Tuesday, 16 September 2014

KIKWETE: NIMETEKELEZA AHADI KWA ASILIMIA 80.





“HAKUNA wa kukisuta Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwani kimetekeleza sehemu kubwa ya ahadi zake kwenye ilani,” anasemwa Rais Jakaya Kikwete alipofanya ziara mkoani Dodoma hivi karibuni.
Anasema kwa kiasi kikubwa Serikali iliyopo madarakani inayoongozwa na CCM imetekeleza kwa vitendo ahadi zake na sasa miradi mingi ya maendeleo imewafikia wananchi.



 “Nisingependa Chama Cha Mapinduzi kisutwe kwa kushindwa kuwaletea maendeleo watu wake, lakini wa kusema na kuzoza wapo tu na kelele za mlango hazimzuii mwenye nyumba kulala,” anasema.

Kwa mujibu wa Rais Kikwete zaidi ya asilimia 80 ya ahadi alizotoa wakati anaingia madarakani zimetimizwa na zilizobakia atazimaliza kabla ya kuondoka madarakani. Anasema wakati anaingia madarakani mwaka 2005 alitoa ahadi mbalimbali katika maeneo tofauti zikiwamo zilizoandikwa katika Ilani ya CCM, ambazo zimeendelea kutimizwa kwa kadiri fedha zinavyopatikana.
Matumaini ya asilimia 100
“Sasa tumefikia asilimia 80 ya utekelezaji wa ahadi zetu. Naamini tunaweza kufanikiwa kwa ahadi zote na kama tutashindwa basi tutaacha kidogo sana, lakini kumbukeni tumetekeleza hata yale ambayo hayakuwa katika ahadi (kutokana na umuhimu wake),” anasema Rais Kikwete.
Anasema Serikali anayoiongoza itaendelea kutimiza wajibu wake mintarafu ahadi alizotoa wakati wa kuwaomba kura wananchi na kwamba hata mambo yatakayobaki yatakuwa na maelezo ya uhakika.
Dhana ya maisha bora
Anabainisha kuwa, dhamira ya Serikali ya kuinua maisha ya Watanzania iko pale pale na kwamba hilo linafanyika siyo kwa kuwajaza fedha watu mifukoni kama wengine wanavyofikiria.“Tunaposema kuinua maisha ya Watanzania wengine wanafikiri ni kumwaga fedha mifukoni mwao, uwezo huo haupo,” anasema.
Anafafanua kwamba dhamira ya kuwaletea wananchi maendeleo inaafikiwa kwa kupitia uboreshaji wa miundombinu mbalimbali ikiwemo barabara, shule, umeme, vituo vya afya na njia za mawasiliano ili kuwarahisishia wananchi katika kitimiza malengo yao ya maendeleo.
Ukusanyaji mapato
Anasema Serikali imeboresha ukusanyaji wa fedha za ndani ili kuongeza mapato na kupunguza utegemezi wa nje katika miradi ya maendeleo. Kadhalika anasema makusanyo ya mapato yameongezeka kutoka Sh bilioni 170 kwa mwezi hadi Sh bilioni 900 hivi sasa na kwamba ongezeko la fedha hizo linasaidia sana katika ujenzi wa barabara kwa viwango vya lami na hata zile za vijijini.
“Tumetimiza ahadi kwenye maeneo mengi na tunaahidi kuendeleza uwekezaji kwenye barabara, umeme na maji,” anasema. “Mwaka 2005 niliahidi kuongeza jitihada katika kukusanya mapato ya Serikali ili kuboresha upatikanaji wa huduma. Tutaendelea kuongeza fedha kwenye halmashauri kwa ajili ya ujenzi wa barabara na madaraja,” anasema.
Anabainisha kuwa, miongoni mwa mambo makubwa yaliyofanywa na Serikali ya Awamu ya Nne anayoiongoza ni ujenzi wa barabara za lami ambazo zimekuwa zikiunganisha mikoa na mikoa na nyingine zitakapokamilika zitaunganisha nchi na nchi na hivyo kuleta mapinduzi makubwa katika uchumi.
Katika ziara hiyo, Rais Kikwete alizindua ujenzi wa barabara ya Dodoma- Iringa inayotokea Dodoma hadi Fufu, yenye urefu wa kilomita 70.9. Pia alizindua ujenzi wa barabara kwa kiwango cha lami kutoka Mayamaya hadi Bonga yenye urefu wa kilomita 188.15. Mradi huo ni sehemu ya barabara kutoka Dodoma hadi Babati kupitia Wilaya ya Kondoa.
Kuunganisha nchi na zingine
Rais Kikwete anasema kufunguka kwa barabara kutoka Dodoma hadi Iringa na ile ya Dodoma hadi Babati kutakuza maradufu shughuli za kiuchumi na kupunguza umaskini kutokana na barabara hizo kuwa sehemu ya barabara kuu inayoanzia Cape Town, Afrika Kusini kupitia Tanzania hadi Cairo Misri, maarufu kama The Great North Road.
Anasema umuhimu wake si tu kwamba itaunganisha Dodoma na Iringa au Dodoma na Babati bali itakuwa kichecheo cha ukuaji wa shughuli za kiuchumi na kijamii katika Ukanda wa Nyanda za Juu Kusini na mikoa ya Kati na Kaskazini.
Pia anasema barabara hiyo itasaidia kuboresha maisha ya wananchi, kuongeza kipato na kuimarisha mawasiliano kwani sehemu ya barabara ya Dodoma hadi Iringa inaungana na barabara zinazounganisha Tunduma hadi Zambia na Namanga Mpakani mwa Kenya zinazounga barabara inayotokea Cape Town, Afrika Kusini hadi Cairo, Misri.
“Serikali itaendelea na jitihada za ujenzi wa barabara za lami kama njia nzuri ya kupanua shughuli za kiuchumi na kuendeleza dhana ya maisha bora kwa kila Mtanzania,” anasema. Anasema barabara ni njia kubwa ya wananchi kupata maendeleo na hivyo kukamilika kwa barabara inayounganisha Dodoma na Babati kwa mfano, kutapunguza mzunguko wa safari ya kwenda mikoa ya kaskazini kwani watu sasa watapitia Kondoa na si kulazimika kupitia Singida.
Katika ziara hiyo mkoani Dodoma, Rais pia aliweka jiwe la msingi kwa ajili ya ujenzi wa daraja la Gulwe Katika Wilaya ya Mpwapwa ambalo mpaka kukamilika kwake litagharimu Sh bilioni 3.3. Ujenzi wa daraja hilo kubwa le nye urefu wa nusu kilometa utakwenda sambamba na ujenzi wa madaraja madogo tisa ikiwa ni njia mojawapo ya kunusuru njia ya reli ya Gulwe na Godegode ambayo imekuwa ikisombwa na maji mara kwa mara.
Kwa mujibu wa Mtendaji Mkuu wa wakala wa Barabara Nchini (Tanroad), Patrick Mfugale, ujenzi wa daraja la Gulwe unatarajia kukamilika mwaka 2015 (soma kwa kina kuhusu daraja hilo Ijumaa). Mradi mwingine wa barabara uliozinduliwa ni ule wa barabara ya Mbande mpaka Kongwa ambapo Serikali imekusudia kuijenga kwa kiwango cha lami.
Barabara hiyo baadaye itaendelea kujengwa ikipitia Mpwapwa hadi Kibakwe. Wakati akiomba kura kwenye kampeni iliyofanyika wilayani Mpwapwa mwaka 2005, Mbunge wa Mpwapwa wakati huo, George Lubeleje, ‘alichomekea’ suala la ujenzi wa barabara hiyo ya Mbande - Kongwa na sasa mradi huo umeanza ili kutekeleza ahadi hiyo ya Rais.
“Kwenye ilani ya CCM ya mwaka 2010 – 2015 barabara hiyo iliingizwa kwenye upembuzi yakinifu lakini (nashauri) kwenye ilani inayokuja waingize ujenzi wa barabara yote ingawa kazi hiyo ni kubwa,” anasema Rais. Anaongeza: “Safari ni hatua, tutaangalia kama kutakuwa na uwezekano kuongeza barabara za ndani mbili au tatu katika Mji wa Kongwa kwani tumetimiza ahadi kwenye maeneo mengi.”
Naye Waziri wa Ujenzi, Dk John Magufuli, anasema mradi wa barabara kutoka Mbande hadi Kongwa ni moja ya ahadi katika ilani ya CCM. Anasema sehemu ya ujenzi wa barabara hiyo iliyozinduliwa ni kielelezo tosha kuwa Serikali imedhamiria kujenga barabara kwa ajili ya kuwaletea wananchi wake maendeleo.
Waziri Magufuli anasema barabara iliyozinduliwa ni sehemu ya barabara yenye urefu wa kilometa 101.7 ya kutoka Mbande hadi Kibakwe. Pia anasema ujenzi wa barabara iliyozinduliwa yenye urefu wa kilometa tano, asilimia 85 ya kazi yote imekamilika. Fedha za ndani Magufuli anasema barabara nyingi nchini zinajengwa kwa kutumia fedha za ndani kwa asilimia 100 bila kutegemea wafadhili.
“Tanzania ni moja ya nchi zinazojenga barabara zenye viwango bora kwa kutumia fedha zake za ndani,” anasema. Pia Serikali itatoa bilioni moja kwa ajili ya kusaidia ujenzi wa barabara za vijijini katika Wilaya ya Kongwa. Aidha anasema Serikali imetoa kiasi cha Sh bilioni 1.2 kwa ajili ya kukarabati barabara ya kutoka Chopogoro hadi Kibakwe ili iweze kupitika majira yote ya mwaka.
“Haya yote yanatokea kutokana na kujenga uhusiano mzuri kati ya wafadhili, na mafanikio katika sekta ya barabara yanaonekana wazi,” anasema Magufuli.
Waziri Magufuli anasema, mwenye macho hasiti kuona kwamba Serikali ya Awamu ya Nne imepiga hatua kubwa katika ujenzi wa barabara na madaraja isipokuwa kwa ‘wale ambao hawana macho’.Anasema kuanzia mwaka 2005 hadi sasa madaraja makubwa 2046 yamejengwa huku idadi ya madaraja madogo ikiwa ni 7546.
Kupunguza mwendo wa safari
Pia Waziri Magufuli anasema kukamilika kwa barabara Dodoma- Babati itasaidia sana katika kuiunganisha Tanzania na mataifa mengi ya Afrika na pia itasaidia sana katika kupunguza mwendo wa safari. Akitoa mfano, Magufuli anasema kutoka Babati hadi Dodoma (kupitia Singida) ni kilometa 421 lakini ukipitia njia ya Kondoa umbali unapungua hadi kilometa 260.
“Watu walikuwa wakisafiri kilomita 161 zaidi lakini kukamilika kwa barabara hii kutaokoa muda na fedha nyingi. Hii njia ni fupi lakini watu wanashindwa kupita kutokana na ubovu wa barabara. Mtu anaona ni bora kupita barabara ya kuzunguka japo ni ndefu. Ujenzi huu ukikamilika utapunguza gharama na muda pia,” anasema.
Makandarasi na ajira
Waziri Magufuli anawataka makandarasi kuwapatia kazi vijana ambao wako katika maeneo ambayo ujenzi unaendelea na si kuwatoa mbali, nje ya maeneo hayo. Kisha anawageukia vijana akisema: “Vijana mkipata kazi msiibe mafuta, mkiwa mnaiba mafuta mtachelewesha mradi.”
Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Barabara (Tanroards) Patrick Mfugale, anasema awamu nyingine ya ujenzi wa barabara itahusisha barabara ya Tunduru, Mangaka hadi Mtambalaswa yenye urefu wa kilometa 202.5. Anasema sehemu ya Mayamaya hadi Mela yenye urefu wa kilometa 99.35 itajengwa na Kampuni ya China Henan International Cooperation Group Company Limited (CHICO) kwa gharama ya Sh bilioni 100.14 na ujenzi utachukua miezi 36.
Pia barabara ya Mela hadi Bonga yenye urefu wa kilometa 88.8 itajengwa na Kampuni ya China Railway Seventh Group Company Limited kwa gharama ya Sh bilioni 83.39.
Anafafanua kwamba mradi huo unatekelezwa kwa fedha za mkopo kutoka Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) inayochangia asilimia 64.79, Serikali ya Japan kupitia Shirika la Maendeleo la Kimataifa (JICA) linachangia asilimia 32.83 na Serikali ya Tanzania inatoa asilimia 2.39.
Katika kuhakikisha utekelezaji wa ujenzi wa barabara ya Mayamaya, Mela hadi Bonga yenye kilometa 188.15 unakamilika, mradi umegawanyika katika sehemu mbili ambazo ni Mayamaya hadi Mela kilometa 99.35, na Mela Hadi Bonga kilometa 88.8.

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!