, hata nilipopata ubunge nilipewa unaibu waziri wa Tamisemi pale Ikulu, baadaye waziri sasa Waziri Mkuu. Hili llimenipa uzoefu, kuijua Serikali na kuwa karibu na chama, kuniwezesha kukijua chama pia kuijua nchi kwa jumla na kuwa mwepesi kupokea ushauri. Kuwa tayari kupata ushauri kwangu siyo dhambi," alisema Pinda akihitimisha:
"Nadhani ukichanganya yote hayo na baraka zenu nyie mnaotutakia mema, nadhani mambo yatakwenda vizuri."
Chanzo:Mwananchi
No comments:
Post a Comment